Uchaguzi 2020 ACT-Wazalendo: Bima ya Afya kwa wote kupitia Hifadhi ya Jamii

Uchaguzi 2020 ACT-Wazalendo: Bima ya Afya kwa wote kupitia Hifadhi ya Jamii

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
Joined
May 5, 2014
Posts
631
Reaction score
1,577
Katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 kila Chama cha Siasa nchini kimetoa ahadi ya Bima ya Afya kwa Watanzania. Hii ni hatua kubwa sana kwani miaka 5 iliyopita ni ACT Wazalendo peke yake ndio tulikuwa na ajenda hii katika Ilani yetu ya 2015. Kwamba Vyama vyote vimeikumbatia ajenda Hii ni Ushindi mkubwa kwetu katika ushawishi wa kisera. Hata hivyo vimetamka tu kuwa vitawezesha Bima ya Afya kwa Watanzania bila ya kusema utekelezaji wake utakuwaje. ACT Wazalendo inayo majibu.

Kupitia Ilani ya ACT Wazalendo Chama chetu kimeeleza kwa kina ni namna gani itatetekeleza Ahadi hiyo ya kuwezesha kila Mtanzania kuwa na Bima ya Afya ifikapo Mwaka 2025. Mapendekezo ya ACT Wazalendo yatabadilisha kabisa Maisha ya Watanzania waliowengi hasa wanaojihusisha na Kilimo, Uvuvi na Ufugaji, 67% ya Watanzania wote.

Serikali itakayoundwa na ACT Wazalendo na washirika wake itachukua hatua zifuatazo;

- Mfumo wa Hifadhi ya Jamii utaunganishwa na Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa ambapo kila Mwanachama wa Skimu ya Hifadhi ya Jamii atapata Fao la Bima ya Afya litakalosimamiwa na Mfuko wa Bima ya Afya. Hapatakuwa na michango tofauti ya Bima ya Afya na Hifadhi ya Jamii.

- Kila Mtanzania ambaye ni Mkulima, Mfugaji, Mvuvi, Mfanyabiashara ndogondogo au mtu yeyote asiye kwenye sekta Rasmi atachangiwa na Serikali 1/2 ya Mchango wa kima cha Chini cha kuchangia kwa Mwezi kwenye Hifadhi ya Jamii. Mchango huu wa Serikali kwenye Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii utatoka kwenye Bajeti ya Kila Mwaka.

- Mtu atakayechangia kwa miaka 10 mfululizo kwenye Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii atakuwa na sifa ya kulipwa Pensheni atakapokuwa na Umri wa kustaafu uliowekwa na Serikali. Akifariki Dunia kabla ya kutimiza miaka 10 michango yake na riba italipwa kwa warithi wake. Akitaka kujitoa kabla ya miaka 10 atalipwa kiasi alichochangia na riba. Akijitoa baada ya miaka 10 atalipwa pesa yote iliyo kwenye Akaunti yake ya Skimu ya Hifadhi ya Jamii ikiwemo Mchango wa Serikali

- Bima ya Afya, Fao za Uzazi kwa Wanachama Wanawake, Fao la Bei kwa Wakulima, Bima ya Mazao, Samaki/Dagaa na Mifugo na Mikopo kwa Vyama vya Ushirika na Jumuiya za Wananchi itakuwa ni sehemu ya mafao ya muda mfupi kutoka Skimu ya Hifadhi ya Jamii ya Taifa

Kwa mujibu wa makadirio ya idadi ya Watu wazima Tanzania na ukuaji wa idadi ya Watu, na kwa kuzingatia kiwango cha chini cha kuchangia cha Shilingi 30,000 kwa Mwezi kwa kila Mtanzania; Gharama za Mchango wa Serikali ( MATCHING FUNDS ) kwa Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa watu walio nje ya Sekta Rasmi ili kila Mtanzania kuwa na Bima ya Afya inakadiriwa kufikia shilingi Bilioni 648 kila mwaka. Fedha hizi zitatoka kwenye Bajeti ya Serikali ya Kilwa Mwaka kwa Mujibu wa Sheria Maalumu itakayotungwa na Bunge.

Faida ya Mfumo huu ni nini ?

1. Mfumo huu utarahisisha malipo ya Hifadhi ya Jamii na Bima ya Afya kwa Mwananchi kuchangia mara moja tu kwa Chombo kimoja tu. Ukiwa na Kadi ya Hifadhi ya Jamii moja kwa moja unakuwa na Bima ya Afya, Bima ya Mazao kwa Wakulima na Bima ya Majanga kwa Wakulima, Wavuvi na Wafugaji. Wafanyakazi watachanga mara moja tu badala ya sasa ambapo wanalipa Hifadhi ya Jamii na pia wanalipa Bima ya Afya.

2. Mfumo huu utatoa kivutio kwa Wananchi wengi kujiwekea Akiba kwani kila Shilingi 1 wanayoweka Serikali pia inawawekea Shilingi 1 nyengine. Uwiano wa uwekaji Akiba nchini kwa Pato la Taifa utaongezeka na hivyo kuwezesha Uwekezaji mkubwa wa kuongeza shughuli za Uchumi kuongezeka.

3. Uwekezaji wa ndani utakua kwa kasi na hivyo Nchi kuweza kutekeleza Miradi mikubwa ya uzalishaji Mali inayochukua muda mrefu kuanza kuzalisha faida kama vile Kilimo cha umwagiliaji, Viwanda vya kuongeza thamani ya Mazao ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo.

4. Kila Mtanzania atakuwa na Bima ya Afya kwani Mtu 1 Mwanachama wa Hifadhi ya Jamii anachangia Watu 5 kwenye Bima ya Afya. Skimu ya Hifadhi ya Jamii ya Taifa ikifikisha Watu 10M, itakuwa ni Sawa na Watanzania 60M kuwa na Bima ya Afya.

5. Watanzania wengi watakuwa na Pensheni ya uzeeni bila kujali kama alikuwa Sekta Rasmi au Sekta isiyo Rasmi.

Bima ya Afya kwa wote kutokana na Sera za ACT Wazalendo ni zaidi ya Bima ya Afya. Ni Hifadhi ya Jamii. Ni Maisha. Vyama vingine vieleze namna gani vitatekeleza ajenda hii kubwa na muhimu sana kwa Wananchi.

Imetolewa na

Zitto Kabwe, Mwami Ruyagwa
Kiongozi wa ACT Wazalendo
Septemba 17, 2020
Mafia, Pwani.
 
Bima zinalipiwa, sasa ni nani atazilipia hizo bima ili wote tuwe na bima?!

Bora mgesema matibabu bure tungewaelewa.
 
Back
Top Bottom