HUKU bilionea wa Urusi, Roman Abramovich, ambaye ni mmiliki wa klabu ya Chelsea akitarajiwa kushuka leo kutoka kilele cha Mlima Kilimanjaro, safari aliyoianza Septemba 3, juhudi za mashabiki wa timu kuonana na bilionea huyo zimekwama.
Kikwazo ni viongozi wa mashabiki hao kushindwa kuonana na wakala wa kampuni iliyomleta bilionea huyo ya African Environment, hivyo kuwa vigumu kutokana na kuwapo ulinzi mkali dhidi ya bilionea huyo.
Awali, mashabiki hao walipanga kuonana na bilionea huyo aliyetua nchini Septemba 2 na kuanza kupanda Mlima Kilimanjaro siku iliyofuata, ambaye anatarajiwa kushuka leo kabla ya kuondoka nchini kesho.
Kwa mujibu wa mratibu wa mashabiki hao, Stive Munguto ‘Ticha' alisema pamoja na nia yao njema ya kutaka kuonana na bilionea huyo, wamekwama baada ya kushindwa kuonana na viongozi wa African Environment.
"Tumefanya kila linalowezekana ili kuona ni njia gani itakayowezesha kuonana na Abramovich, lakini tumekwama kukutana na viongozi wa Kampuni ya African Environment," alisema Munguto.
Hata hivyo, alisema bado wanaendelea na jitihada zao za mwisho ili kuweza kuzungumza naye baada ya kushuka leo, baada ya kufanikiwa kufika eneo la barafu, umbali wa mita 4,800 kutoka usawa wa bahari.
Bilionea huyo wa Kirusi anashuka leo kutoka Mlima Kilimanjaro akipitia lango la Mweka, kabla ya kufanya ziara ya siku moja katika Chuo cha Hifadhi ya Wanyamapori Mweka.
Source Tanzania daima