Dr. Chapa Kiuno
JF-Expert Member
- Sep 11, 2009
- 443
- 18
Thursday, September 24, 2009 10:28 AM
JUMLA ya mashahidi 17 wanatarajiwa kuieleza mahakama jinsi aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba na wenzake walivyoisababishia Serikali ya Tanzania hasara ya sh bilioni 11.7.
Ushahidi huo unatarajiwa kutolewa mbele ya mawakili wakiongozwa na Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, akisaidiana na Frederick Manyanda, Ben Lincoln, Tabu Mzee na Oswald Tibabyekomya, mbele ya jopo la mahakimu wakazi, John Utamwa, Saul Kinemela na Sam Rumanyika, jana alitaja orodha hiyo ya mashahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Mashahidi wanaotarajia kutoa ushahidi huo akiwemo aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Absalaam Khatib na aliyekuwa Kamishna wa Madini wa Wizara ya Nishati na Madini, Gray Mwakalukwa.
Wengine ni Maria Kyejo, Nakuela Senzia, Kesisia Mbatia, Bertha Soka, George Kaindoa, Nyero Hizza, Geogre Tigiti, Agrey Temba, P. J. Mlindoko, Neema Kitalu, Mustapha Ismail, Ludovick Kandege, Saddy Kambona, P. N. Kasela na Christine Shekidele.
Mashahidi watatoa ushahidi kwa upande wa Mahakama na bada ya mashahidi hao kuorodheshwa wakili Boniface aliuomba upande wa utetezi katika kesi hiyo nao kutaja orodha ya mashahidi wake na vielelezo watakavyovitumia katika kesi hiyo, kwa kuwa waraka namba 2 wa Jaji Mkuu wa mwaka 1999, unaelekeza upande wa utetezi kufanya hivyo.
Hata hivyo, ombi hilo la upande wa mashitaka liliibua mjadala ambapo wakili wa Mramba Hurbet Nyange alidai kuwa mteja wake hapaswi kutaja mashahidi wake wala vielelezo hadi upande wa Jamhuri utakapomaliza kutoa ushahidi.
Wakili Boniface nae alionekana kupinga maelezo yaliyotolea na wakili huyo mtetezi na kudai kwamba kifungu cha 231(1)(a) cha Sheria ya Kesi za Jinai, kinamtaka mshitakiwa atoe ushahidi na kuita mashahidi wake.
Hata hivyo, Hakimu Utamwa alilazimika kuingilia kati malumbano hayo na kuuhoji upande wa utetezi kama umesoma na kuuona waraka namba 2 wa Jaji Mkuu wa mwaka 1999, ili kujua unataka nini katika hatua za usikilizwaji wa awali wa kesi za jinai kama hiyo.
Mawakili wote wa upande wa utetezi walijibu kuwa hawajawahi kuuona, ndipo Hakimu Utamwa alipomtaka Wakili Mwandamizi wa Serikali, Frederick Manyanda, kuusoma kwa sauti waraka huo ili mawakili wa utetezi waweze kuusikia na kuelewa.
Kabla Manyanda hajaanza kuusoma waraka huo, wakili Nyange aliinuka na kudai kwa msisitizo kuwa hajauona waraka huo, lakini hata kama atauona na kuusoma, msimamo wake utabaki kuwa ule ule.
Mheshimiwa Hakimu, sijauona waraka huo, lakini hata kama nikiuona na kuusoma, msimamo wangu na mteja wangu upo pale pale, kwamba Sheria ya Makosa ya Jinai ndiyo sheria kubwa katika kesi za jinai kuliko waraka huo wa Jaji Mkuu, alisisitiza madai yake na kusababisha watu waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo kuangua vicheko.
Wakili huyo mtetezi wa mshitakwia namba moja aliendelea na msimamo wake na hakutaja mashahidi wake kwa kudai kuwa kuwataja mapema wanaweza wakarubuniwa na vitisho kwa upande wa serikali.
Kesi hiyo inaendelea leo mahakamani hapo.
</SPAN>
Na Pilly Kigome, Dar