Aina za Uponyaji wa Kiroho

Aina za Uponyaji wa Kiroho

John Magongwe

Member
Joined
Jan 4, 2024
Posts
71
Reaction score
119
Aina za Uponyaji wa Kiroho

Uponyaji ni nini

Uponyaji ni tendo la kiimani la kupokea uzima katika roho au mwili kwa njia ya kuombewa, kuwekewa mikono au kulisikia neno sahihi la Yesu Kristo. Tendo hili la kiimani humletea muumini uzima wa kiroho na afya ya kimwili pale ilipopunguka. Wengi walipoponywa udhaifu wa miili yao, waliponywa pia na roho zao.
Kumbuka kuwa furushi la uponyaji lilikwishaachiliwa pale msalabani. Maana, Yeye mwenyewe Yesu Kristo alizichukua dhambi zetu katika mwili wake, ili tulipokuwa wafu kwa dhambi zetu, tuwe hai kwa mambo ya haki. Kwa kupigwa kwake, sisi tumeponywa (1Petro 2:24).
Uponyaji haufanywi na mtu yoyote yule isipokuwa Mungu. Hata madaktari bingwa, wao hawaponyi bali hutoa tiba tu. Wanaweza kutoa tiba lakini mgonjwa asipone. Mwenye kuponya ni Mungu. Aidha, watumishi wa Mungu pekee, ndio hufanyika kama daraja au chombo cha kuleta uponyaji ulioachiliwa kwao na Bwana, kwa mhusika mwenye kuhitaji (Mathayo 10:8).

Aina za uponyaji wa kiroho

Uponyaji kwa njia ya kuwekewa mikono

Mtu aliyekuwa dhaifu anaweza kupokea nguvu ya Mungu kwa kuwekewa mikono na mtumishi wa Mungu. Hata kama mtumishi hakuukemea udhaifu huo, lakini kitendo cha kuweka mikono yake juu ya kichwa cha mgonjwa ni dawa tosha ya kuleta uponyaji. Maana imeandikwa; “watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya” (Marko 16:18).

Uponyaji kwa kuombewa
Mtu dhaifu wa mwili anahitaji kuombewa ili apokee uponyaji wake. Kwa kuombewa, mgonjwa anaweza akawa China (katika bara jingine), na mtumishi wa Mungu akawa Tanzania (Afrika bara jingine), lakini uponyaji ukafanyika saa ile ile ya maombezi, kwani maombi hayana umbali (Mathayo 17:18). Mara nyingi njia ya kuombewa huambatana pia na kuwekewa mikono (Matendo 28:8).

Uponyaji kwa kulisikia neno la Yesu Kristo
Kuna wakati ambapo mtu aliyekuwa dhaifu huponywa kwa neno la Mungu tu, kwa sababu neno la Mungu ni silaha tosha. Mtu mwenye imani ya uponywaji, akifungua moyo wake na kuliruhusu neno la Bwana liingie, basi ujue neno halitapita bure, ni lazima liponye, ligange, lihuishe kila kitu ndani ya mwili na roho pia (Isaya 55:10-11).

UPONYAJI KWA KARAMA NA UPONYAJI KWA IMANI
Kimsingi, Yesu aliponya kwa njia mbili tofauti: (i) Kwa kufundisha Neno la Mungu ili kuwatia moyo wagonjwa wawe na imani ya kuponywa, na (ii) Kwa kufanya kazi katika karama za kuponya, kadiri Roho Mtakatifu alivyopenda. Katika huduma Yake ya kuponya, Yesu alikuwa na mipaka aina mbili: (i) Kutokuamini kwa wagonjwa, na (ii) Mapenzi ya Roho Mtakatifu kutaka kujidhihirisha kupitia “karama za kuponya”.

Mfano wa Yesu kutumia Karama ya Kuponya
Huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Betzatha, nayo ina matao (vibaraza) matano. Ndani ya hayo matao, jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, (wakingoja maji yachemke; kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika ile birika, akayatibua maji, basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata).
Palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia, simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda (Yohana 5:2-9).

Tunajuaje kwamba mtu huyu aliponywa kwa njia ya “karama ya kuponya” na si kwa imani yake? Kwanza: mtu huyu hakuwa anamtafuta Yesu, badala yake, Yesu alimkuta ameketi kando ya birika. Kama mtu huyo angekuwa anamtafuta Yesu, hiyo ingekuwa ishara kwamba ana imani kwa sehemu fulani. Pili: Yesu hakumwambia huyo mtu kwamba imani yake imemponya, kama alivyokuwa na kawaida ya kufanya mara nyingi alipowaponya watu. Tatu: wakati huyo mponywa alipohojiwa baadaye na Wayahudi kwamba nani amemwambia “simama uende”, alijibu kwamba wala hakumjua. Kwa hiyo, ni hakika kabisa kwamba si imani yake katika Yesu iliyosababisha uponyaji huo, bali ni mtu aliyeponywa kwa njia ya “karama ya kuponywa” iliyodhihirishwa kama Roho Mtakatifu alivyopenda.

Mfano wa Petro kutumia Karama ya Kuponya

Hebu tuangaliea kwenye kitabu cha Matendo ya Mitume 3:1-8:
1 Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa.
2 Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. 3 Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka.
4 Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi. 5 Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. 6 Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. 7 Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. 8 Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu.

Hapa tunaona kuwa kiwete alikaa kwenye mlango wa hekalu siku zote kwa lengo la kuomba msaada kutoka kwa waingiao hekaluni. Hakuomba uponyaji kwani hakuwa na imani, kwa sababu ndiyo kwanza mitume wa mwanzo walikuwa wameanza kufanya kazi za utumishi wa Mungu. Kilichotokea hapa ni uponyaji kwa njia ya karama ya kuponya, uliofanyika kupitia Petro, AKIWA NI MTUMISHI WA MUNGU, kama Roho Mtakatifu alivyopenda.

Tukumbuke kuwa karama ya uponyaji hainunuliwi kwa fedha, kwani ile ni nguvu ya kiroho kutoka kwa Mungu, kama inavyoamuliwa na Roho Mtakatifu, wala siyo bidhaa inayoweza kushikika mkononi. Ndiyo maana katika matendo ya Mitume 8:20, Petro alimwambia yule mchawi Simon aliyetaka kutoa fedha ili apewe karama ya uponyaji, kuwa “Fedha yako na ipotelee mbali pamoja na wewe, kwa kuwa umedhamiria ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali”.

Siyo kila mtumishi wa Mungu ana karama ya uponyaji. Aidha, siyo kila kanisa lina mtumishi wa Mungu mwenye karama ya uponyaji. Wengine wana karama nyingine, kama vile uinjilisti, ualimu, uchungaji, utume, unabii, miujiza, nk, lakini hawana karama ya uponyaji (1Wakorintho 12:4-11). Ambapo, 1Wakorintho 12:11 inasema kuwa “LAKINI KAZI HIZI ZOTE HUZITENDA ROHO HUYO MMOJA, YEYE YULE, AKIMGAWIA KILA MTU PEKE YAKE KARAMA APENDAVYO YEYE”. Hivyo, kama una tatizo la kiuponyaji, TAFUTA KANISA SAHIHI, AMBALO MIONGONI MWA WATUMISHI WAKE, KUNA MTUMISHI WA MUNGU MWENYE KARAMA YA UPONYAJI.

Mfano wa mtu kuponywa kwa imani yake

Batimayo alikuwa kipofu aliyeponywa kwa imani yake kwa Yesu (Marko 10:46-52).
Wakafika Yeriko. Hata alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko pamoja na wanafunzi wake na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando yanjia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo! Inuka, anakuita. Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu. Yesu akamjibu akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu! Nataka nipate kuona. Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.

Hapa, kwanza: Yesu hakumtafuta Batimayo. Hii ni kinyume kabisa na mambo ya pale penye mlango wa kondoo penye birika. Ukweli ni kwamba Yesu alikuwa anampita, na kama Batimayo asingepaza sauti, Yesu angeendelea kutembea na angepita. Maana yake ni kwamba Batimayo asingeponywa. Ingekuwaje kama Batimayo ameketi hapo na kujiambia hivi: “Kama ni mapenzi ya Yesu mimi niponywe, atakuja nilipo, aniponye”? Nini kingetokea? Batimayo asingeponywa kamwe.

Ishara ya kwanza kwamba Batimayo alikuwa na imani ni kwamba alimpazia Yesu sauti. Pili: Batimayo hakukubali kukatishwa tamaa na wale waliokuwa wanajaribu kumnyamazisha. Watu walipojaribu kumyamazisha, “alizidi kupiga kelele” (Marko 10:48). Hiyo inaonyesha imani yake. Tatu: Yesu hakuitikia kilio cha Batimayo mwanzoni. Inawezekana kwamba pengine alikuwa hasikii, lakini kama alisikia, Yesu hakuitika. Yaani, aliruhusu imani ya mtu huyo ipimwe. Kama Batimayo angekata tamaa baada ya kupiga kelele mara moja tu, asingeponywa.

Nini kifanyike katika uponyaji

Iwe makanisani, au po pote utakapokuwa kwa ajili ya kuombewa uponyaji, mtumishi wa Mungu atakufanyia uponyaji kwa kupitia njia mbili:
1. Uponyaji kupitia imani yako binafsi kwa Mungu:
Tukaze imani kwa sababu mara nyingi inaonekana ni kama kwamba maombi yetu hayatajibiwa. Hapo ni imani yetu inapimwa. Basi, tunahitaji kudumu kusimama, tukikataa kuvunjwa moyo kwa sababu zo zote zile. Kupitia njia hiyo, tunaimarisha nguvu na imani yetu kwa Mungu, hivyo maombi yetu kujibiwa.

2. Uponyaji kwa karama kupitia mtumishi wa Mungu, kama Roho Mtakatifu alivyopenda:
Kama una tatizo la kiuponyaji, FANYA UTAFITI ILI UJUE KANISA SAHIHI AMBALO LINA MTUMISHI WA MUNGU ALIYE NA KARAMA YA UPONYAJI.
Usizunguke kwenye makanisa mbalimbali na kujilaumu kuwa unaombewa lakini huponi. Hapo ni kwamba hujaenda kwa mtumishi wa Mungu mwenye karama ya uponyaji.
 
Unakaribishwa mhimbili ndugu mtumishi , nafikiri baada ya ujio wako vitanda vitabaki wazi kabisa, asante 🙏
 
Back
Top Bottom