Akili Mnemba ni teknolojia iliyosambaa ulimwenguni ikiwa imerahisisha kazi za binadamu kutokana na kwamba inaweza kufikiri kama binadamu. Lengo la AI ni kuweza kufanya mambo kama vile kutambua mifumo, kufanya maamuzi, na kuhukumu kama binadamu.
Akili mnemba (AI) ni seti ya teknolojia zinazoiwezesha kompyuta kutekeleza majukumu mbalimbali ya kina na kwa uwezo mkubwa kadri ya maelekezo ya mtumiaji, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kuona, kuelewa na kutafsiri lugha inayozungumzwa na maandishi, kuchanganua data, kutengeneza picha na video na kutoa mapendekezo ya utatuzi wa matatizo mbalimbali.
Akili mnemba ni muhimu katika shughuli za kila siku kwani husaidia kurahisisha utendaji kazi wenye ufanisi hata hivyo kama itatumika katika namna ovu inaweza kuleta madhara makubwa ikiwemo kutengeneza na kusambaza taarifa zisizo sahihi mfano picha, sauti, na video.
Pamoja na lengo zuri la teknolojia hii ya Akili Mnemba (AI), watu wasio wema wamekuwa wakiitumia katika kupotosha habari mbalimbali katika Jamii.
Baadhi ya nchi Ulaya zimechukua hatua ya dhati kukabiliana na matumizi ya akili mnemba ambapo zimeyataka makampuni yenye majukwaa makubwa ya kimtandao, kuziwekea alama maalumu video, sauti na maandishi vilivyotengenezwa kwa kutumia akili bandia ili watumiaji wavitambue.
Zinahofia kuwa teknolojia ya akili Mnemba inaweza kuwa ardhi yenye rutuba ya kukuza taarifa za kupotosha na habari za uongo kwa jamii na kuweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii, hasa siku hizi ambapo matumizi ya intaneti yanaongeza duniani.
Wote ni mashahidi katika vita mbili zinazoendelea kati ya Urusi na Ukraine, pia Hamas dhidi ya Israel kumekuwa na matumizi makubwa ya teknolojia ya akili mnemba ambapo vitu mbalimbali kama sauti, video na picha vimekuwa vikizalishwa kwa ajili ya nia ovu ya kupotosha na kubadili maana ya asili.
Mathalani, Oktoba 15, 2023, Mtumiaji wa Mtandao wa X anayefahamika kwa jina la Gasper E. Temba, PVR alichapisha ujumbe unaodokeza sehemu ya hotuba ya Rais wa Zambia Hakainde Hichilema akidokeza kuwa hatagombea tena kwa muhula wa pili kwenye uchaguzi wa mwaka 2026.
Video hii baada ya kusambaa ilileta sintofahamu nchini Zambia mpaka hapo ilipokuja kugundulika kuwa imepotoshwa kwa kutumia teknolojia ya Akili Mnemba.
Fikiria ni watu wangapi wanalishwa habari potofu, chuki, hila nk kutokana na matumizi mabaya ya teknolojia ya akili mnemba.
Ifike wakati tutambue kuwa kila tunachokutana nacho au kupewa kwenye mitandao tukipime kwanza uhalisia wake kabla ya kukitumia ili kupunguza kasi ya usambazaji wa habari potofu.