Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
ABDULWAHID SYKES KATIKA "THE MAKING OF TANGANYIKA" NA JUDITH LISTOWEL
Maggid Mjengwa:Judith anaeleza pia kushindwa kwa Abdul Sykes kwenye kugombea urais wa T. A. A. Jambo hili ningependa Mwalimu wangu Mohamed Said alitolee maoni yake juu ya tafsiri ya jambo hilo.
Mwenyekiti,
Maggid Mjengwa Mwenyekiti kuna kitu kidogo umekosea katika swali lako.
Ulitakiwa uulize hivi, ''Judith anaeleza pia kushindwa kwa kura chache kwa Abdul Sykes kwenye kugombea urais wa TAA."
Ungeuliza hivi swali la kwanza kwa msomaji angejiuliza kwa nini Nyerere alishinda kwa kura chache?
Abdul laiti angegombea uchaguzi ule kwa nia ya kushinda angeshinda bila wasiwasi wowote.
Abdul angeshinda kwa kuwa Nyerere hakuwa anajulikana na mtu yoyote ukimtoa yeye mwenyewe Abdul, Ally Sykes, Dossa Aziz na John Rupia.
Ukiangalia vipi uongozi wa TAA ulibadilishwa mwaka wa 1950 utaona Schneider ndiye aliyesimama kumwondoa kaka yake Thomas Plantan kwenye uongozi na akawaingiza Abdul na Dr. Kyaruzi.
Kabla ya uchaguzi ule wa April 1953 Abdul Sykes akiongozana na Ali Mwinyi Tambwe alikwenda Nansio,
Ukerewe kwa Hamza Mwapachu ili apate kauli ya mwisho ya Mwapachu kuhusu Nyerere, kuwa bado ana fikra kuwa Nyerere atiwe katika uongozi wa juu wa TAA na 1954 waunde TANU na Mwalimu aongoze harakati za kudai uhuru wa Tanganyika?
Jibu la Mwapachu lilikuwa Abdul amsaidie Nyerere kuingia katika uongozi wa juu wa TAA na amsaidie kupata ushindi na mwaka unaofuatia TANU iundwe na Nyerere awe kiongozi wa harakati za uhuru.
Sababu aliyotoa kumpa Abdul ni kuwa yeye alikuwa anaona Nyerere anafaa zaidi kwa uongozi wa TANU kuliko Abdul lakini akaongeza kueleza kuwa Abdul kama Muislam kuongoza harakati za uhuru zitawazidishia Waingereza ukaidi kwani wanaweza wakachukua harakati za uhuru kama vurugu nyingine za Waislam mfano wa Vita Vya Maji Maji vya 1905.
Kwa siasa za nyakati zile bila ya Nyerere kukubalika na wenyeji wa Dar es Salaam Abdul akiwa mmoja wa hawa wanamji, Nyerere asingeweza kushinda uchaguzi ule.
Hivyo basi ndani ya ile ''inner circle ya inner circle,'' ya TAA ndani ya TAA Political Subcommittee uamuzi ulipitishwa kuwa Nyerere lazima ashinde uchaguzi ule.
Laiti viongozi hawa wangefanya khiyana ya kumkataa Nyerere kwa sababu yeyote ile wangekuwa wamefanya kosa kubwa sana.
Nyerere aliiongoza TANU na harakati za kudai uhuru wa Tanganyika kwa ustadi na ufanisi mkubwa sana.
Abdul Sykes hakumueleza Listowel haya na kwa miaka mingi historia hii hakuna aliyekuwa anaijua hata Nyerere mwenyewe hakupata kusema kuwa kwanza alipokelewa na Abdul Sykes na pili kuwa alipata kugombea urais wa TAA dhidi ya Abdul Sykes.
Siku Mwalimu alipotaja jina la Abdul Sykes hadharani katika hotuba yake ya kuwaaga wazee wa Dar es Salaam Ukumbi wa Diamond mwaka wa 1985, Mwalimu alisema ''anadhani'' Abdul Sykes nafasi yake katika TAA alikuwa Katibu.
Mwalimu hakuwa na uhakika na historia ya uongozi wa Abdul katika TAA ilibidi adhanie.
Ningependa kuhitimisha kwa kusema kuwa aliyemweleza Listowel historia ya uchaguzi ule baina ya Abdul Sykes na Julius Nyerere alikuwa Denis Phombeah ambae ndiye alikuwa Meneja wa Ukumbi wa Arnautoglo ulipofanyika uchaguzi ule na yeye akawa ndiyo Returning Officer.
Denis Phombeah