marcoveratti
JF-Expert Member
- Sep 21, 2017
- 1,019
- 1,824
DONALD Trump ni Rais wa 45 wa Marekani. Hicho cheo chake sina shida nacho. Trump ni bilionea wa dola, kwa Shilingi ya Nyerere, ni trilionea. Nina kazi muhimu leo na huo utajiri wake.
Trump ni mtu msema hovyo. Ana kiburi. Wengi humuona ni ‘mtambo’, akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Marekani, Nancy Pelosi. Mimi sina shida na hayo yote, nina kazi muhimu na ule mwonekano wa Trump. Mwonekano wa afya.
Juni 14, mwaka huu, yaani miezi miwili na ushee ijayo, Trump atatimiza umri wa miaka 74. Atakuwa anadaiwa miaka sita kutimiza yale makumi manne mawili yaliyoandikwa kwenye maandiko matakatifu, kwamba kuyafikia ni bahati sana.
Pata bahati ya kumuona Trump japo kwa video, akitembea, akisalimiana na watu na kufanya kazi mbalimbali. Jambo moja litakushangaza; uimara wake. Trump yupo vizuri mno kiafya japo umri umekwenda.
Ni nadra kumpata mtu mwenye umri wa Trump halafu awe na nguvu zile. Wengi wakishafikia umri wa miaka 60, habari huwa mbaya. Mwili huzidiwa uchovu, hujikongoja kuliko kuishi.
Kwa nini Trump ni imara? Nikakumbuka; Trump ni tajiri. Ana pesa chafu. Hana shida, kwa nini asiwe alivyo?
Nikamkumbuka Warren Buffett. Binadamu mwenye pesa ndefu kupindukia. Mara kadhaa alishaorodheshwa kama tajiri namba moja duniani. Na mara nyingi yumo ndani ya Tatu Bora. Buffett ana umri wa miaka 89. Babu sana. Hata hivyo, anadunda, afya nzuri. Anaingia ofisini kufanya kazi zake vizuri.
Namtazama pia Carlos Slim Helu. Bonge la bilionea katika sarafu ya The Fed. Muongo wa kwanza wa Milenia ya Tatu, Carlos alitamkwa mara nyingi kuwa tajiri namba moja dunia. Pata picha ya umri wake. Ni miaka 80. Hata hivyo yupo imara utadhani ana miaka 60.
Sasa nataka kukubaliana na mwandishi wa jarida la Forbes, Teresa Ghilarducci, katika andiko lake la Mei 2019 lenye kichwa “The Rich Have More Of Everything… Including Lifespan”. Kwamba matajiri wana zaidi ya kila kitu ikiwemo umri wa kuishi.
Tafsiri ya andiko kwa kujumlisha utafiti ambao uliambatanishwa ili kushibisha maudhui, ni kwamba matajiri wanapata zaidi, hata umri wa kuishi. Matajiri huishi miaka mingi kuliko maskini.
Teresa aliandika kuwa utafiti unaonesha watu wenye kipato cha dola 12,000 (Sh28 milioni) kwa mwaka, uwezekano wa kufariki dunia mwaka unaofuata ni uwiano wa 1.30. Yaani asilimia 30 zaidi ya wastani wa kawaida.
Akaandika pia, wale wenye vipato vya dola 250,000 (Sh575 milioni) kwa mwaka, uwiano wao wa kufa mwaka unaofuata ni 0.70, yaani chini ya asilimia 30 ya wastani wa kawaida.
Kwa kipimo kilekile cha Trump, Buffett, Carlos na matajiri wengine, niliweka kusudi la kukubaliana na wanasayansi (madaktari) wa mtandao wa WebMD, ambao Julai 7, 2015 waliandika “Rich People Die Differently”. Matajiri hufa kitofauti.
Katika andiko hilo, imebainishwa kwa utafiti wao kuwa watu wenye utajiri kuanzia dola 70,000 (Sh161 milioni) na kuendelea, maumivu ambayo huyapata kuelekea vifo vyao ni theluthi moja ya yale ambayo maskini huyapitia.
Wameeleza kuwa uchovu wa mwili na mgandamizo wa mawazo kwa maskini kipindi cha kuelekea vifo vyao ni mkubwa mno, ukilinganisha na matajiri.
Nikamleta mawazoni bilionea mzee zaidi duniani, Chang Yun Chung, ambaye ni bosi wa kampuni ya usafiri wa majini ya Pacific International Lines (PIL) yenye makao makuu yake, Singapore. Ana umri wa miaka 101, anaifukuza 102.
Mpaka leo, Chang anaingia ofisini kufanya kazi kama kawaida, licha ya kwamba Agosti 2018, alimkabidhi mwanaye, Teo Siong Seng, ubosi wa PIL. Unabishaje kuwa matajiri wanaishi muda mrefu kwa afya bora?
