Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
KUHUSU MWENENDO NA ONGEZEKO LA DENI LA TAIFA LA ZANZIBAR
(2020-2024) "UNAPOSHINDWA KUHESABU, UTASHINDWA KUDHIBITI"
Tarehe 7 Januari 2025, ACT Wazalendo inatoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu ongezeko kubwa na lisilokuwa la kawaida la Deni la Taifa la Zanzibar katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Hussein Mwinyi.
Ripoti ya mwaka wa Fedha 2023/2024 iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania mwezi Disemba 2024 inaonyesha kuwa deni hilo limepanda kwa kasi kutoka TZS bilioni 887 mwezi Juni 2021 hadi kufikia TZS trilioni 3.6 mwezi Juni 2024. Hili ni ongezeko la deni mara 4 zaidi yaani zaidi ya asilimia 400 kati ya 2021 na 2024. Kwa miaka hii mitatu, kasi ya kuongezeka Deni la Zanzibar kwa mwaka ni wastani wa asilimia 59 ilhali kasi ya ukuaji wa Uchumi wa Zanzibar kwa mwaka ni wastani wa asilimia 6 tu. Mwenendo wa Deni la Taifa la Zanzibar kwa miaka minne iliyopita (2021 - 2024) ni kama ifuatavyo: -
SN. Muda. Deni La Taifa
1. Juni 2021. TZS 887 Bilioni
2. Juni 2022. TZS 1.34 Trilioni
3. Juni 2023. TZS 2.74 Trilioni
4. Juni 2024. TZS 3.6 Trilioni
Takwimu hizi zinathibitisha kushindwa kwa Serikali ya Awamu ya Nane ya Rais Mwinyi kusimamia uchumi wa Zanzibar kwa uwazi na ufanisi. Badala ya kupunguza mzigo wa madeni, serikali imeongeza mikopo bila kuweka mikakati madhubuti ya kulipia madeni hayo kwa njia inayowalinda wananchi wa kawaida.
Pia soma: Deni la Taifa kufikia trilioni 91, nchi imekaribia kuuzwa?
Katika hotuba yake ya hivi karibuni, Rais Dkt. Mwinyi alidai kuwa deni la taifa la Zanzibar ni TZS trilioni 1.2 pekee, akikanusha ongezeko kubwa linaloelezwa na Benki Kuu. Hata hivyo, ripoti za Benki Kuu zinaonyesha kuwa deni limefikia TZS trilioni 3.6346, ikiwa ni tofauti kubwa na madai ya Rais. Hali hii inazua maswali makubwa kuhusu uwazi wa taarifa za Serikali na dhana ya uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma.
Serikali ya Zanzibar inadaiwa kuelekeza sehemu kubwa ya fedha hizi katika miradi mikubwa ambayo haijatoa matokeo ya moja kwa moja kwa maisha ya wananchi wa kawaida. Badala yake, miradi hii imekuwa chanzo cha mzigo wa kiuchumi, huku gharama zake zikiwa kubwa kuliko faida zinazotarajiwa. Ripoti za Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa Zanzibar zinaonyesha kasoro kubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za mikopo.
Wananchi wa kawaida wanabeba gharama za riba kubwa za madeni haya kupitia ongezeko la kodi, mfumuko wa bei, na ukosefu wa huduma za msingi. Serikali imeshindwa kushughulikia changamoto za kiuchumi zinazowakumba wananchi, kama vile mfumuko wa bei wa bidhaa muhimu, ukosefu wa ajira, na malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi wa sekta ya umma. Badala ya kuwapa matumaini, serikali imewazunguka wananchi wake katika mtego wa madeni makubwa yanayoendelea kuwa mzigo kwa kizazi cha sasa na kijacho.
ACT Wazalendo inasisitiza kwamba Zanzibar inahitaji mwelekeo mpya wa kiuchumi na kisiasa. Serikali inayoongozwa na Rais Mwinyi imeonyesha wazi kushindwa kutimiza matarajio ya wananchi. Badala ya kubuni mikakati ya kukuza uchumi wa ndani, serikali imeegemea kwenye mikopo isiyo na tija, huku ikipuuza sekta zinazoweza kuchangia ukuaji wa uchumi, kama kilimo, viwanda, uvuvi, na ubunifu.
Kwa msingi huu, tunatoa wito kwa Serikali ya Zanzibar kutoa maelezo ya kina na ya uwazi kuhusu hali ya deni la taifa na mipango ya matumizi ya fedha hizo. Vile vile wananchi waelezwe riba za madeni hayo na mpango wa Serikali kuyalipa upoje?
Tunawataka wananchi kuhoji kwa nini rasilimali za umma zinakuwa mzigo badala ya kuwa fursa za kuboresha maisha yao. Aidha, tunawahimiza Wazanzibari kuungana kupinga utawala wa CCM unaoendelea kuongeza umasikini na changamoto za kiuchumi kwa wananchi wengi.
Zanzibar inastahili uongozi wenye maono, uwazi, na mipango thabiti ya kiuchumi inayojali maslahi ya wananchi wote. ACT Wazalendo itaendelea kusimama na wananchi katika kutetea haki zao na kupinga ukosefu wa uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za taifa.
Imetolewa na;
Prof. Omar Fakih Hamad
Msemaji wa Sekta ya Fedha, Uchumi na Dira ya Maendeleo Zanzibar
Kwa niaba ya ACT Wazalendo