SoC02 Ahadi za wabunge na akili za wapiga kura

SoC02 Ahadi za wabunge na akili za wapiga kura

Stories of Change - 2022 Competition

Bosi Kalewa

Member
Joined
Aug 27, 2022
Posts
7
Reaction score
4
Unapotazama maamuzi ya serikali wakati mwingine inashangaza sana. Ukisikiliza kauli za wanasiasa inashitua mno. Lakini kubwa kuliko na kinachonyong'onyesha akili, mifupa, mapafu na nyoyo ni mitazamo, fikra, upeo na kila kitu kutoka kwa raia au kwa maana nyingine wapiga kura wenyewe.

Yawezekana kwa aina ya tawala za Kiafrika, Watanzania ndiyo watu pekee ambao ni rahisi mno kuwaongoza. Yaani kuwaongoza Watanzania ni rahisi kuliko kufanya mazungumzo ya faragha na mkeo. Lakini ukitembea ndani ya taifa hili unagundua kuwa ni taifa gumu sana kuliongoza na kufikia malengo.

Utawaongoza ndiyo, lakini kuna faida gani kuongoza watu ambao hawakuelewi kiongozi wao unataka nini, na kibaya zaidi wao wenyewe hawajui wanataka nini. Muelewa anataka umuongoze katika jambo analoliamini. Asiyemuelewa anataka umuongoze tu ili mradi naye kaongozwa.

Niwapo nje ya Dar (mikoani) napenda kujichanganya na watu ili kuwasoma fikra na mtazamo wao. Na zaidi kupata taswira halisi ya maisha ya Mtanzania. Ndiko kwenye uhalisia wa kile tuambiwacho na watawala, wanahabari na mshirika ya umma na binafsi.

Wiki iliyopita nilikuwa katika moja ya mikoa ya katikati ya nchi. Licha ya kutumia wikiendi yangu kwa kukaa maeneo ya watu wenye nafuu ya maisha na elimu vichwani. Lakini picha niliyoondoka nayo nimegundua kuwa tatizo la nchi hii siyo viongozi wala wanasiasa. Inatosha kusema tuna matatizo.

Watu wazima na akili zao matumbo yamewavimba kama 'matenki' ya mafuta. Jasho linawatoka kwa kelele zenye muingiliano na lugha isiyo na staha. Wamekaa wanamsifia mbunge wao kuwa kawajengea barabara ya kilometa kadhaa. Mtu unajiuliza mbunge gani wa kujenga barabara hata ya kilometa moja jimboni?

Wao wanasifia kwa maana ya kwamba mbunge ndiye aliyejenga barabara. Huku wakimponda mbunge aliyetangulia kabla, kwamba hakuwahi kujenga hata choo cha shule. Kinachotokea ni kwamba wabunge wengi wanabebeshwa mzigo usio wao, kwa sababu ya wao wenyewe kutoa ahadi ya kufanya mambo ambayo siyo jukumu lao.

Wabunge wanaingia kwenye kampeni kama mapedeshee kwa kutoa ahadi kibwege bwege tu. Na wananchi nao kwa sababu wanataka kusikia mambo mazuri tu huingia mkenge. Kwa sababu raia hawapendi kuahidiwa mipango wanataka kuahidiwa vitu.

Kwenye kampeni waambie ukiwa mbunge utawaletea ndege ya kuwapeleka kanisani na misikitini na sokoni. Utachaguliwa kwa kura zote. Lakini ukiwaambia kuwa ukiwa mbunge utashirikiana na wananchi ili kuhakikisha ndege zinanunuliwa. Utapigiwa kura na mkeo tu kama siyo mume.

Watanzania wapo hivyo. Wanataka kufanyiwa kila kitu siyo kushirikishwa kufanya kitu. Mgombea bora kwenye masikio wa Watanzania ni yule muongo muongo, anayeahidi jambo yeye kama yeye na siyo kwa kushirikiana na raia wake. Tunapenda kudanganywa na tunajivunia hilo.

Wananchi hawajui kabisa kuwa ahadi za wabunge wakati wa uchaguzi huwa zinatekelezwa vipi. Kwa pesa zao wenyewe? Ruzuku za ndani ya chama cha mgombea? Au kwa bajeti ya serikali? Wengi huamini ahadi za mbunge zinatekelezwa kwa pesa ya mfukoni mwake.

Lakini kwa serikali za Kiafrika, elimu ya uraia ni kitendawili kutolewa. Kwa sababu wanaotakiwa kutoa hawataki kuamsha waliolala ili wajue haki zao za kiraia. Bado tupo na wale wale maadui tulioachiwa na Mwalimu, ambao ni maradhi, umasikini na ujinga.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom