Abdul Nondo: Mikopo ya Wizara kuna ubabaishaji, nimeomba mkopo mwenyewe, wameandika tumeomba Watu 10

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
5,352
Reaction score
15,876
Your browser is not able to display this video.
SUALA LA MIKOPO KWA VIJANA CHINI YA WIZARA YA MAENDELEO YA VIJANA BADO NI CHANGAMOTO
Ngome ya Vijana ACT Wazalendo tumeona inayoitwa orodha ya wanufaika wa maombi ya mkopo kupitia mfuko wa Maendeleo ya Vijana chini ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana iliyotolewa tarehe 28 Aprili, 2026.

Itakumbukwa kuwa Ngome ya Vijana ACT Wazalendo tuliongea kupitia vyombo vya habari tarehe 21 Aprili, 2026. Tulieleza umma ya kwamba Ngome ya Vijana ikiongozwa na mimi kama mwenyekiti na Vijana wengine zaidi ya 25 na Vijana wengine tunaowafahamu tuliomba mkopo huu kila mmoja kwa namna yake kwa lengo la kuona mchakato wa maombi na changamoto zinazojitokeza.

Katika hatua ya maombi ya mkopo huu, tulishuhudia changamoto kadhaa, ikiwemo Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kugoma kuwaandikia Vijana barua za utambulisho kwa sababu vijana wengi walitakiwa kuonesha eneo wanalofanyia biashara ikiwa Vijana wengi ndio walikuwa wanaanza biashara, changamoto nyingine ni muda wa maombi ya mkopo kuwa mfupi, ukosefu wa taarifa na uratibu usioeleweka.

Jana, tarehe 28 Aprili, 2026 Wizara ya Maendeleo ya Vijana imetoa orodha ya wanaoitwa wanufaika wa mkopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ikiwemo na mimi Abdul Omary Nondo katika orodha hiyo ambapo wanasema bado hatua ya benki wakiendelea kuchambua. Kiasi kilichoidhinishwa kwangu ni shilingi milioni 50 zilizoombwa kwa ajili ya biashara ya ununuzi na usambazaji wa viazi mviringo.

Kwa jicho la harakaharaka unaweza kudhani hii ni hatua njema na kwamba suala hili la mikopo ya vijana chini ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana ni halisia. Hata hivyo, Ngome ya Vijana ACT Wazalendo tunapoitathmini hatua na mchakato mzima wa Wizara tunauona kama mchakato uliojaa ujanjaujanja na ubabaishaji kwa Vijana na suala zima la uwezeshaji vijana.

Tunaendelea kusisitiza na kuitaka Wizara ya Maendeleo ya Vijana iwe "Serious" katika mambo yanayohusu Vijana hasa uwezeshaji na Mikopo kwa vijana bila kuingiza Propaganda. Ni vyema tuelewe ya kwamba mimi Abdul Omary Nondo kupewa mkopo

huu haimaanishi ya kwamba nina sifa na vigezo bora zaidi kushinda vijana wengi waliokosa, kwani ninawafahamu vijana wengi wenye sifa na vigezo stahiki zaidi yangu ila wamekosa mkopo huu. Mimi ninaamini ya kwamba Abdul Omary Nondo kuorodheshwa kupewa mkopo huu ni kama njia ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana kutaka kuonesha umma kwamba mikopo ipo na Vijana wamepewa ikiwa hakuna uhalisia, kwa hoja zifuatazo;-
  • Mkanganyiko katika Idadi ya Wanufaika;
Wizara ya Maendeleo ya Vijana kupitia Waziri Joel Arthur Nnauka katika kitabu chake cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 13 alisema Bungeni hadi kufikia tarehe 3 Aprili, 2026 Vijana takribani 30,384 walikuwa wameomba mkopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, ambapo Ngome ya Vijana tulisema bado ni idadi ndogo sana ukilinganisha na idadi ya Vijana wenye uhitaji wa uwezeshaji na Mikopo, iliyotokana na masharti na vigezo vigumu, taarifa hafifu, muda mchache na uratibu usioeleweka.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana ya jana tarehe 28 Aprili, 2026 Wizara inasema Vijana wanufaika waliopewa mkopo ni Vijana takribani 1,961 sawa na 6.45% ya walioomba ambao ni vijana 30,384. Takribani vijana 28,423 wakikosa.
  • Walioomba Binafasi Wanasomeka Kikundi;
Lakini jambo la kusikitisha zaidi hata idadi ya vijana hao 1,961 wanaoitwa ni wanufaika wa mkopo kwa taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Maendeleo ya Vijana jana sio taarifa sahihi kwasababu walioomba binafasi wamewekwa kwenye orodha kama kikundi cha watu ilihali maombi yao hayakuwa ya kikundi.

Mfano, Mimi Abdul Omary Nondo niliomba mkopo mwenyewe sio kikundi. Na taarifa ya wizara iliruhusu kuomba mtu mmoja au kikundi. Lakini kilichonishangaza ni kuona katika orodha hiyo eneo la jina langu kuongezewa idadi ya watu 10 ambapo wanaume ni 7 na wanawake ni 3 ambao wote hawa siwajui, na wanaitwa wanufaika wa mkopo. Hili limejitokeza katika kila jina la mtu aliyepewa mkopo mbele kuna wanaoitwa idadi ya wanufaika ambapo wote hawa ndio wanafanya idadi ya wanufaika 1,961 iliyotajwa na Wizara.

Tungeweza kusema ni "Value Chain Analysis" ya watakaonufaika na mradi katika shughuli ya kiuchumi ila wametajwa kwa jinsia KE na ME maana yake sio "Value Chain Analysis " bali ni ni aidha orodha hewa iliyoongezwa ili kuonesha vijana wengi wamepata ikiwa sio kweli au ni orodha hewa iliyoongezwa kwa dhamira nyingine tofauti.

Ngome ya Vijana tunaendelea kufuatilia hatua kwa hatua juu ya utolewaji wa fedha hizi, vigezo, marejesho, uratibu na taarifa stahiki ili kundi kubwa la vijana linufaike kuliko ubabaishaji unaoendelea hivi sasa.

Mapendekezo Yetu
  • Tunaitaka Wizara ya Maendeleo ya Vijana kutoa ufafanuzi maana halisi ya wanaoitwa wanufaika 1,961. Wizara itueleze wamepatikana namna gani. Mfano mimi nimewekewa wanufaika 10 (wakiume 7 na wakike 3) ikiwa siwajui.

  • Tunaitaka Wizara ya Maendeleo ya Vijana kuondoa vigezo vya leseni ya biashara katika kuomba mkopo kwa vijana wanaoanza biashara ambao ndio wengi ili Vijana wengi wanufaike.

  • Tunaitaka Wizara ya Maendeleo ya Vijana haraka ifungue dirisha la pili ili Vijana wote ambao hawakupewa fedha awamu hii ya kwanza wapewe. Fedha hizi ni kodi za wananchi na fedha hii ni mkopo vijana watalipa.

  • Tunaitaka Serikali kurejesha fedha zote Tsh. bilioni 200 ambazo zimepelekwa Wizara za kisekta, zirejeshwe kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili kutunisha Mfuko kwa lengo la kunufaisha Vijana wengi zaidi waliokosa.

  • Tunataka Wizara ya Maendeleo ya Vijana itoe sababu ya vijana wote waliokosa mkopo awamu hii ya kwanza waambiwe sababu ya wao kukosa, kila kijana aliyeomba akakosa apewe sababu ya kukosa na kama kuna kasoro apewe nafasi arekebishe na mchakato uendelee. Haipaswi kuishia tu kusema wamekosa.



​
 
Nadhani bado Serikali haijajipanga vilivyo kwenye suala la utoaji mikopo kwa vijana.

Kama kweli Serikali inahitaji kutengeneza ajira kwa vijana, watoe mikopo ya kueleweka, mfano siwezi kuomba mkopo wa 1-5 Million alafu ukategemea nitafanya kitu cha maana.

Muhimu: Angalieni Idea, na aidha kama hamuelewi kinachoandikwa waiteni wahusika kuitetea proposal. Huwezi kupata undani kwenye concept ya 5 pages.

Kama Serikali haijajipanga, iache kwanza utoaji wa mikopo, vinginevyo mtatafuta lawama na vijana, sawa na ile mikopo ya Halmashauri.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…