kwamtoro
JF-Expert Member
- Nov 15, 2010
- 4,922
- 3,239
| Paul Severin, akiwa nje ya duka lake, kijijini Ovada, Tarafa ya Kwamtoro, Kondoa. PENGINE siku ile ya Novemba 4, mwaka 1998 ilikuwa ni siku ya balaa na isiyoweza kusahaulika, katika maisha ya Paul Severin. Siku hiyo ndiyo aliyodiriki kuutoa uhai wa mwanadamu mwenzake. Kutokana na sababu ambazo hata hivyo anadai anazijutia. Kwa nini aliua? Severin, mzaliwa wa Kijiji cha Ovada, Tarafa ya Kwamtoro, Wilayani Kondoa, Dodoma ambaye ni mfanyabiashara anaeleza kilichomsibu. Anaeleza kuwa mwaka ule, alikuwa na duka lake kubwa ambalo anaeleza kuwa lilikuwa limejaa bidhaa. Kutokana na wingi wa majukumu, nilimwamini rafiki yangu, Dennis Leba, nikamwachia duka ili alisimamie wakati nikifanya mambo mengine, anasema. Anaongeza kuwa aliporudi kuangalia hali ya duka lake, alikuta kuna upungufu wa zaidi ya Sh600,000. Hapo ndipo alipoamua kumhoji rafiki yake. Nilipomwuliza zilipo fedha, alinijibu tena kwa jeuri, kuwa hajui zilipo, na kama akitaka atanilipa, anasema Anaongeza: Niliumia, lakini nikamwachia Mungu. Ila alichoniudhi, ni yeye kujigamba kwa watu akiwaambia kuwa mimi siwezi kumfanya chochote kwa kuwa ni mtoto mdogo sana kwake. Severin anasimulia zaidi kuwa, maneno ya kashfa yalizidi, Leba alikuwa akimtusi, hasa alipokuwa amelewa. Ndipo Novemba 4, , 1998, Severin na wenzake walikuwa wanakwenda katika huduma ya ulinzi shirikishi. Akielekea yalipo makutano yao kabla ya kuanza ulinzi, alimuona Leba akiwa ameketi na wenzake. Hasira za ghafla zilinishika- nikaweka mshale wangu katika upinde- nikaurusha na ukamchoma shingoni. Alikufa pale pale, anasimulia Severin. Anasema, baada ya kuua, alikwenda mwenyewe hadi kituo cha polisi cha Kwamtoro, kilometa 27 kutoka kijijini Ovada, akajikabidhi mikononi mwa polisi. Nilijua nimefanya kosa, nikaenda mwenyewe polisi, lakini polisi walidhani ama nilikuwa nimechanganyikiwa au natania, anasema Baada ya taarifa za kifo kufikishwa polisi, ndipo polisi walipoamini maneno ya Severin, na aliwekwa mahabusu. Kesi yangu ilisikilizwa kwa zaidi ya miaka minne, nilikaa mahabusu kwa muda huo wote, anasema Baada ya kesi yake kusikilizwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania mjini Dodoma, alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela, kwa kosa la kuua bila kukusudia. Maisha yake gerezani yalikuwaje? Severin, anasema, kifungo hicho kwake kilikuwa ni fundisho tosha. Kwani akiwa jela tu, alianza kuishi maisha matakatifu. Nilikuwa nikisoma Biblia na kuomba sana, nikaanza kuwafundisha wenzangu neno la Mungu, niligeuka na kuwa mzee wa kanisa, anasimulia Anasema: Nilikuwa nikifanya kazi kwa bidii na kwa kujituma, sikuwa mkaidi na sijawahi kupigwa na askari magereza hata siku moja kwa kosa lolote lile, kwa kuwa sikuwa nikifanya makosa. Utiifu na bidii ya kazi vilimfanya awe kiongozi wa wenzake, yaani mnyapara. Anaelezea ratiba yake ya kila siku gerezani na kusema, walikuwa wakiamshwa asubuhi sana na baada ya kupata kifungua kinywa cha uji saa moja na nusu, walielekea kazini. Tulipangiwa kazi kila mtu katika eneo lake, wakati mwingine tulipewa mafunzo ya ufundi na askari magereza, jambo ambalo limenisaidia mno, anasema na kuongeza: Nawashukuru sana askari magereza, nilijifunza kushona vikapu na sasa ni hodari. Anasema, saa nane ulikuwa ni muda wa kurudi gerezani na aliutumia wakati huo kusoma neno la Mungu, akiwahubiria na wafungwa wenzake kabla ya kulala. Tukio asilolisahau gerezani Severin amekaa gerezani kwa muda mrefu, ameona mengi, lakini lipo tukio asilolisahau. Siku moja, tukielekea kufanya kazi fulani, mfungwa mwenzetu alimuua mfungwa mwingine, anasema. Anasema, mfungwa huyo alichukua kipande cha kuni na kumpiga nacho kwa nguvu mfungwa mwenzake kisogoni ambaye inasemekana walikuwa na ugomvi. Alimpiga kwa nguvu kiasi kwamba, pigo mmoja tu, liliufanya ubongo wa mfungwa yule kumwagika chini. Tukio hilo, liliniumiza na kunifanya nisile chakula kwa muda wa siku