NJOO SASA AFRIKA
Bahati mbaya, huo utafiti wa kuonesha matajiri wanaishi vizuri miaka mingi na hufa bila maumivu, bila shaka haukufanywa Afrika. Kama wangechukua sampuli japo 10 za matajri wa Afrika katika utafiti wao, wangetoa ripoti tofauti.
Afrika, kadiri mtu anapoongeza kiwango chake cha utajiri, ndivyo wasiwasi unavyoongezeka. Maisha ya tabu yanamsogelea. Magonjwa yasiyoambukiza, hasa presha na kisukari huweka maskani kwenye mwili wake. Katika matajiri wa Afrika, ni wachache mno hupata nafasi ya kufurahia utajiri wao.
Afrika, ni bara ambalo matajiri huishi katikati ya hofu ya kufilisiwa. Ndio maana, Afrika, matajiri hujiona salama kujipendekeza kwa watawala.
Afrika, matajiri hutumia muda mwingi kuwaza kuibiwa na kufilisika. Hiyo ni sababu saa nyingi huzitumia kazini. Hukosa hata muda wa kutosha na familia zao.
Afrika, ndio bara ambalo kuna matajiri wengi huamini nguvu za giza zinalinda utajiri na kuuongeza. Waganga wa kienyeji hutengeneza fedha nyingi kupitia matajiri wa Kiafrika.
Afrika, matajiri hawatakiwi kupenda vyama vya upinzani. Wakigundulika imekula kwao. Mamlaka za kodi zitabisha hodi. Watapewa malimbikizo ya kodi hata ya kipindi ambacho kampuni haijazaliwa.
Uzuri hufahamika kuwa tajiri anapopelekewa malimbikizo ya kodi hata ya nyakati hajazaliwa, hujua anatakiwa kufanya nini. Kuunga mkono utawala. Akijifanya kukomaa, kuna jela au kufilisiwa.
Afrika, ndio bara ambalo taasisi ya kibiashara yenye kutoa ajira 50,000, inaweza kufungwa kwa sababu za kisiasa. Afrika, watawala huwaonea makusudi wafanyabiashara wasiofungamana nao.
Mpaka hapo, nikuulize; matajiri wa Afrika wana raha gani ya kufurahia utajiri wao? Wanazungukwa na wasiwasi kila upande. Watawala, wezi makazini na uchawi. Muda wote inabidi wawe macho maifisini. Hawachukui hata likizo ya miezi miwili kwa mwaka angalau kula maisha na kufurahia utajiri wao.
Wanakuwa watumwa wa pesa na watawala. Fedha atafute yeye kwa jasho na maumivu mengi, lakini akiulizwa siri ya utajiri wake anamshukuru kiongozi aliye madarakani.
Pesa zake, hawezi hata kusema aende Norman's Cay kupumzika mwezi mmoja, afurahie maisha na jasho lake la utafutaji, lakini kuna kiongozi anapiga simu moja kuagiza mamilioni na yanamtoka.
Halafu hayo mamilioni anahongwa mwanamke mchepuko wa kiongozi serikalini, ambaye anakwenda kula bata na kufanya shopping za Gucci na Miu Miu, Paragon Shopping Mall, Singapore.
Afrika, kuna matajiri familia zao hazina furaha. Ukiambiwa “huyu ndiye mke wa bilionea” unabaki kutoa macho, mke au msukule? Hafanani. Mke akiomba pesa, mume anamjibu hakuna. Kisha, kuna kiongozi fulani akitaka pesa, zinatoka.
Afrika, kuna wanaokula bata lakini hizo pesa wanazolia bata hawajui zimetafutwaje. Wanatumia tu. Na kuna wanaotafuta pesa lakini hawajui zinatumiwaje. Wanatoa tu.
Inawezekana Afrika ilitakiwa iwe sayari inayojitegemea, lakini Mungu alipoona tungemalizana kwa visasi, roho mbaya, husuda, kukamiana, kukomoana na ushirikina, akaiweka duniani. Ila kiukweli, Afrika ni sayari ya kivyake.
Afrika, tajiri anaweza kuogopa kuwasiliana na ndugu yake, kisa ni mwanasiasa wa upinzani. Anahofia kumkasirisha mtawala. Matajiri wa Afrika ni binadamu wanaoteseka sana.
Afrika, mtu ambaye maisha yake yanampa uhakika wa kula na kulala, ana furaha kuliko tajiri. Ana afya nzuri. Hasumbuliwi na presha wala kisukari.
Afrika, tajiri anajenga bifu na maskini. Na anatumia fedha na connection za kiserikali ili kummaliza. Badala ya kutumia mamiloni kula bata, atayatumia kununua bunduki aue mbu.
Angalia matajiri wa duniani; hawana stress za siasa. Ndio maana unaweza kusikia kila mwaka, Falcom 900 EX ya Mukesh Ambani, tajiri namba moja Asia, imetua KIA. Mtu mzima amekuja kula bata Serengeti.
