SoC01 A hungry man, an angry man (Mwenye njaa ni mwenye hasira)

SoC01 A hungry man, an angry man (Mwenye njaa ni mwenye hasira)

Stories of Change - 2021 Competition

Langlang

JF-Expert Member
Joined
Jul 29, 2021
Posts
347
Reaction score
302
Kwa wale waliosoma vizuri somo la Kingereza, watakuwa wamekutana na huo usemi, a hungry man is an angry man – mwenye njaa ni mwenye hasira. Huenda ni kweli na hili linaweza elezewa vizuri na mtu aliyepitia mapito hayo. Na hapa sizungumzii ile njaa ya mchana mtumishi anayoipata akiwa kazini. Sio ile njaa ya siku moja ambapo mtu anapokosa mlo katika kipindi kile tumbo linapotoa mngurumo wa aina fulani anajisikia ana njaa. Nazungumzia pale inapofikia mtu kujidhalilisha kutokana na ukosefu wa chakula, anaenda kudoea chakula kwa jirani, kila siku na wakati mwingine akiwa na familia yake, kama anayo. Au anajizuia kudoea na kuzimia mara kwa mara kutokana na hiyo njaa.

Mtu anajikuta katika hali hii, mara nyingi, pale anapokosa uwezo wa kukidhi mahitaji yake na ya wanaomhusu ya chakula, iwe kutokana na ukosefu wa pesa, kuzidiwa na madeni au kukosa fursa za kuweza kujikimu – yaani umaskini. Umaskini husababisha kukosa elimu muafaka ambayo inasababisha udumavu wa uchambuzi yakinifu wa masuala muhimu ya maisha.

Ukiwa maskini unakosa chakula, ukiwa na njaa unakosa raha. Ukikosa chakula ukaishi na njaa, baada ya muda unaamua mambo unayoona yatakuletea chakula na raha – mazuri au mabaya. Baada ya maamuzi haya, haijalishi tena wanajamii watakufikiriaje ili mradi utakuwa umetatua tatizo lako, hususan la muda mfupi. Hii ni balaa, usiombe ikukute.

Viongozi wetu wamekuwa wakituhimiza tusikae vijiweni, tusichague kazi, tufanye kazi yoyote halali itakayoingiza kipato na watu wakaweza kujikimu. Kuna waliotekeleza hayo – wajasiriamali, wamachinga…nk. ambao baadhi yao, shughuli hizo zimewatoa kiuchumi na mambo yao yamewanyookea. Hii inadhihirishwa na wingi wa Wajasiriamali wadogowadogo na Wamachinga mitaani. Wako pia waliokwama.

Nilikuwa nazungumza na jamaa yangu aliyetoka Kahama hivi karibuni, akawa ananielezea fursa zilizoko kule, mate yakanitoka. Akanielezea mlo wa kawaida wa mchimbaji kuwa asubuhi anaweza anza na sima ya ugali wa nguvu au ikiwa ni chai inaendana na chapati kama saba hivi, mtu mmoja. Lengo kuu la wanaoishi huko ni dhahabu – kila mtu ni dhahabu, baas. Akasema kuna fursa za kilimo – alizeti, pamba, mbogamboga, mpunga, matikiti na hata uvuvi. Lakini pia akaelezea fursa zilizosahaulika za madini mbalimbali ya mabaki yatokanayo na uchenjuaji/uchimbaji wa dhahabu ambayo hayajafikiriwa kama eneo muhimu la uwekezaji. Anasema maeneo haya ni tosha kabisa kuwa sekta muhimu ya kuingiza pato la kutosha kwa taifa. Aliyoyasema ndugu yangu huyo hayatofautiani sana na niliyoyaona Mererani kwenye migodi ya Tanzanite.

Ukiwasikiliza wanasiasa wakizungumzia utajiri wa nchi hii, utawasikia wakitaja madini yaliyopo, maeneo ya kilimo, utalii, uvuvi na saa nyingine hata viwanda – na wanasema hizo ndizo fursa zenyewe, halafu wanaishia hapo. Tunao wanasiasa wahandisi, waliobobea katika masuala ya madini, kilimo, uvuvi, uchumi, sheria na kila kitu – yaani hatuna upungufu wa wataalam katika nyanja zote. Lakini tunakosa mawazo ya kitaalam ya jinsi tutakavyoachana na umaskini uliopiga kambi hapa nchini.

Tunapofikiria maendeleo ya maana hapa kwetu, utagundua wanasiasa wanazungumzia mabweni, madawati, vyoo vya mashule, zahanati, barabara…nk. Kila mahali anatozwa ushuru kwa kile wanachoita maendeleo. Ukipanda aisi ushuru, ukiingia sokoni na kapakacha ka maparachichi, ushuru, ukiangusha mti shambani kwako, ushuru…nk. Zinaanzishwa Mamlaka chungu nzima kushughulikia maushuru hayo. Unaposhindwa kulipa hayo maushuru, unaitwa mpinga maendeleo.

