Uchaguzi 2020 ACT Wazalendo wazungumzia Maamuzi ya Tume zote mbili za Uchaguzi (NEC na ZEC) juu ya rufaa zilizokatwa na wagombea wa ACT-Wazaendo

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu Waandishi na Watanzania wenzangu, Nianze kwa kuwashukuru kuja kwenu kuitikia wito wetu na mashirikiano mnayokipa Chama chetu cha ACT Wazalendo.

Leo tumewaita hapa kuzungumzia mapokeo ya chama chetu juu ya Maamuzi ya Tume zote mbili za uchaguzi yaani NEC na ZEC juu ya rufaa zetu zilizokatwa na wagombea wa Chama Chetu kwa nafasi za Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani.

Kwanza, niwashukuru Tume zote mbili za Uchaguzi yaani NEC na ZEC kwa kutekeleza wajibu wao wa kisheria wa kutenga muda na kuzifanyia kazi Rufaa hizo kwa kadri walivyoona wao inafaa. Tunafahamu kuwa Rufaa zilikuwa nyingi kwa nchi nzima na wametumia muda mwingi sana katika kuzitafutia majawabu hoja zilizopelekwa mbele yao na wagombea ambao hawakuridhika na maamuzi ya Wasimamizi wa Uchaguzi wa ngazi za Majimbo na Wilaya. Tunawashukuru pia kwa kuwarudisha baadhi ya wagombea wetu Bara na Visiwani.

Ndugu Waandishi, Chama chetu pamoja na kufahamu ukweli kwamba Sheria zetu za Uchaguzi ile ya Zanzibar nambari 4 ya 2018 kifungu cha 52(4) na ile ya Taifa ya Uchaguzi kifungu cha 40(6) vinaeleza kuwa maamuzi ya Tume kwa Rufaa zinazohusu uteuzi kuwa ni ya mwisho, tumeona ipo haja ya kuwaeleza wanachama wetu na watanzania kwa ujumla kwa vipi tunaamini tume haikutenda haki kwa Rufaa ambazo zimekataliwa kwa sababu mbali mbali zilizoelezwa na Tume.

Na hii ni kutokana na kuibuka kwa wimbi la taarifa za upotoshaji kuwa wagombea wetu walifanya uzembe katika kutozingatia sheria na ujazaji wa fomu hizo. Sisi tunasema kuwa hakuna uzembe wowote uliofanywa na wagombea wetu na ndio maana tumeamua kuweka wazi wa nini hasa kimetokea.

Ndugu Waandishi, naomba nianze na Rufaa za wagombea wa Ubunge wa majimbo sita ya Zanzibar zilizokataliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa hoja kuwa zimewasilishwa nje ya muda. Majimbo yenyewe ni Jimbo la Wawi, Kiwani, Ole, Mkoani, Chambani na Kijini.


Ndugu Waandishi na Watanzania. Sio kweli hata kidogo kuwa wagombea wetu wa majimbo haya wamewasilisha Rufaa zao nje ya Muda. Wagombea wote kwenye majimbo hayo wamewasilisha Rufaa zao ndani ya masaa 24 kama inavyoelekezwa na kanuni ya 31(1) ya kanuni za uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2020. Chama kimejiridhisha kuwa Mgombea wa Jimbo la Wawi kwa mfano, amewasilisha Rufaa yake na kupokelewa tarehe 28-08-2020 Saa 11:15 Jioni ikiwa ni masaa 20 tu tangu tarehe na saa ya kutoka uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi juu ya Pingamizi zake za asili uamuzi ambao ulitolewa tarehe 27-08-2020 saa 3:30 Usiku.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Mgombea wa Jimbo la Ole ambae uamuzi wa pingamizi umetoka tarehe 27-08 -2020 Saa 3:30 Usiku na Rufaa yake imepokelewa tarehe 28-08-2020 Jioni, Mgombea wa Kiwani ambae uamuzi wa Pingamizi zake umetolewa tarehe 28-08 -2020 na Rufaa yake imepokelewa Saa mbili Asubuhi ya tarehe 29-08-2020, muda sawa sawa na Mgombea wa Mkoani na Chambani huku Mgombea wetu wa Jimbo la Kijini amewasilisha Rufaa yake tarehe 28-08-2020 Saa 4:20 Asubuhi kwa kuwa uamuzi wa pingamizi zake umetoka tarehe 27-08-2020.

