12/24/2008
DED aliyesimamishwa Ilala aibukia Shinyanga
Zulfa Mfinanga
DED aliyesimamishwa Ilala aibukia Shinyanga
Zulfa Mfinanga
ALIYEKUWA mkurugenzi mtendaji wa manispaa ya Ilala, John Lubuva, ambaye alisimamishwa kazi kutokana na kuhusishwa na zoezi la bomoabomoa iliyofanyika Tabata Dampo jijini Dar es Salaam, amehamishiwa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Vijijini.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Amos Mshandete zinasema kuwa Lubuva ameanza kazi mwezi huu.
Mshandete, aliyesema kuwa hafahamu chochote kuhusu sababu za mabadiliko ya uongozi katika wilaya hiyo, alisema Lubuva amefika wilayani hapo kuchukua nafasi ya Pius Affa.
"Mimi, kama mwenyekiti wa halmashauri hii, ninachofahamu ni kwamba niliitwa na mkurugenzi aliyehamishwa Pius Affa akanieleza kuwa anahamishiwa mkoa Arusha na nafasi yake itachukuliwa na mkurugenzi kutoka Dar es Salaam ambaye ni John Lubuva," alisema Mshandete na kuongeza:
"Zaidi ya kumpokea sijui kingine chochote na maelezo mengine ya ziada yanaweza kutolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)."
Waziri wa TAMISEMI, Celina Kombani alilithibitishia gazeti hili jana kuwa Lubuva amehamishiwa Shinyanga kuendelea na wadhifa wake ule ule wa mkurugenzi Mtendaji.
Alisema pamoja na matatizo yaliyomkuta jijini Dar es Salaam alipokuwa mkurugenzi wa manispaa ya Ilala, Lubuva bado ana sifa za kuendelea na wadhifa wake kwa kuwa kosa hilo ni la kwanza.
"Taarifa za Lubuva kuhamishiwa Shinyanga ni za kweli tena ukweli mtupu yuko huko na bado ni mkurugenzi mtendaji. Tumefikia hatua hiyo baada ya kufuata taratibu zote za kazi za kumfukuza mtu baada ya kufanya makosa zaidi ya mara tatu," alisema Kombani na kuendelea:
"Kumfukuza mtu ni hatua ya mwisho baada ya kumpa karipio na karipio kali. Hili ni kosa la kwanza kwa John Lubuva hivyo amepewa karipio lakini pia amepewa kuiongoza Shinyanga kwa kuwa wilaya hiyo ni ndogo ikilinganishwa na Ilala."
Alisema uwepo wa Lubuva Shinyanga ni sehemu ya karipio na serikali inaamini kuwa mtendaji huyo atabalika na kuwa bora zaidi.
Februari mwaka huu Lubuva alisimamishwa kazi kutokana na kuhusishwa na ubomoaji haramu wa nyumba za wakazi wa Tabata Dampo akiwa mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Ilala
Kusimamishwa kwa Lubuva kulienda sambamba na serikali kutoa kifuta machozi cha Sh1.7 bilioni kwa wakazi hao ambao nyumba zao zaidi ya 88 zilibomolewa katiak zoezi hilo
Serikali ilikubali kuingia gharama hiyo kutokana na zembe na ukiukwaji wa taratibu na kanuni za notisi kuhusu ubomoaji nyumba unaohusishwa na ufisadi.
Fedha hizo zilitumika kulipa Sh20 milioni kila nyumba iliyobomolewa na kutoa kiwanja bure eneo Buyuni, Wilaya ya Ilala, kwa kila mkazi.
Akisoma Tamko la Serikali jijini Dar es Salaam jana kutokana na matokeo ya Tume Maalumu ya Kuchunguza Ubomoaji wa Nyumba hizo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Stephen Wassira alisema uamuzi huo wa serikali unatokana na kubaini kwamba ubomoaji huo haukuzingatia uamuzi wa Baraza la Ardhi.
Wassira alifafanua kwamba uamuzi wa Baraza la Ardhi ulitaka Halmashauri (Ilala) iangalie taratibu zilizopo katika kuwaondoa wavamizi katika eneo husika.
Wassira alitaja taratibu hizo ambazo zilipaswa kuzingatiwa kwamba ni kufikisha dhamira hiyo ya ubomoaji kwanza katika vikao vya juu vya timu ya menejimenti na vikao vya Baraza la Madiwani.
Wassira aliongeza kuwa taratibu nyingine zilizokiukwa ni wananchi kutoshirikishwa katika azma ya ubomoaji huo, kitu ambacho ni kinyume na misingi na kanuni za utawala bora huku kukiwa na harufu ya rushwa.
"Kulikuwepo kwa viashiria vya vitendo vya rushwa japo haikuweza kuthibitishwa," alisema.
Alisema taratibu zinataka notisi ya ubomoaji wa nyumba za makazi uwe siku 30, lakini katika ubomoaji wa Tabata notisi ilitolewa Febrari 27 na utekelezaji ukaanza Februari 29, yaani siku mbili baadaye.
Alisema uamuzi wa serikali kulipa fidia hiyo, haukuzingatia kama wakazi hao wanaishi kihalali au haramu bali umetokana na kubaini ukiukwaji wa taratibu ambazo zilitokana na maafisa wake kushindwa kuzisimamia.
Waziri Wassira aliweka bayana msimamo wa serikali kwamba, malipo hayo hayahusiani na nyumba ambazo hazijabomolewa kwani wakazi hao hadi sasa wamefungua kesi Mahakama Kuu kupinga kuondolewa katika eneo hilo.