Inajulikana kuwa kila mtu mzima analipa kodi. Na mlipa kodi analo tegemeo kuwa kodi yake, haijalishi ni kidogo kiasi gani, itatumika kumletea maendeleo. Na kwa wanaoitwa wanyonge, maendeleo kwao yanajitokeza kama upatikanaji wa maji safi wanakoishi, barabara nzuri, upatikanaji wa madawa wanapougua, uwezo wa kusomesha watoto…nk. Kwa wanaoishi vijijini, mambo hayo yanayoitwa maendeleo huwa wanayaona wanaposafiri na kupita mijini. Na kwa maana hiyo, unapomuelezea habari za barabara za juu kwa juu, midege ya Boeng au kumjengea kiongozi sanamu au jumba la mabilioni, anajisikia kama vile kadhulumiwa, hayamhusu.

Kuna msemo fulani unaosema kuwa ni ujinga kujifunza kutokana na makosa yako ikiwa kuna uwezekano wa kuyatumia makosa ya wengine kujiendeleza. Sisi tunakwama wapi? Mabeberu wana viwanda vingi toka zamani na wamekuwa wakizalisha kila tunachohitaji huku wakijipatia mali ghafi toka kwetu. Dhahabu ni aina ya madini ambayo yamewasaidia mabeberu katika kuimarisha uchumi na sarafu zao il-hali huku kwetu yanaonekana ni madini kama yalivyo mengine.

Dhahabu yote izalishwayo inachukuliwa huku tukiambulia ka-mrahaba fulani tunakojivunia. Kwa mabeberu kitu kinachoitwa Gold Bullion kina umuhimu wake. Kwetu sisi chenye thamani ni Mrahaba!!! Kuna masimango yanayopita mitandaoni kuwa nchi yetu ni mojawapo ya nchi 10 zenye sarafu yenye thamani ya chini kuliko zote duniani, wakati dhahabu ipo, nchi 10 maskini duniani na nchi 10 watu wake wasio na raha duniani lakini pia ni mojawapo ya nchi zenye amani tele duniani. Tunajifariji, umaskini wetu unaendana na amani yetu. Inabidi tuendelee kujivunia amani. Mungu atupe nini!? Ni wazi sasa kuna mahali tumekwama. Je ni katika sera? Ni Mipango? Ni Siasa? Ni Uongozi?

Tumekuwa tukiambiwa na wanasiasa kuwa serikali inatekeleza sera za chama tawala kiasi kwamba inabidi tujiulize ikiwa kukwama kwetu ni kutokana na sera hizo?! Na kwa kuwa mipango ya maendeleo haitakiwi kupingana na sera, basi masimango yote yaliyotajwa yanaingia huko. Yaani siasa zimeunganishwa na mipango ya maendeleo. Na ikiwa hayo ni ya kweli, wataalamu wetu watuongoze namna ya kujikwamua kutokana na kilevi hicho, yaani kilevi cha siasa iliyochanganywa na sera.

Lakini pia labda ni Uongozi, kwamba wanaopewa dhamana hawajui walitendalo – kwamba wanapuyanga tu mara wapewapo dhamana na/au wanaopewa dhamana hizo, sio. Mfano rahisi, anayepewa ukuu wa mkoa ni Kapteni wa jeshi wakati mkuu wa wilaya ni Jenerali, niambie jinsi ambavyo kazi zitafanyika hapo. Na hili sio la ajabu hapa kwetu kwani hakuna vigezo rasmi vilivyowekwa, nani aajiriwe kama nani. Au inawezekana pia wanaopewa dhamana wanaamrishwa kutekeleza matakwa ya mamlaka ya uteuzi wao kiasi kwamba wanatakiwa kuimba mapambio ya kumsifu na kumtukuza kila wakati. Hili nalo linawezekana na linasababisha kutetereka kwa ubunifu katika uongozi mahali popote.

Huenda ni wakati sasa wataalamu wetu wakaonyesha makucha yao. Nchi za mabeberu wanaotusaidia kuendesha nchi, na hili halina ubishi, mipango ya muda mrefu huzindikwa na wataalamu na haibadilishwi na kiongozi yeyote kwa matakwa yake. Wanapochaguliwa hutekeleza mipango waliyoikuta. Hapa kwetu kila anayechaguliwa huja na mipango yake iitwayo sera. Mfano rahisi, katiba inayoitwa ya Warioba iliasisiwa na chama tawala. Ikatumia mabilioni ya fedha za walipa kodi – maskini kwa matajiri, lakini ilipofikia kila mtu anapajua, kwa masikitiko makuu. Na kwa kuwa mifumo iliyopo haina mbavu za kuwajibishana, viongozi hawashindwi kuchezea kodi za walipa kodi kwa manufaa yao.

