You are using an out of date browser. It may not display this or other websites correctly. You should upgrade or use an alternative browser.
Lissa Assenga
ZIMWI LIKUJUALO HALIKULI LIKAKWISHA!
Maisha ya binadamu ni kama safari katika msitu mnene wenye miti mingi sana.Wapo wanaovuka salama hadi ukingoni mwa msitu, na hukutana na ziwa kubwa lenye kina kirefu ambalo hakuna ajuaye siri iliyofichwa chini ya kina hicho. Ila cha zaidi ni kwamba kuna uwepo wa amani na utulivu. Cha kushtusha zaidi juu ya msitu huu ni kwamba licha ya kuwepo kwa wanyama wakali katika msitu huu, kuna mazimwi wakubwa na wakutisha waishio kwa kurubuni akili za binadamu na kuwapotosha na hatimaye kuwapoteza pasipo julikana.
Moja ya zimwi linalosemekana kuwa tishio kwa maisha ya binadamu, kwani limejaliwa nguvu za kipekee na uwezo wa ajabu wa kuwalaghai na kuwazamisha binadamu wengi wenye akili timamu katika giza totoro lililosukwa na miti mirefu, ni zimwi la ushoga na usagaji. Zimwi hili limekwapua akili za watu wa rika zote si vijana, si wazee. Idadi inazidii kuongezeka kwa kasi sana nchini na hata duniani.
Ushoga ni hali ya mwanaume kufanya mapenzi na mwanamume mwenzake na usagaji ni hali ya mwanamke kufanya mapenzi na mwanamke mwenzake. Watu wengi hasa vijana, tabia ya ushoga na usagaji imekuwa ikiwaathiri kisaikolojia na hata kupelekea waathirika kushindwa kuacha tabia hiyo kwa urahisi.
Kama wahenga walivyosema,”ukiona vyaelea… ujue vimeundwa” vivyohivyo, tabia hii ya usagaji na ushoga imekuwa na vyanzo na vichochezi vingi hasa katika karne za sasa ambapo dunia imekuwa kama kijiji. Ongezeko la vichochezi hivi hupelekea ongezeko kubwa la mahaini wa utamaduni wao wenyewe. Vichochezi hivi ni pamoja na;
Malezi mabovu kuanzia ngazi za chini za kifamilia hadi ngazi za kijamii. Malezi ya mtoto huanza tangu anapozaliwa amabapo mzazi anashughulika sana na ukuaji wa mtoto wa kimwili, kijamaa, kihemko utambuzi na kupotoka kwake. Wazazi wengi wa leo hawabebi jukumu hili la malezi ipasavyo na hata kujikuta wanakosa muda wa kujua mienendo ya watoto wao hivyo, tabia mbalimbali kama za ushoga na usagaji zinaanza kuchipua na kujijenga ndani ya mtoto. Hasa anapokosa mtu wa kumsaidia, hupelekea mtoto kuathirika na tabia hii na kuwa sugu kadri anavyoendelea kukua. Katika majumba mengi, wafanyakazi wa ndani ndio wanaobeba jukumu la kulea watoto. Ukizingatia kwamba wafanyakazi hao wa ndani wanakuwa na usuli tofauti wa kimaisha, wengi wao wanakuwa hawajaenda shule na wengine wana kuwa katika umri mdogo na hivyo kukusa upeo wa kutosha katika malezi ya mtoto na hata mtoto huishia kupotoka nakujiingiza katika tabia za ushoga au usagaji.
Mitandao ya kijamii kama vile`facebook`, `twitter`, `instagram` na `whatsapp` imekuwa mawakala wakubwa wa kuhamasisha vijana kuiga tabia hii ya usagaji au ushoga. Mitandao ya kijamii imewapotosha watu wengi hususan vijana kwani hutumia muda mwingi kutizama video, kuwasiliana na ndugu, jamaa na marafiki kutoka pande zote za dunia, kupata taarifa mbalimbali kutoka kwa watu mashuhuri ambao ni waathirika wa tabia hii ya usagaji na ushoga na hata kupelekea kuyaishi yale wanayoyaona na kuyapata kutoka kwenye mitandao hii ya kijamii. Watanzania wanakiuka utamaduni wao na kuiga yale yasiyofaa kutoka kwenye tamaduni zingine kama vile vijana wakiume kuvaa hereni na mavazi ya kike, vijana wa jinsia moja kuwa na uhusiano wa kimapenzi, watu kutaka kubadili jinsia zao.Hili ni chukizo kubwa kwa tamaduni la kitanzania.
