Abdallah Said Kassongo kiongozi wa TANU Youth League Tabora 1958

Abdallah Said Kassongo kiongozi wa TANU Youth League Tabora 1958

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
1545853613128.png

TANU Youth League ya Tabora chini ya uongozi wa Abdallah Said Kassongo ilikuja kuwa tawi hodari sana na lenye mipango mikubwa Tanganyika nzima.

Kassongo na wanachama wengine wa TANU Youth League, Zena bint Malele, Jaffari Idd (aliyekuwa mpishi wa Nyerere katika mkutano wa kura tatu), Juma Salum Kisogo na Shaban Rukaya kwa juhudi zao wenyewe bila kutaka ushauri wa viongozi wa TANU Tabora, waliamua kuwaleta Nyerere na wajumbe wengine wa PAFMECA hadi Tabora kuja kufanya mkutano wa hadhara. Nyerere Tom Mboya, Francis Khamis, Kanyama Chiume na Dr. Kiano walikuwa Mwanza wakihudhuria mkutano wa PAFMECA.

Jaffari Idd alikwenda kwa mfanya biashara mmoja wa kihindi mjini Tabora, Rajabali Hirji, kumuomba aiazime TANU gari yake kwenda Mwanza kumchukua Nyerere na kumleta Tabora.

Hirji alikuwa ndiyo kwanza amenunua gari mpya ya Kimarekani, Chevrolet. Hirji kwa furaha alikubali na vijana wakaondoka kwenda Mwanza usiku ule ule.

Pale Nzega mfanyabiashara mmoja wa Kiarabu, aliyejulikana kwa jina moja la Yahya alijitolea petroli kwa ajili ya safari nzima ya kwenda Mwanza.

Walipofika Mwanza Kassongo alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa Paul Bomani kuuliza habari za Nyerere.

Bomani alimjulisha Kassongo na wenzake kuwa Nyerere na wageni wake wote walikuwa wakikaa Mwanza Hotel katikati ya mji. Nyerere alipotoka nje ya Mwanza Hotel na kuliona lile gari kubwa la Kimarekani lililokuwa likingíaa lenye herufi kubwa, ‘’TANU Youth League,’’ zimebandikwa ubavuni mwake, alifurahi sana na akatabasamu kwa furaha.

Vijana wa TANU walikuwa wamechoka kwa safari.

Pale pale Kassongo alimwambia Nyerere kwamba walikuwa wametoka Tabora kuja kumchukua yeye na wajumbe wa PAFMECA kuwapeleka Tabora kukutana na kuwasalimu wananchi.

Nyerere na ule wajumbe wote wa PAFMECA walikubali kwenda Tabora ijapokuwa safari hiii haikuwa katika ratiba yao. Bomani alimpigia simu Rajab Saleh Tambwe, mwenyekiti wa Mkoa wa TANU Tabora kumjulisha juu ya kuwasili kwa waheshimiwa katika wilaya yake jioni ile.

Walipokuwa njiani kwenda Tabora msafara ulisimama Nzega ambapo tawi la TANU chini ya Rashid Nyembo uliwapokea kwa ngoma ya Kimanyema iitwayo Kisonge.

Wajumbe wa PAFMECA waliwasili Tabora jioni sana na walipelekwa moja kwa moja hadi Parish Hall ambako umati mkubwa ulikuwa ukisubiri kuwapokea.

Siku iliyofuata TANU ilifanya mkutano mkubwa kiwanja cha ndege cha zamani ambapo Nyerere, Francis Khamis na Kanyama Chiume walitoa hotuba. Tom Mboya, kwa sababu zisizojulikana, alinyimwa ruhusa na serikali kuhutubia.

Huu ulikuwa mkutano wa pili mkubwa uliohutubiwa na Nyerere tangu ule uliofanyika Soko Kuu la Tabora mapema mwaka ule baada ya Kura Tatu, siku Nyerere alipotokwa na machozi ya uchungu.

Siku hii itaingia ndani ya historia ya Tanganyika kuwa ni siku ambapo mwimbo maarufu wa Kinyamwezi uliimbwa, mashairi yake yakiwa yamebadilishwa kwa Kiswahili kuwa, ‘’TANU Yajenga Nchi.’’

Mwimbo huu uliimbwa kwa mara ya kwanza katika viwanja hivi.

Huu ulikuwa wimbo wa ushindi wa vita ukiimbwa hapo zama na Wanyamwezi wakitoka vitani.

Kuwako kwa wanasiasa wazalendo wa Afrika ya Mashariki na Kati wakiwa wamekusanyika pamoja na wote wakizungumza kwa kauli moja wakiitaka Uingereza kutoa uhuru kwa makoloni yake yote barani Afrika, kulitia imani zaidi kwa watu nchini Tanganyika na nje ya mipaka yake.

Kwa TANU Youth League Tabora, hadhi yake ilipanda zaidi mbele ya Nyerere na kwa makao makuu ya chama mjini Dar es Salaam.

(Kutoka kitabu ''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924-1968)...'')
 
Kwa kweli umenirudisha mbali sana kwani nawakumbuka vizuri kina Nyembo na Tambwe
Historia nzuri sana
 
Kwa kweli umenirudisha mbali sana kwani nawakumbuka vizuri kina Nyembo na Tambwe
Historia nzuri sana
Aisee sisi tumekuwa tukisikia tu kwa nyembo kumbe hili jina linahistoria.
Kuna huyu anaitwa nyembo sijui ni mjukuu au ni mtoto mpaka leo utasikia nakaa Ipuli kwa nyembo.
 
Aisee sisi tumekuwa tukisikia tu kwa nyembo kumbe hili jina linahistoria.
Kuna huyu anaitwa nyembo sijui ni mjukuu au ni mtoto mpaka leo utasikia nakaa Ipuli kwa nyembo.
Mzee alikuwa maarufu sana Mungu amrehemu
Nawakumbuka sana wazee hao walipigania uhuru
Ndio wakombozi wetu na hao watakuwa wajukuu wake.
 
Back
Top Bottom