SoC02 Afya Yetu Watanzania

Stories of Change - 2022 Competition
Joined
Aug 18, 2022
Posts
11
Reaction score
4
Afya; Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, ni hali ya ustawi kamili wa kimwili, kiakili na kijamii na sio tu ukosefu wa magonjwa na udhaifu.

Kuna aina mbalimbali za afya kama vile afya ya kimwili, kiakili, kiroho, kihisia na kijamii. Afya inaweza kukuzwa kwa kuhimiza shughuli zenye afya kama vile mazoezi ya kimwili ya kawaida, kuzingatia chakula bora na usingizi wa kutosha, hii inajumuisha na kupunguza au kuepuka shughuli au hali zisizofaa zinazohatarisha afya kwa namna moja au nyingine kama vile kuvuta sigara, lishe duni au mkazo mwingi (stress).

Baadhi ya mambo yanayoathiri afya yanatokana na uchaguzi wa mtu binafsi, kama vile kujihusisha na tabia hatarishi, huku mengine yanatokana na sababu za kimuundo, kama vile iwapo jamii imepangwa kwa njia inayorahisisha au vigumu kwa watu kupata. huduma muhimu za afya. Licha ya hayo bado, mambo mengine ni zaidi ya uchaguzi wa mtu binafsi na wa kikundi, kama vile matatizo ya maumbile.

Afya ni moja kati ya mambo muhimu sana kwa maendeleo ya kila mtu, jamii na taifa kwa ujumla wake kwani bila ya kuwa na afya bora hakuna kinachoweza kufanyika kwa ufasaha. Nachelea kusema kwamba afya bora ndio msingi imara unaojenga taifa imara.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na mambo kadha wa kadha yanayohatarisha afya zetu sisi kama watanzania. Licha ya juhudi mbalimbali zinazofanyika na serikali kupitia wizara ya afya katika kutoa miongozo mbalimbali itakayochochea afya bora kwa watanzania wote ambayo pia ina faida na hasara zake.

Hivyo hakuna budi zichukuliwe hatua madhubuti katika kukuza na kuboresha afya za watanzania ambao ndio wahusika wakuu katika mustakabali na maendeleo ya taifa letu kwa ujumla. Makala hii inaenda kuangazia baadhi ya masuala mtambuka ambayo yatachochea mabadiliko katika sekta ya afya. Aghalabu, afya bora ni matokeo ya pamoja kati ya juhudi za serikali pamoja na juhudi za wananchi wenyewe katika kuboresha afya zao.

Mosi, kupima afya mara kwa mara. Imekuwa kawaida kwa watanzania wengi kuwa na desturi ya kupima afya mpaka kuwe na jambo/msukumo fulani kutoka nje. Mfano ikifika wakati wa kupata ajira mpya au kujiunga na taasisi flani.

Hii inafanya watu kupima afya zao kwa sababu hiyo tu na sio kwa mustakabali wa afya binafsi. Ni wakati sahihi sasa kuacha na haya mazoea na kubadili mtazamo kuhusu kupima afya. Kupima afya mara kwa mara husaidia mambo mengi ikiwemo kujua muenendo wa afya ya mtu husika ambayo husaidia kugundua dalili mapema hivyo kuchukua hatua mapema ili kujiweka vizuri. Watanzania tupime afya zetu mara kwa mara kwa faida ya yetu sisi wenyewe na sio mpaka hamasa flani kutoka nje.

Pili, kujiunga na mifuko mbalimbali ya bima ya afya. Ni ukweli usiopingika kwamba gharama za matibabu zipo juu sana kwa mwananchi wa kawaida kuzimudu. Na gharama hizo zipo juu zaidi ikiwa hauna bima yoyote ya afya.

Ni wakati muafaka sasa watanzania tujiunge na mifuko ya bima ya afya kwa ajili ya matibabu yetu sisi wenyewe. Uzuri ni kwamba nchi ina makampuni na taasisi nyingi zinazotoa huduma ya bima ya afya hivyo ni vyema kutumia faida hii kupata huduma ya bima ya afya ili kupata matibabu pale itakapohitajika.

Pia ni jukumu la serikali kuhimiza watanzania wa hali zote kujiunga na hii mifuko ya bima ya afya. Ni kweli kuna baadhi ya sehemu za kimatibabu huduma za afya kwa wenye bima ni tofauti na kwa wanaolipia (cash) lakini hiyo haiondoi umuhimu wa bima ya afya kwa ajili ya kupata huduma za matibabu.

Tatu, kushiriki katika midahalo na mihadhara mbalimbali kwa lengo la kuchangia mitazamo, maoni na mawazo mbalimbali. Watanzania tuamke na kushiriki katika majukwaa haya kwa tija na maendeleo ya sekta ya afya nchini kwetu.

Kwani ujenzi wa misingi imara ya afya ni matokeo ya kushiriki kwa pamoja kati ya serikali, taasisi zinazohusika na maswala ya afya bila kusahau wananchi wenyewe. Hii itachochea uwanda mpana katika kuboresha afya zetu wenyewe.

Nne, serikali kupitia kwa wizara ya afya itengeneze mazingira bora na wezeshi kwa maendeleo ya sekta ya afya nchini. Hii itachochea maboresho na mapinduzi kwenye sekta ya afya kwa kiwango kikubwa. Serikali na taasisi binafsi za afya ziajiri watumishi wengi wenye sifa stahiki katika kada ya afya ili kupunguza uhaba wa watumishi wa afya.

Hii inakwenda sambamba pamoja na kuboresha mazingira ya kutoa huduma za afya kwa kujenga vituo bora na vya kisasa kwa kutolea matibabu pia, kununua vifaa tiba vya kutosheleza kutoa huduma za afya kwa wananchi wote wa mijini na vijijini. Hatua hii itaboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watanzania.

Tano, mamlaka za afya zilizo chini ya wizara ya afya zitimize wajibu wao na majukumu kwa kadiri ya sheria za kuanzishwa kwake. Mamlaka hizi ni muhimu sana kwa mustakabali wa sekta yetu ya afya. Mamlaka kama vile TMDA, NIC, GCLA na MSD zinapaswa zitimize wajibu wao kisheria ili kuboresha mazingira ya utolewaji wa huduma za afya hivyo kupelekea huduma bora za afya kwa wananchi wote katika sekta ya afya. Hii iende sambamba na wajibu na uwajibikaji bora (responsibility and accountability) kwa watumishi wa kada ya afya ili kuzidi kuboresha sekta ya afya kwa ujumla wake.

Sita, watanzania tushiriki katika kutunza mazingira yetu yanayotuzunguka ili kuboresha afya kwa mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla. Kwani afya bora ni matokeo pia ya mazingira safi na salama. Hii inajumuisha pia kwa kuacha tabia zote zinazohatarisha afya zetu wenyewe kama vile kujitibu magonjwa nyumbani, kutopata lishe bora ili kujenga miili yetu, ngono zembe, msongo wa mawazo (stress), ulevi uliokithiri pamoja na matumizi ya madawa ya kulevya. Pia watanzania tujifunze njia na mbinu mbalimbali za kujiepusha na magonjwa mbalimbali ambayo ni rahisi kuepukika kwa juhudi za awali.

Hitimisho; Afya bora ni matokeo ya juhudi za pamoja kati ya wananchi, jamii, taasisi za kiafya, na serikali kwa ujumla. Hivyo basi, shime sasa watanzania tuungane kwa pamoja katika kukuza na kuendeleza sekta yetu ya afya kwa maendeleo yetu sisi wenyewe, jamii zetu na taifa letu kwa ujumla. Hii ni kwa kutimiza majukumu yetu ipasavyo.
 
Upvote 2
Karibuni wanajukwaa kwa maoni, mawazo, mapendekezo na ushauri. Bila kusahau kupigia kura ilo andiko. Asanteni
 
Kuna swala la Afya ya akili pia linatakiwa lipewe kipaumbele kwani linaweza kusababisha hata sehem nyingine za mwili kuzoofika na kuweza kushambuliwa kirahisi na magonjwa.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…