tatu. Msamaha Aprili 25, 2008 baada ya kukaa jela kwa miaka 12, Severin aliitwa kwenye ofisi ya mkuu wa magereza. Alipewa habari ambazo zilikuwa ni mwanga mpya kwake. Niliambiwa kuwa, nimepewa msamaha (parole), hivyo nitatumikia kifungo cha nje kwa miaka iliyobaki, nilifurahi sana, anasema. Anaseama kuwa Juni 20, 2008 kwa kiasi fulani alikuwa huru kwani alianza kutumikia kifungo cha nje kwa miaka iliyobaki. Maisha baada ya kutoka jela Miongoni mwa mambo yaliyomuumiza Severin pengine kuliko kifungo kile alichotumikia, ni kukataliwa na mke wake mpenzi, Bari Antoneta, mara baada ya kutoka jela. Mke wangu hakuwahi kuja kunisalimu jela, kwa miaka yote hiyo, lakini hilo halikunifanya nisimpende. Binti yangu alifariki nikiwa gerezani, lakini mke wangu pia hakuja kunipa taarifa hizo, anasema Anasema, baada ya kutoka jela, alimfuata mke wake na kumwomba waishi kama zamani, lakini mke wake alikataa katakata. Nilikwenda mpaka kwa mzee wa kanisa na kuwaita wazazi wa pande zote, lakini bado mke wangu alinikataa, anasema Severin. Kitendo hicho kilimhuzunisha, lakini si hivyo tu, bali alikuta nyumba yake, mali zake zote wakiwemo ngombe na mbuzi, vimepotea. Ilinibidi kuanza moja, sina mke, mtoto, nyumba wala mifugo. Ilikuwa ni wakati wa huzuni kwangu, anasema. Lakini pia maisha yalikuwa magumu zaidi kwake, kuanza uhusiano mpya na wanakijiji wenzake pale Ovada. Severin anasema alinyanyapaliwa. Wenzake walimkwepa, alikosa marafiki alitawaliwa na zaidi ya upweke. Walikuwa wananiogopa, nafikiri kwa kuwa ni muuaji na nilifungwa jela, anasimulia Severin. Severin anaeleza kuwa alipiga moyo konde, akaanza kulazimisha kuwa karibu na watu, alizungumza nao, kuwasalimu na kuwahoji hili au lile. Ingawa walimnyanyapaa, lakini hakuonyesha chuki kwao, alielewa ni kwa nini wanafanya hivyo. Bado walitawaliwa na hisia kuwa mimi ni muuaji anafafanua Severin. Anasema: Nikaanza kulima, nililima kwa hasira shamba la hekari nane za alizeti, huku nikiuza dagaa. Anasema mwanzoni, wanakijiji waliogopa kununua bidhaa zake, lakini alipiga moyo konde na taratibu walianza kumzoea. Nilijitahidi kuwa mwema kwa watu wote, nilikwenda kuwasalimu hata na ndugu za marehemu niliyemuua,ingawa ilikuwa ni vigumu, anasema. Severin hakupata mapokezi ya kuridhisha toka kwa ndugu za marehemu Leba, lakini alijitahidi kuonyesha ukarimu kwao na hatimaye walianza kumpenda. Nilipotoka niliazimia kuishi maisha mapya ndani ya Kristo, niliokoka na sikutaka kurudi nyuma tena, anasema. Anaeleza kuwa aliendelea na kilimo ambapo awali alipata magunia 40 ya alizeti ambayo yalimpatia mafuta na aliweza kufungua upya duka. Nilifungua duka kubwa, huku nikiendelea na kilimo. Mpaka sasa nina nyumba ya kuishi, ninao mbuzi 30, ngombe 17 na mashine ya kukoboa na kusaga nafaka, anasema. Severin anaeleza kuwa alipata mke mwingine na kwa sasa wamefanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike. Anasisitiza kuwa, jela si mahali pabaya sana kama ambavyo wengi wanapatafsiri. Ile ni sehemu ya mafunzo, kwani pasipo magereza, jamii yetu ingekuwa na wahalifu wengi na amani isingekuwepo, anasema. Anasema, utaratibu wa parole ni funzo kwa wote, kwamba, endapo utafanya mema ukiwa gerezani, basi utapata msamaha. Magereza haina nia mbaya, madhumuni yao ni kufunza na kuadibu, anasema Lakini, Severin anaiomba serikali kuwawezesha wafungwa wanaomaliza vifungo vyao ili wajue pa kuanzia maisha baada ya kifungo. Mimi nilitumia jasho jingi kufikia hapa nilipo, lakini kwa wengine ambao watashindwa kabisa, watajikuta wanafanya tena uhalifu, anashauri Severin. Majirani zake Severin, akiwamo padri wa Kanisa la Africa Inland (AICT) Ovada, Lucas Makumbi anamtaja Severin kama muumini imara na bora kijijini kwao. Severin ni hodari, muungwana, mkarimu na mcheshi. Kila mtu anampenda, anasema Padri Makumbi Padri huyo anasema, pamoja na kuwa alihukumiwa kwa kuua, lakini tabia zake zimemfanya awe miongoni mwa wanakijiji wanaopendwa pengine kuliko wote hapa kijijini. |