Akina Bill Gates, wanatafuta pesa na kuukuza utajiri wao ili wajenge kesho bora ya watoto na wajukuu vizazi kwa vizazi, watengeneze legacy kwa jamii, ndio maana wanatoa sana misaada. Kisha sasa, ni kuishi maisha yao. Kula bata za daraja la kwanza.
Unawaona Gates na Buffett wanacheza Ping-Pong kitajiri. Maisha yanataka utulivu na usahaulifu wa presha za kazi. Unamuona Jeff Bezos ‘amejikarantini' kisiwani Laucala, Thurston Point, mwezi mzima. Unatafuta hela ili iweje?
Trump, anashutumiwa kuwa tangu awe Rais, hufanya ziara za kila mwezi kwenye uwanja wake wa gofu, National GC, Washington DC. Mtu mzima anakwenda kucheza gofu na kusahau mambo ya The Oval Office, White House.
Ndio sababu matajiri wa nje ya Afrika wanaishi miaka mingi na afya. Hawawazi kufurahisha wanasiasa, wala hawaogopi kuweka wazi mapenzi yao ya kisiasa. Na wanaowapenda wakishindwa uchaguzi, bado ni salama. Hawaibuliwi makimbikizo ya kodi.
Matajiri wa duniani huwakuti kwenye bifu na maskini. Hawakutani na shinikizo la kutoa pesa kwa viongozi wa kisasa eti ili wawe huru na salama. Wanafanya kazi, wanatanua ngome za kibiashara, wanatoa misaada kwa wahitaji, kisha wanaishi maisha yao. Bata tu. Presha zitoke wapi? Lazima wachelewe kufa.
Mwaka 2008, Reginald Mengi, alilalamika kwenye vyombo vya habari kuwa mmoja wa mawaziri alipeleka pendekezo Baraza la Mawaziri eti Serikali imfilisi. Ni kipindi ambacho ilisemwa sana kuwa Mengi alikuwa mpinzani.
Moise Katumbi alipotokeza kutaka kupimana ubavu na Rais Joseph Kabila, ndipo Serikali ya Kinshasa iligundua Katumbi alikuwa mkwepa kodi. Akafungwa. Ni Afrika.
Afrika, matajiri hawapewi thamani wanayostahili kama walipa kodi, waajiri na wajenga uchumi wa nchi. Endapo watakosana na watawala, mazuri yao yote hugeuka uhalifu. Chifu MKO Abiola aliuawa gerezani Nigeria, Julai 7, 1998, kisha fedha zake benki zilichotwa hovyo, familia yake haikuambulia chochote. Ndio sababu Afrika, matajiri huamua kulamba miguu watawala.
Afrika, watawala hujiona wana mamlaka ya kuwaendesha matajiri na utajiri wao wakati hawajui ulipatikanaje. Na matajiri kwa hofu ya kupoteza utajiri wao, huamua kutii kila agizo.
Afrika, matajiri hutegemea ushauri wa wapambe wasio na maarifa yoyote ya bashara. Ushauri wao ni michongo ya ushirikina na wanawake. Unakuta tajiri anamsikiliza mpambe kuliko mkewe.
Ukweli ni kuwa maisha ya matajiri Afrika ni mafupi kwa sababu ya mazingira ya siasa za nchi na mitindo yao ya kimaisha. Furaha inaanzia nyumbani lakini mke hawaelewani. Watoto hawapo huru kwa baba yao.
Sina maana kila tajiri Afrika ale bata kama la Roman Abramovich, anavyozunguka dunia na Bandit au Mukesh anavyokula raha zote za dunia ndani ya Antilia, 27 storey building, la! Kila mmoja ale kwa urefu wa kamba yake.
Lazima kujiachia. Hivyo ndivyo kurefusha maisha. Unakuta mzee anaonekana kijana. Anaishi vizuri. Afrika, mtu akipata utajiri, ghafla anaanza kuzeeka. Akili zinakuwa za kizee. Anajibana mpaka mateso. Anafanya kazi bila kupumzika, anajiua taratibu.
Nyumbani haelewani na mkewe, anazidi kujiua. Watawala nao wanawapa presha nyingi. Ni vigumu kukuta matajiri Afrika wenye zaidi ya umri wa miaka 80. Maisha yao ni mafupi sana. Sijui wanatafuta pesa wafanyie nini? Hawana raha nazo kabisa.
Muone Mo Ibrahim anavyoishi. Alivyo huru na mwenye fikra pana. Ni kwa sababu alichukua uraia wa Uingereza. Angeendelea kuwa raia wa Sudan, Afrika, na yale maono yake, ama angeshafilisiwa au angeshakufa.
Mwaka jana niliona Yusuf Manji alikamatwa Marekani kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa. Hivi kesi yake iliisha? Hili la Manji nimeuliza tu, lipo nje ya mada yetu hii.
Sent using Jamii Forums mobile app