Ndugu Waandishi na Watanzania. Uchunguzi wetu umebaini kuwa kilichotokea ni hujuma iliyofanywa na Wasimamizi wa Uchaguzi wa majimbo hayo niliyotaja ambao kwa makusudi wamepeleka taarifa za uongo kwa Tume ya Uchaguzi kwa kujaza katika Fomu Nam. 9B kuwa maamuzi ya kuwaengua wagombea wetu/maamuzi ya pingamizi yametoka tarehe 26-08-2020 ili ionekane kuwa Rufaa zilizowasilishwa tarehe 28 na 29 Agosti, 2020 zilikuwa Nje ya muda jambo ambalo si kweli.

Sisi Act Wazalendo tunaamini kabisa wasimamizi hao wa Uchaguzi wa majimbo hayo ambao huko nyuma tulishatoa kauli ya kutilia mashaka uadilifu wao, walifanya hivyo kwa makusudi ili kuipotosha Tume wakati wa kusikiliza Rufaa zetu. Matokeo yake Tume iliacha kushughulika na hoja za Rufaa zilizowasilishwa na kujikita juu ya muda wa uwasilishwaji wa Rufaa.

Chama kimemwandikia barua Mwenyekiti wa Tume kumtanabahisha juu ya hujuma na upotoshaji uliofanywa na Wasimamizi wa Uchaguzi wa kujaza taarifa za Uongo kwenye sehemu ya 2 fomu ya nambari 9B. Tumeiomba Tume ikiona inafaa ipitie upya uamuzi wake badala ya kusubiri sisi tufungue shauri la uchaguzi hapo baadae.

Ndugu Waandishi, Wanachama wa ACT Wazalendo na Watanzania kwa ujumla.

Jambo la pili ambalo Chama chetu kinataka kuliweka wazi leo ni kuhusu kutoteuliwa kwa Wagombea wetu 11 wa Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani saba kule Zanzibar.

Kwanza niseme kuwa Chama chetu kama Taasisi tunaheshimu maamuzi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar lakini hii haina maana kuwa tunaamini wametutendea haki katika kufikia maamuzi yao. Tunaamini kabisa kuwa hoja za Pingamizi dhidi ya Wagombea wetu zilikuwa dhaifu na kwamba Hoja tulizowasilisha kwenye Rufaa zilikuwa za msingi kwa Tume ya Uchaguzi


Zanzibar kuwateua wagombea wetu kushiriki kwenye Uchaguzi kama Wagombea.

Pili, kumekuwepo na upotoshaji mkubwa wa taarifa na kilichojiri kwenye Pingamizi na Rufaa hizi, taarifa zinazolenga kujenga taswira kuwa Wagombea wetu walikuwa wazembe sana katika kujaza na kurudisha fomu. Hivyo tumeona ni muhimu kuwaelezeni kwa undani sababu walizoondolewa wagombea wetu hao 11. Na hapa nitaweka wazi Pingamizi na Rufaa za kila mmoja wao.

