Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
SERIKALI IMEWATENGA WANAWAKE WA VIJIJINI
Leo dunia inapoadhimisha siku ya wanawake vijijini, hapa nchini Tanzania hali ya wanawake, hasa wa vijijini bado ipo duni. Sensa ya 2022 inaonyesha kati ya wanawake milioni 31.6, wanaoishi mjini ni milioni 11.2 na waliosalia wote wanaishi vijijini wengi wao wakiwa katika sekta isiyo rasmi huku asilimia 65 ya wakulima vijijini wakiwa ni wanawake.
Licha ya wanawake kuwa wachangiaji wakubwa wa ukuaji uchumi kwa kupitia kilimo, bado jitihada za Serikali kuondoa umasikini na kumnyanyua mwanamke ni ndogo. Zaidi wanawake hawashajiishwi vya kutosha kushiriki katika sekta zinazokuwa kwa kasi kama vile sekta ya ujenzi, sekta ya uzalishaji viwandani, sekta ya usafirishaji na uhifadhi wa mizigo.
Wanawake wa vijijini wanakabiliwa na changamoto ya huduma za kijamii inayochagizwa na uwekezaji mdogo katika huduma za afya msingi na mfumo mbovu wa ugharamiaji wa huduma za Afya. Kama ilivyo kwa wananchi wote, mwanamke wa kijijini kaachiwa mzigo wa kugharamia huduma ya afya kwa kulipia moja kwa moja kutoka mfukoni, au kupitia bima za gharama zenye matabaka ambazo wengi wao hawamudu kuzikata.
Pia Wanawake ndio wanaoteseka zaidi na uhaba wa upatikanaji wa Maji Vijijini hali inayowafanya watembee umbali mrefu kutafuta maji na kuathiri shughuli nyingine ya kujiongezea kipato. Hata shughuli ya ulezi wa watoto wakati mwingine ulegalega kutokana na mama kutumia muda mrefu katika kutafuta maji.
ACT Wazalendo tuanitaka Serikali ijielekeze katika kumkwamua mwanamke wa kijijini kwa kufanya yafuatayo:
- Mosi, Serikali iwekeze kwenye teknolojia rafiki na ya kisasa katika kilimo, irahisishe upatikanaji wa pembejeo, ifungamanishe kilimo na viwanda pamoja na kutafuta masoko ya uhakika.
- Pili, Serikali ifungamanishe huduma za afya na hifadhi ya jamii ili kuwawezesha wananchi wasio kwenye sekta isiyo rasmi kuweka akiba na kupata huduma ya afya kama fao.
- Tatu, Serikali iwekeze vya kutosha kwenye miradi ya maji, ili kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji kwa wananchi. Kwa madhumuni ya kumaliza tatizo la maji nchini, ACT Wazalendo katika ilani ya uchaguzi tuliahidi kutenga Trilioni 10; yaani trilioni 2 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.
Imetolewa na;
Ndg. Janeth Joel Rithe
Waziri kivuli wa Ustawi, Maendeleo ya Jamii, wanawake na watoto.
15 Oktoba 2023.
Ndg. Janeth Joel Rithe
Waziri kivuli wa Ustawi, Maendeleo ya Jamii, wanawake na watoto.
15 Oktoba 2023.