Kuna habari kwamba wengi wa wataalamu wetu wanapenda kuwa wanasiasa zaidi kuliko fani zao za kitaaluma kiasi kwamba, utawakuta ma-profesa na ma-dokta wengi wanaolilia siasa kwa sasa kuliko zamani. Huenda hii inatokana na ukweli kwamba hapa nchini, siasa inalipa kuliko fani yoyote ile na anapoingia hakuna hatari wala athari yoyote itakayomkabili. Mshahara mnono na marupurupu tele. Ni raha tu.

Zipo taarifa kwamba Tanzania imejaliwa madini ya kila aina – kuanzia almasi, dhahabu, gesi, mafuta, uranium… hadi makaa ya mawe. Yametapakaa kila mahali lakini tunachosikia zaidi ni dhahabu, almasi na tanzanite. Thamani ya gesi inazidi kutoweka masikioni petu, sijui kwa nini. Ni nini hasa tofauti yetu na mabeberu katika kuleta maendeleo? Wao wana nini ambacho sisi hatuna? Wanachopanga wao kinafanikiwa, chetu kinakwama, je, ni vipaumbele vyetu ndio vya hovyo? Ni wataalamu wetu ndio hawajui kazi zao? Kuna uhusiano gani kati ya kupanga na utekelezaji wa mipango kwao ili sisi nasi tuwaige? Mimi naamini kuwa tunao wataalamu wa kutosha, tatizo ni jinsi gani ya kuwatumia walete mabadiliko chanya katika jamii.

Tunao wabunge wanaotembelea maeneo yao na kufanya mikutano ya mara kwa mara na wapiga kura wao. Kuna wanaokusanya kero zao na kuahidi kuzifanyia kazi lakini ni kwa kiwango gani wamefanikiwa kutatua kero hizo? Wanao uwezo gani wa kutekeleza nia zao njema kwa manufaa ya wananchi? Mfumo ulioko unaruhusu vipi wakamilishe ndoto zao za kuwafikishia wapiga kura wao maendeleo?

Tukubaliane kuwa ikiwa mwakilishi wa wananchi anashindwa kutekeleza matakwa ya wapiga kura wake, basi mfumo unahitaji mabadiliko. Nje ya hapo tutakuwa tunapiga bla-bla na kuwalaghai waTanzania. Je, ni njia ipi rahisi ya kubadilisha mfumo butu kama huo? Je, ni kupitia katiba? Kutumia Bunge? Kutegemea matakwa ya Rais? Hapa nchini, CCM imepinga matumizi ya Katiba hivyo kuachia Bunge au Rais. Ni vipi mamlaka hizi zitafanikisha majukumu haya? Zitaweza? Mimi sidhani.

Tukubaliane kwamba, ikiwa masimango tajwa hapo juu yana ukweli, na ikiwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwa ni pamoja na ujinga na umaskini, wananchi wamedumisha amani, ni kweli pia watakuwa wanagugumia ndani kwa ndani kutokana na machungu wayapatayo kwa madhila yanaowakabili. Je, watayavumilia machungu hayo hadi lini? Je, hatupaswi kujua kuwa uvumilivu huwa na kiwango na kikomo? Je, nini hatma ya kikomo hicho?

Viongozi wasibweteke. Yapo matukio katika nchi mbalimbali ambapo viongozi walijisahau wakidhani umaskini na ujinga walionao wapiga kura wao ni kinga kwao halafu ghafla hasira za wananchi zinajitokeza na mambo yanaharibika mazima.

Nimalizie kwa kuiasa serikali yetu kuwa makini na mipango mbalimbali inayoitekeleza kuwa waepukane na mipango inayobadilika-badilika kila awamu inapoingia kazini. Na wanapozungumzia maendeleo, mipango iwe inazungumzia kodi kama chanzo cha malipo ya sekta zote zihusuzo maendeleo. Hizo tozo/ushuru zisizo na kichwa wala miguu ambazo zinawatesa wananchi wanaponyang’anywa mali zao kwa kisingizio cha kutochangia maendeleo zifike mwisho. Zinaongeza umaskini, zinapunguza raha na kupunguza nguvu zake za manunuzi. Haya yanapotokea, anakabiliwa na njaa na anakabiliwa na msonononeko usio wa kawaida. Mtu wa aina hii hujawa na hasira tele.

Hadi hapo naamini watu wa vijijini tunaelewana. Mungu atubariki hadi mwisho.

LANGLANG
 
Upvote 1
Back
Top Bottom