Mgombea wa Jimbo la Mtoni Ndugu Juma Duni Haji

Huyu ni Makamo wa Mwenyekiti wetu wa Chama na ameondolewa na Tume kwenye orodha ya wagombea kwa kile kilichoitwa Taarifa zake hazijitoshelezi kumtambua mgombea na hivyo kupelekea kuwa na kiapo kibovu. Taarifa gani hizo? Ni kwamba katika hati tatu za kiapo zilizojazwa, Hati mmoja mgombea amewacha kukata kwenye sehemu ya jinsia kwamba aidha yeye ni Mwanamke au Mwanamme. Pamoja na Mzee Duni kuwa ni mtu maarufu na mtu ambae ameshahudumu kwenye Serikali kwa miaka mingi na kujieleza mbele ya Tume kuwa yeye ni mwanamme na hiyo kukosa kukata hapo ilikuwa ni kosa la kibinaadamu, Tume haikutaka kabisa kuzingatia hilo na ikaamua kutomteua kugombea.

Tumejiuliza sana hivi kweli Tume hii haifahamu makosa ya kibinaadamu? Mbona Tume hii hii kwenye hizi fomu za uteuzi ilisahau kuchapisha sehemu nzima inayotakiwa kuwemo kwenye fomu kwa mujibu wa kanuni hadi pale Chama chetu tulipowatanabahisha?

Wagombea wa Jimbo la Konde, Bububu, Nungwi na Wete

Ndugu Waandishi, Wanachama wa ACT Wazalendo na Watanzania.

Wagombea wa majimbo hayo manne niliyoyataja wameenguliwa kugombea kwa hoja moja kubwa inayofanana ambayo ni Utumishi wa Umma na kwamba wameshindwa kufata masharti ya kushiriki siasa kwa watumishi wa Umma ya kushiriki kwenye siasa.

Ndugu Waandishi, Kwanza naomba sote tuelewe kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 51(1) (a) mpaka (c) ndio zinapoelezwa sababu zipi zinazotakiwa kuwekwa kama pingamizi dhidi ya fomu ya uteuzi. Sababu zenyewe ni tatu tu ambazo ni

Taarifa za mgombea zilizotajwa hazitoshelezi kumtambua mgombea

Ametoa taarifa za uongo katika fomu ya uteuzi

Fomu ya uteuzi ya mgombea haikuzingatia au haikuwasilishwa kwa mujibu wa masharti ya sheria ya Uchaguzi.

Ndugu Waandishi, katika sababu hizo Hoja ya mtu kuwa mtumishi wa Umma na ambae hakufata taratibu za kuingia kwenye siasa haiendani na sababu zote tatu zilizotajwa na sheria. Tumeieleza Tume hivyo kwenye utetezi wetu.


Hata hivyo, kilichoonekana kuegemewa na Tume na wagombea walioleta Pingamizi ni kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Mtumishi wa Umma (Ushiriki wa Siasa) ya mwaka 2003, Kanuni ya 133 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2014 za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Ndugu Waandishi na Wanachama wa ACT Wazalendo

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imejipotosha sana kwenye jambo hili kwani inafahamu fika kuwa ikiwa Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Sheria za Utumishi na Sheria za Uchaguzi, mtumishi wa Umma ambae anashiriki kwenye siasa pasipo kufata utaratibu uliowekwa na Sheria, Mamlaka ya nidhamu ya kumuadhibu au kumzuia mtumishi huyo asigombee sio Tume ya Uchaguzi bali ni Mwajiri. Na hayo ndio maelekezo ya Kifungu cha 15 cha Sheria Namba 3 ya 2003 na Kanuni ya 133(7) ya Kanuni za Utumishi wa Umma.

Wagombea wetu wote waliwasilisha mbele ya Tume vielelezo vyao ama vya Barua za Likizo bila ya Malipo au Notisi ya kusudio lao la ushiriki kwenye siasa au Barua za Kuacha Kazi. Kwa Mfano, Mgombea Issa Said Juma wa Jimbo la Konde alionesha Barua kutoka kwa Muajiri wake Shirika la Bima ya Tarehe 5 Agosti, 2020 siku 21 kabla Tume haijatoa fomu za Uteuzi akiruhusiwa kuwepo likizo ya kushiriki siasa kuanzia tarehe 28 Julai, 2020.

Mgombea Hassan Jani Masoud yeye alionesha Barua yake ya Kuacha kazi ndani ya masaa 24 kwa mujibu wa Kanuni ya 25 ya Kanuni za Utumishi wa Umma pamoja na slipu ya kurudisha mshahara wa mwezi mmoja kama sheria inavyotaka. Mgombea Hasne Abdalla Abeid ameonesha barua ya kupewa likizo bila ya malipo kutoka kwa Katibu Mkuu wake ya Tarehe 13 Agosti, 2020 akipewa likizo bila ya Malipo kuanzia tarehe 1 Septemba, 2020 yaani siku 9 kabla ya siku ya uteuzi wa iliyowekwa na Tume. Mgombea wa Jimbo la Wete Ndugu Is-Haq yeye alionesha mbele ya Tume barua yake ya kutoa indhari ya kushiriki kwenye siasa iliyotolewa tangu mwezi wa Juni.

Hoja iliyokuwa inatolewa kuwa wameanza michakato ya siasa kabla hawajapewa Barua za Likizo au ndani ya siku zinazotakiwa na Sheria hilo halikuwa ndani ya mamlaka ya Tume bali ni mamlaka ya Muajiri. Tumesikitishwa sana kuona Tume wamejiingiza kwenye kushughulika na jambo ambalo hawana mamlaka nalo kisheria.

Ndugu wananchi, yote hayo ni uthibitisho kuwa Wagombea wetu walikidhi matakwa na sifa za kuteuliwa kuwa Wagombea lakini Tume imeshindwa kabisa kuzingatia hoja na vielelezo vilivyotolewa na badala yake ikaamua kuwakosesha wagombea wetu fursa ya kugombea.

Mgombea wa Jimbo la Chake Chake, Ole na Chonga

Ndugu Waandishi, Wanachama wa ACT Wazalendo na Watanzania

Wagombea wa majimbo matatu niliyoyataja hapo wameondolewa kwenye orodha ya kugombea kwa sababu mbili zinazofanana. Moja ni suala la kudhaminiwa na wadhamini waliomdhamini Mgombea zaidi ya Mmoja na Pili


Viapo vyao kuwa na matatizo. Naomba nichukue fursa hii kuwaeleza wananchi na Wananchama wetu ukweli wa jambo hili na masikitiko yetu kwanini Tume imepuuza hoja zetu.

Wadhamini: Ilielezwa mbele ya Wasimamizi wa Uchaguzi na Tume kuwa katika orodha ya Wadhamini kwenye fomu za Wagombea wetu, baadhi ya majina ya wadhamini wao wanaonekana kuwadhamini wagombea wa chama kingine. Wagombea wetu waliieleza Tume tangu wakati wa Usikilizaji wa Pingamizi hadi wakati wa Rufaa kuwa sio kweli kama wadhamini wao wamewadhamini wagombea wa chama kingine na kwamba kama majina ya wadhamini wao yamejitokeza kwenye fomu za wagombea wengine basi hiyo jinai iliyofanywa makusudi kuwakosesha sifa wagombea wetu.

Wagombea wetu waliwaleta wadhamini wao wote mbele ya Msimamizi wa uchaguzi na kumuomba awaite ndani wakati wa usikilizaji ili watoe ushahidi kuwa wao hawakumdhamini mgombea mwengine na kama majina yao yanaonekana kwengine basi yameghushiwa. Msimamizi wa Uchaguzi alikataa katakata licha ya wahusika kuruhusiwa kuita mashahidi chini ya kifungu cha 51(7) cha Sheria ya Uchaguzi.

Kwahiyo ilikuwa ni dhahiri kuwa Wasimamizi wa Uchaguzi walikuwa wanaufahamu mpango huo wa kutengenezwa wadhamini bandia kwenye fomu za wagombea wa vyama vyengine ambao kiukweli ni vyama rafiki vya Chama cha Mapinduzi lengo ikiwa kutengeneza kosa la kikanuni kwa mujibu wa kanuni ya 15(2) ya Kanuni za Uchaguzi.

Tuliiomba Tume wakati wa usikilizaji wa Rufaa izingatie Hoja ya kwanini Msimamizi wa uchaguzi alikataa kuitwa kwa mashahidi (Wadhamini wanaosemwa majina yao yametokeza kwa wagombea wawili) wakati sheria inamruhusu kufanya hivyo? Kwanini hao wadhamini wanaosemwa kujitokeza kwenye fomu za wagombea wengine havikuletwa kadi zao za vyama vengine jambo ambalo ni takwa la kikanuni? Zaidi ya yote, Hata pale tulipoitaarifu Tume kuwa Wadhamini hao wawagombea wetu wamechukua hatua za kuripoti jinai hiyo kwenye vyombo vya sheria, Tume haijataka kuzingatia.

Viapo Vibovu: Ilielezwa pia mbele ya Tume kuwa Wagombea wetu hao wamewasilisha fomu zao za uteuzi zikiambatana na viapo vibovu hivyo wamefanya makosa chini ya kifungu cha 51(9) na 51(1)(c) ya Sheria ya Uchaguzi. Sasa ubovu unaoongelewa na Tume ni upi? BAadhi ya Wagombea wetu ilionekana kwenye viapo vyao kuftwa kwa wino mweupe kwa lengo la kuandika jina la Chama liweze kuingia kwenye hiyo sehemu ndogo ya kiapo. Na sio kwamba kufuta huko ilikuwa kuandika facts/ taarifa ambazo zilikuwa labda za uongo au zenye kupotosha. HAPANA! Sasa kwa wale wataalamu wa Sheria wanajua kuwa hilo halibatilishi uhalali wa kiapo ambacho kina jina na Saini ya anaeapa na anaeapishwa ikiwemo sehemu kiapo kilipoapishwa.

Ndugu Waandishi na Wanachama wa ACT Wazalendo

Kwa Mgombea wa Jimbo la Kijini,


Yeye ameenguliwa kwa hoja kuwa ameeleza kwenye fomu yake kuwa yeye hana kazi wakati anayo kwa kuwa anamiliki Gari ya Biashara. Hii kwa kweli ilikuwa ni Hoja dhaifu sana kwa tume kuizingatia na kupelekea kumuondolea mtu sifa yay a Kugombea zaidi ya sifa zilizowekwa na katiba na Sheria. Tunasema hivyo kwa sababu kufanya biashara au kutofanya biashara si miongoni mwa taarifa ambazo kutolewa kwake au kutotolewa kwake kunampa au kunamuongozea sifa za uteuzi mgombea kwa mujibu wa Kifungu cha 44 cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2018. Msingi wa hoja hii ndugu waandishi ulijengwa na Tume yenyewe ya Uchaguzi ya Zanzibar wakati wanashughulikia Shauri la Pingamizi alizowekewa Ndugu Seif Sharif Hamad ambapo tume ilitoa ufafanuzi wa ipi ni taarifa ya uongo kwa muktadha wa Kifungu cha 51(1)(b). Tume hii ilisema

“Ili taarifa ionekane iwe ya Uongo basi iwe inaelekeza kupotosha ukweli kwa namna ambayo inamnufaisha mtoa taarifa hiyo” Ukr 4 wa Uamuzi wa Tume.

Tumeiuliza Tume na tunaendelea kujiuliza Hivi mtu akiacha kuandika taarifa ya biashara anayofanya kunamnufaisha vipi mgombea wakati suala la kufanya au kutofanya Biashara sio miongoni mwa Sifa za kugombea Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa Mujibu wa Ibara ya 69 ya Katiba ya Zanzibar na Kifungu cha 44 cha Sheria ya Uchaguzi ?

