Maboso
JF-Expert Member
- Feb 18, 2013
- 5,164
- 5,762
Wanajukwaa, kuna habari ambazo bado sijapata uthibitisho wake kwamba kuna ajali mbaya imetokea mteremko wa mlima wa Iringa mjini kwenda Ipogolo. Inasemekana basi la kutoka Mwanza, Lupondije Bus lilikuwa linakwenda kushusha abiria Ipogolo stand baada ya kuwashusha abiria wa stendi kuu mjini Iringa likapata ajali usiku huu maeneo ya kisima cha bibi. Nimepata uthibitisho wa kifo cha mtu mmoja kutoka kwa ndugu yangu ila inasemekana waliofariki ni wengi na pia kuna majeruhi wengi. Kama ilivyo ada, JF ni sehemu yenye mjumuiko wa watu kutoka sehemu mbalimbali, naomba waliopo eneo hilo watujunze zaidi.
Updates:
Updates:
WATU zaidi ya wanne wamekufa papo hapo na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa vibaya baada ya basi lenye namba za usajili T 798 AKV mali ya Lupondije Express Kutoka Mwanza kuja Iringa kupinduka eneo la Mteremko wa Ipogolo mjini Iringa wakati basi hilo likielekea kufaulisha abiria wa Mbeya.
Imeelezwa kuwa baadhi ya abiria waliokufa katika ajali hiyo na majeruhi ni wale ambao walitakiwa kushuka stendi kuu ya mabasi ya mabasi yaendaye mikoani mjini Iringa ila dereva wa basi aligoma kuwashusha stendi na kupitiliza nao kwenda Ipogolo kufaulisha abiria wa Mbeya kwanza ndipo arudi kuwashusha stendi.
Ajali hiyo imetokea majira ya saa 2 usiku baada ya basi hilo kufeli breki katika mteremko huo huo mkali kabla ya kupinduka .
Wema Zuberi ni mmoja kati ya majeruhi wa ajali hiyo aliyekuwa ametoka mkoani Dodoma kuelekea Mbeya alieleza kuwa mwendo wa basi hilo toka amepanda Dodoma kuja Iringa haukuwa mkali sana ulikuwa ni mwendo wa kawaida.
Japo alisema kuwa baada ya kuingia mjini Iringa katikati ya mji ndipo dereva wa basi hilo alionyesha kuendesha basi hilo kwa mwendo mkali zaidi kiasi cha baadhi ya abiria kulalamika mwendo huo na kutaka kushushwa ila dereva hakuweza kusikia zaidi ya kuwapuuza abiria hao.
“Abiria wengi walionyesha kumlalamikia dereva huyo kwanza kutokana na kuwapitiliza stendi pasipo kuwashusha na pili mwendo kasi ambao alikuwa akienda nao ili kufanikisha kutufaulisha abiria tuliokuwa tukielekea Mbeya “
Alisema kabla ya kufika eneo hilo ambalo basi lilipinduka kuna kona kali na mteremko mkali na kilichoonekana haraka haraka ni dereva kushindwa kukata kona hiyo baada ya Breki kufeli na hivyo kulazimika kuhama njia na kugonga kingo za barabara hiyo na kupinduka .
Mkuu wa wilaya ya Iringa Bw Richard Kasesela akizungumza na mwandishi wa habari hizi eneo la tukio alisema kuwa zoezi la kuendelea kutafuta miili iliyobanwa na basi hilo imekuwa ngumu kutokana na kukosekana kwa gari la kuinua basi hilo na tayari amemwagiza meneja wa Tanesco kuleta gari hilo na iwapo dereva hayupo basi kuamka na kuendesha mwenyewe .
Hata hivyo alisema kuwa kuanzia sasa dawa ya madereva hao ni kuwashughulikia kwani kama Rai imekwisha tolewa mara nyingi na bado ajali zinaendelea kutokea.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Bw Peter Kakamba ambae pia alikuwepo eneo la tukio kusaidia kuokoa majeruhi na kutoa maiti katika basi hilo pamoja na mkuu huyo wa wilaya wananchi mbali mbali walioongozwa na askari polisi ,alisema kuwa hadi majira ya saa 5 usiku wakati tunakwenda mitamboni bado ilikuwa ni mapema kuweza kujua ni watu wangapi wamepoteza maisha kwani zoezi lilikuwa bado linaendelea.
Kamanda huyo aliahidi kutoa taarifa mara tu zoezi hilo litakapokamilika kwa kuinua basi hilo na kutazama kwa kina kama kuna miili ambayo imefunikwa chini ama lah.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia miili minne ikiwa tayari imetolewa katika basi hilo huku majeruhi wengi wakiwa wamepata majeraha makubwa mikononi ,miguuni na kichwani,Majeruhi wa ajali hiyo wamelazwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa