Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
SMZ ichukue hatua stahiki kwa maafisa wa MIMCA na KMKM, waliohusika na udhalilishaji Watembeza Utalii
Hivi karibuni kupitia Mitandao ya Kijamii tumewaona Askari wa Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) wakiwadhalilisha na kuwapiga watembeza Watalii katika Bahari ya Kisiwa cha Mnemba, kilichopo nje kidogo ya pwani ya Matemwe, walipokuwa wakifanya ziara za kuonyesha Pomboo kwa watalii (Dolphin tour) Mnemba Kaskazini Unguja, Baada ya tukio hilo tarehe 25/11/2024 tumeona taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Mahusiano katika Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, ikikemea vikali ilichokiita Tukio la Kutotii Amri kwa mmoja ya watembezaji wageni katika Hifadhi ya Mnemba (MIMCA).
Chama cha ACT Wazalendo tumepokea kwa mshangao na masikitiko taarifa za kudhalilishwa watembeza watalii hao, huku Wizara yenye jukumu la kuwalinda, kuwatetea na kuwalea nayo ikiamua kuendelea kuwakandamiza kwa kuwahukumu bila ya kufanya uchunguuzi na kujiridhisha, sababu hasa ya tukio lile ni nini?
ACT Wazalendo tunaamini kuwa kilichotokea ni zaidi ya kile kinachoitwa kutotii amri kutokana na athari zinazoweza kujitokeza kuwa kubwa zaidi, kiuchumi na sekta nzima ya utalii kwa kuzingatia kitendo cha udhalilishaji wa kipigo walichopata watembeza utalii hao, kimetokea mbele ya wageni.
ACT Wazalendo tunalaani vikali, tukio hilo la udhalilishaji wa watembeza watalii lililotekelezwa na wasimamizi wa hifadhi ya Mnemba (MIMCA) kwa kushirikiana na Kikosi cha KMKM, mbele ya wageni waliokuwa wakifurahia vivutio vya utalii na ni aibu kubwa kwa nchi yetu, hali hii inaonesha wazi namna, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inyoongozwa na Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, kushindwa kuwa na mipango na usimamizi mzuri katika sekta ya utalii.
ACT Wazalendo tunaamini kwamba, tukio hili la kufukuzana kwa boti baharini na kuwapiga watembeza utalii hadharani linaonesha ukosefu wa usalama wa wageni na kuwaathiri watalii kwa kuonesha udhaifu katika usimamizi wa kiusalama wao, aidha tukio hili limeharibu taaswira ya sekta ya utalii, hasa ikizingatiwa kuwa Mnemba ni eneo maalum la wageni, lenye utaratibu maalum wa kuingia na kutoka, tunajiuliza kwa nini ikiwa namba ya boti na nahodha wanajulikana, wasimamizi wa hifadhi ya MIMCA hawakuchukua hatua za kistaarabu kuzungumza na watembeza watalii, badala ya kutumia nguvu mbele ya wageni? Kutokana na tukio hili ACT Wazalendo, tunaitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kufanya mambo yafuatayo:-
1. Kulaani na kukemea, kitendo walichofanyiwa watembeza utalii tena mbele ya wageni na wasimamizi wa hifadhi ya MIMCA na Kikosi cha KMKM.
2. Kuchukua hatua stahiki kwa maafisa wa hifadhi ya MIMCA na askari wa Kikosi cha KMKM, waliohusika na kitendo kile cha udhalilishaji walichokifanya.
3. Kuweka utaratibu maalum wa uchukuaji hatua na utoaji wa adhabu kwa watembeza watalii na sio kuwapiga na kuwadhalilisha, mbele ya wageni.
4. Kutoa elimu, kwa watembeza utalii, juu ya namna bora ya kutii na kuheshimu sharia hasa katika maeneo ya hifadhi.
ACT Wazalendo tutaendelea, kusema na kutetea usalama na haki za watu wote, wakiwemo watembeza watalii, ili kuona kuwa haki na usalama wa watalii na watembeza watalii zinazingatiwa bila ya madhara yoyote yale.
Imetolewa leo, tarehe 29/11/2024 na,
Ndugu. Jina Hassan Suleiman
Naibu Msemaji wa Sekta ya Utalii na Urithi wa Taifa.