Pdidy
JF-Expert Member
- Nov 22, 2007
- 57,951
- 32,619
SHIRIKISHO la soka Tanzania mwezi uliopita lilitangaza zabuni ya uchapishaji tiketi za mechi za raundi ya kwanza ya Ligi Kuu, likitaka makampuni yenye uwezo kujitokeza katika muda wa siku nne tu.
Makampuni yaliyotaka kupewa kandarasi hiyo ya kuchapisha tiketi yalitakiwa kuwasilisha maombi yao kwenye ofisi za TFF kati ya Saa 2:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni Septemba 17 hiyo ikiwa ni siku ya mwisho.
Mechi nyingi za Ligi Kuu ya Tanzania ambazo zinachezwa nje ya Dar es Salaam zimekuwa zikitumia tiketi za mechi tofauti tofauti ambazo zimeishapita kwa sababu TFF haina kampuni linalochapisha tiketi au kupunguza gharama za mchezo.
Tunatarajia TFF itatangaza mapema kampuni ambalo limeshinda zabuni ya kutengeneza tiketi za raundi ya kwanza na kuhakikisha kampuni hilo linaanza kutengeneza tiketi hizo mapema zaidi.
Tunasema hivyo kwa sababu mwisho wa kuchezwa raundi ya kwanza ya Ligi Kuu ni Novemba 7, pia TFF ilitoa siku chache kwa wazabuni kujitokeza kuwania zabuni hiyo hivyo tulitarajia TFF pia itatumia muda mfupi ili kupata kampuni litakalotengeneza tiketi za Ligi Kuu.
Tunaamini upo umuhimu wa kupatikana tiketi halali katika kila mechi kwa ajili ya kufanya mahesabu vizuri kila mwisho wa mwaka ili kuweza kutoa ripoti nzuri ya mapato na matumizi.
Pia, tunaamini tiketi halali zikiwepo zitapunguza wizi wa mapato ya milangoni ambao ni tatizo kubwa kwa mapato ya TFF na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu.