Msanii
Agness Suleiman maarufu kama
Aggy Baby, ameibuka mshindi wa
Tuzo ya Muigizaji Bora wa Kike wa Mwaka 2025 katika
Achievers Awards International zilizofanyika nchini Nigeria, kutokana na mchango wake katika sanaa na huduma kwa jamii.
Tuzo hiyo imeelezwa kuwa ni alama muhimu ya
ushirikiano wa kiutamaduni kati ya Tanzania na Nigeria, ikionesha jinsi filamu za Kitanzania zinavyovutia kwa kuonesha amani, utu na mshikamano wa Kiafrika. Hata hivyo, tuzo hiyo imeibua
mjadala mkali mitandaoni.
Wapo wanaomupongeza Aggy Baby wakisema kuwa ni hatua kubwa kwa msanii wa kike kutoka Tanzania kutambulika kimataifa, hasa katika anga la Nollywood lenye ushindani mkubwa. Wanadai kuwa tuzo hiyo ni matokeo ya jitihada zake kujitangaza na kuwakilisha Tanzania katika matukio mbalimbali ya kimataifa.
Lakini upande mwingine wa mashabiki na wadau wa filamu umeonesha
mashaka makubwa, wakidai hawajawahi kumuona Aggy Baby katika filamu au tamthilia yoyote nchini. Baadhi wanasema zaidi ya kufanya
mahojiano ya kujivuna na kukebehi, hawajaona kazi halisi ya kisanii inayoweza kustahili tuzo hiyo.
Mjadala huu umeibua swali kubwa:
Je, tuzo hizi za kimataifa hutolewa kwa kipaji halisi au kwa ushawishi wa umaarufu wa mitandao ya kijamii?
Wadau wa filamu wanashauri tuzo kama hizi ziwe na
uwazi na vigezo vinavyoeleweka, ili kuondoa hisia za upendeleo na kulinda heshima ya wasanii wa kweli wanaofanya kazi kwa bidii.
Kwa upande wake, Aggy Baby hajatoa tamko rasmi zaidi ya kuandika kwenye ukurasa wake wa Instagram. Hata hivyo, mjadala huu unaendelea, huku watanzania wakisubiri kuona kama kweli tuzo hii itazaa matunda ya kimataifa kwa filamu za Bongo.