JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,780
- 6,607
ACT Wazalendo tunapenda kumtahadharisha Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambaye ndiye Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Ndugu Mohamed Mchengerwa kuwa mwenendo wa mambo kuelekea uteuzi wa wagombea kesho tarehe 8 Novemba 2024 unatia mashaka makubwa na unahashiria kuvurugwa kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.
Chama chetu kimefikia hitimisho hilo kutokana na sababu zifuatazo;
Kona zote nchini, wagombea wetu wanafuatwa na wasimamizi wa uchaguzi, watendaji mbalimbali wa serikali na viongozi na makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakishawishiwa na kushinikizwa kuwa wajitoe kuwa wagombea. Wasimamizi wa Uchaguzi kwenye maeneo mengi nchini wameshiriki vitendo hivi kwa kupiga simu kwa wagombea wao wenyewe au kuwapatia makada wa CCM namba za wagombea zilizojazwa kwenye fomu za kugombea. Mifano ya hili ni katika Halmashauri za Tandahimba, Kondoa Mjini, Kondoa Vijijini, Kilwa, Chalinze, Kigoma Mjini, Nyamagana nk. Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi mgombea hawezi kujitoa kabla ya uteuzi, hivyo barua yeyote ya watu kujitoa kabla ya siku ya uteuzi ni BATILI na kinyume na kanuni za uchaguzi.
Kupata matukio yote kimkoa kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa bofya hapa: LGE2024 - Special Thread: Orodha ya Mijadala ya Mikoa yote Tanzania Bara inayoshiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024
Taarifa tunazozikusanya zinaonesha kuwa upo mpango wa wasimamizi wa uchaguzi kuzichafua au kuziongea taarifa fomu za kugombea ili kuwapotezea sifa za kuteuliwa wagombea wa ACT Wazalendo na vyama vingine vya upinzani.
Tumepokea taarifa kuwa baadhi ya Wazimamizi wa uchaguzi wanakusudia kuyapuuza Maelekezo ya Waziri wa TAMISEMI kuvipa vyama uhuru wa kuchagua ngazi ya kudhamini wagombea. Kwenye barua yake ya tarehe 14 Oktoba 2024 yenye Kumb. Namba CCB.126/215/01/85 Waziri wa TAMISEMI aliviandikia vyama kuvitaka kuchagua ngazi ya chini itayodhamini wagombea.
Chama cha ACT Wazalendo kupitia barua ya Katibu Mkuu ya tarehe 20 Oktoba 2024 yenye yenye Kumb. Namba ACT/HQ/OFKM/011/VOL.III/256 Chama cha ACT Wazalendo kiliwasilisha ngazi ya Kata kuwa ndio itayowadhamini wagombea wake. Kwa taarifa tulizozikusanya kwenye baadhi ya maeneo nchini, wasimamizi wa uchaguzi wanakusudia kupuuzia maelekezo hayo ya Waziri wa TAMISEMI nakuwaengua wagombea wa ACT Wazalendo. Mfano wa hili ni Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Ruangwa.
MSIMAMO WETU
Tunamtaka Waziri wa TAMISEMI kuhakikisha kuwa hakuna mgombea hata mmoja wa ACT Wazalendo ambaye ataenguliwa kutokana na fomu za wagombea kuchafuliwa na wasimamizi. Chama chetu kilijiandaa vizuri kuwapa mafunzo wagombea wetu na kuwasimamia kuhakikisha wanajaza fomu vizuri. Ni imani yetu kuwa wagombea wetu wote watateuliwa.Tunamtaka Waziri wa TAMISEMI ahakikishe Maelekezo yake ya kuvipa vyama uhuru wa kuteua ngazi ya chini ya kudhamini wagombea yanazingatiwa katika uteuzi wa wagombea.
Tunamtaka Waziri wa TAMISEMI atoe maelekezo ya wazi kwa Wasimamizi wote wa uchaguzi kwamba waache kupokea barua za wagombea kujitoa kabla ya uteuzi kufanyika na kwamba vyama vya siasa vidharau barua hizo.
ACT Wazalendo hatutakubali uwekezaji mkubwa tulioufanya katika kujiandaa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uharibiwe na wasimamizi wachache wa uchaguzi wasio waadilifu ambao wamejipanga kuuvuruga uchaguzi.