Shinikizo la rika linalochochewa sana na ukosefu wa msimamo na hata kupelekea watu kuzidi kunasa katika mtego wa zimwi hili. Ushawishi na shinikizo liliopo katika makundi ya rika moja hasa shuleni na vyuoni umekuwa moja ya njia kuu inayopaisha ukuaji wa ushoga na usagaji katika jamii zetu. Mazingira ikiwemo watu na hali zinazowakumba watu huchangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa tabia za usagaji na ushoga. Hasa maendeleo ya kihemko yanapotokea kwa vijana wakiwa shuleni na hasa katika shule za jinsia moja, wengi wao hujikuta wakijiingiza katika vitendo visivyofaa kama vile kujiingiza au kushinikizwa kufanya mapenzi na watu wengine wa jinsia zinazofanana na hata kupelekea vijana hawa kuwa wafuasi wa zimwi hili hatari.Hivyo basi wananchi wote wanapaswa kuzingatia vipengele vifuatavyo ili kushinda vita dhidi ya zimwi hili ambavyo ni pamoja na;
Malezi bora yahamasishwe katika ngazi zote hususan katika familia na hata katika jamii. Wazazi wafuatilie kwa karibu kabisa ukuaji na mienendo ya watoto wao hasa wakati wa ukuaji .Hata wanapofika umri wa kujitegemea, wazazi na jamii wanapaswa kuwajenga vijana hawa katika hali ya kukubalika katika jamii. Wazazi wanapaswa kumjengea mtoto wao misingi mizuri ya kimaadili ambayo mtoto atakua nayo na hivyo kuwa vigumu sana kuweza kuathiriwa na shinikizo kutoka kwa kundi rika, kuiga tamaduni zisizofaa na hata kuweza kurekebisha na kuokoa wenzake wanaoangamia katika janga hili katika jamii inayomzunguka. Malezi bora ni muhimu sana hasa kwa watoto kwakuwa “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”.
Elimu ya jinsia itolewe kwa jamii kupitia nyanja tofauti tofauti kama vile vyombo vya habari (redio, runinga na katika mitandao ya kijamii). Mada hii ya tabia ya ushoga na usagaji ijadiliwe katika majukwaa ya hadhara. Madhara ya tabia ya ushoga na usagaji yawekwe bayana ili kuwafikia watu wengi katika kila kona ya Tanzania na ili kuweza kupunguza ongezeko la waathirika nchini.Elimu hii iingizwe katika mtaala wa shule ili vijana wote waliobahatika kwenda shule walazimike kupata elimu hii ya jinsia ili kuweza kujitambua na kuepukana na giza hili totoro.
Tunapaswa kudumisha na kukuza utamaduni wetu wa kitanzania. Hili ni pamoja na kupiga vita udhalilishaji wa kijinsia kama vile ulawiti unaotokea sehemu mbalimbali nchini na hata kuleta maafa makubwa kwa waathirika na hata kupelekea ukuaji wa tabia za ushoga. Kuweka taratibu za kuiburudisha na jamii kiakili nakimwili kwa Kutumia fani za sanaa vyombo vya habari, michezo, muziki wa asili na wa kisasa, filamu na televisheni na kuweka taratibu na itikadi zitakazochuja taarifa zitakazowafikia watu wa rika tofauti tofauti katika jamii.
Kuhamasisha na kutilia mkazo utoaji wa elimu na mafundisho mbalimbali ya dini. Kila muumini ahudhurie mafundisho ya kidini kulingana na dhehebu lake. Licha ya kufundishwa na kuyajua mafundisho ya kidini, wamini wafundishe na wahamasishwe kuyaishi yale wanayofundishwa katika jamii. Jamii nzima iwajibibike katika kulitokomeza zimwi hili hatari sana.
Hivyo basi, vita kali imetangazwa dhidi ya zimwi hili hatari ambaye anatokomeza na kupoteza maisha ya watu wengi sana. Kinachohitakika ni UWAJIBIKAJI,MSHIKAMANO THABITI,UCHAPAKAZI,MSIMAMO na KUTOKUKATA TAMAA kwani ZIMWI LIKUJUALO HALIKULI LIKAKWISHA !
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.