Mgombea wetu wa Jimbo la Tumbatu

Yeye Hoja ilikuwa usahihi wa Mwaka wa kuzaliwa. Kwamba alieweka Pingamizi anasema Mgombea wetu amezaliwa mwaka 1963 na sio 1962. Tumeshtushwa sana na uamuzi wa Tume wa kuhukumu kuwa katika hili wameibua hoja ya kughushi wakati wanajua hiyo ni jinai na wao hawana mamlaka ya kuhukumia. Zaidi ya hapo, hoja ya aidha 1962 au 1963 sio hoja ya yenye mantiki hata kidogo kwa msingi ule ule kuwa miaka inayobishaniwa haimpi umri wenye kumnufaisha Mgombea ilio aweze kuwa na sifa ya kugombea Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi ukizingatia kuwa umri wa kugombea nafasi hiyo ni miaka 21. Tumeshangaa kuona tume imekiuka misingi yake wenyewe uliouweka ndani ya wiki hiyo hiyo.

Mgombea wetu wa Tumbe

Yeye ameenguliwa kwa kile kilichosemwa kuwa hakutoa taarifa zote za makosa aliyowahi kushtakiwa na kutiwa hatiani. Sasa hayo makosa ambayo ameambiwa hakuyataja ni makosa ambayo mleta Pingamizi na mkata Rufaa wake amesema yamefanywa baina ya mwaka 1981 na 1983. Yaani kabla hata Katiba ya Zanzibar yam waka 1984 haijatungwa. Tume ya Uchaguzi imeikubali hoja hii huku ikijua kuwa linapokuja suala la kutiwa hatiani kwa madhumuni ya kumuondolea sifa Mgombea, basi hatia hiyo iwe imepatikana ndani ya miaka mitano kabla ya uchaguzi. Sasa iweje mtu alietiwa hatiani miaka 40 iliyopita akakose sifa leo? Mgombea huyu pia aliibuliwa hoja ya kuwa hajafika kidato cha Tatu. Hoja hii mfu ilijibiwa ipasavyo kwa Tume kuoneshwa vyeti vya kumalizia shule vya Mgombea. Jambo la kushangaza Tume kwa makusudi wamekataa kuzingatia na badala yake wameegemea eti



barua ya zilizondikwa na Mkuu wa Shule na Afisa Mdhamini wa Elimu Pemba kwa barua alizopelekewa Katibu wa CCM Mkoa Kaskazini Pemba. Cha kushangaza na kuchekesha zaidi ni kuwa Barua baina ya Katibu wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba na Mkuu wa Shule ni barua walizoandikiana tarehe 11/9/2020 baada ya kumalizwa kusikilizwa Pingamizi za asili.



Ndugu Waandishi na Wanachama wa ACT Wazalendo



Hayo ndio yaliyotokea kwenye usikilizaji wa Rufaa na kupelekea maamuzi mliyoyasikia kwenye majimbo niliyoyataja. Narudia tena kusema kuwa pamoja na kwamba tunaheshimu maamuzi ya Tume lakini tunaamini kabisa haikutenda Haki kwa wagombea wetu na Chama chetu kwani hoja za pingamizi walizowekewa wagombea wetu zilizkuwa dhaifu mno na zisizokuwa mashiko ya kisheria.



Kwa bahati mbaya sana, tofauti na ilivyo kwenye Kifungu cha 40 (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ambapo mtu asieridhika na maamuzi ya Tume kuhusu pingamizi za uteuzi anaweza kufungua shauri la uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar haitoi nafasi hiyo kwa mazingira kama hayo. Hata hivyo Chama hakizuiliki kwa mujibu wa Katiba na Sheria kuomba mapitio ya kimahakama (Judicial Review) juu ya maamuzi ya Tume jambo ambalo tutalifanya.



Ahsante kwa kunisikiliza.



Imetolewa na​





……………………………………………



Omar Said Shaaban



Mwanasheria Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo
 

Attachments

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…