TATIZO LA KLABU YA SIMBA SIO KICHUYA & MAVUGO KUKOSA KUFUNGA MAGOLI BALI NI HII HAPA
JUZI Yanga waliizidi Simba pointi moja tu na kuongoza Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Bao la pili la Obrey Chirwa lilikuwa zuri sana. Hata hivyo halijumlishi ukweli wowote kwamba Yanga wapo katika kipindi kizuri sana cha mchezo.
Yanga hii na ile ya msimu uliopita nadhani ile ya msimu uliopita ilikuwa nzuri zaidi. Mchezaji kama Thabani Kamusoko naona ameshuka kidogo.
Wanafunga kama kawaida na wamekuja kuongoza Ligi kwa sababu ina wachezaji wengi wanaoweza kubadili matokeo.
Simba hii ya msimu huu ni bora kuliko ile ya msimu uliopita iliyotoa sare sita mfululizo. Siamini moja kwa moja eti kwa Yanga kukaa pointi moja mbele ya Simba ina maana kwamba tayari Yanga ni mabingwa. Bado kuna mechi nyingi za kuchezwa.
Tatizo kubwa la Simba hii ni moja. Niliwahi kuandika siku za nyuma.
Simba hii ina mambo mengi. Ina watu wengi wajuaji. Ni tofauti kidogo na Yanga. Kule Yanga mwenye timu ni mmoja tu, Mwenyekiti wao. Huku Simba kila mmoja anajua kuliko Kocha Joseph Omog au anajua kuliko mwenzake.
Siku hizi Simba wanajipoteza wenyewe, Yanga wanajituliza wenyewe. Zamani Yanga walikuwa na tabia hii ya Simba. Yanga haikuwa timu ya kutulia baada ya kutoka sare na Ndanda, kisha ikafungwa na Stand United kisha kufungwa na Mbeya City. Zamani wangetukumbusha kwanini wanaitwa Gongowazi. Lakini walionekana kujituliza.
Simba ndio ambayo ina mambo mengi kiasi cha kujipoteza mwelekeo.
Msimu huu huu Simba imetaka mechi zao zichezeshwe na waamuzi wa kimataifa, hasa ile mechi yao ya marudiano na watani wa jadi Yanga.
Waamuzi wetu ni wabovu sawa, lakini sikuona mantiki ya Simba kufikia huko.
Msimu huu huu, Simba imeachana na kipa wake, Vincent Angban baada ya kufungwa mabao mawili safi na Victor Hangaya wa Prisons. Ilionekana kama Angban alikuwa mmoja kati ya makipa bora katika Ligi huku timu yake ikiongoza mpaka raundi ya kwanza.
Aliachwa kwa madai kwamba anahujumu timu.
Nilidhani sifa nyingi zilipaswa kwenda kwa Hangaya ambaye anaonekana kuwa hodari sana wa mipira ya hewani kumbe nilikosea. Mpira ulipoisha nikasikia analaumiwa kipa wa Simba.
Baadaye nikamsikia kiongozi mmoja mzito wa Simba akidai kwamba kuna wachezaji wanacheza chini ya kiwango na dawa yao ni kuwaletea wachezaji wapya tu, wazuri zaidi katika nafasi zao. Nikatikisa kichwa kwa mshangao sana.
Simba ilikuwa imetoka kushinda mechi nyingi hadi za Kanda ya Ziwa. Ilikuwa ni bahati mbaya tu kwao kukutana na kipigo cha Prisons. Badala ya kutulia na kujipanga, Simba kama kawaida yake katika miaka ya karibuni ikaanza kujiharibu.
Kuna hili jingine ambalo huwezi kulaumu sana. Huwezi kujua kama tatizo ni Simba au wachezaji wetu.
Wakati msimu ukiendelea Simba ilianza kuvurugana na wachezaji wake wawili mastaa, Jonas Mkude na Ibrahim Ajib. Ilionekana kama vile wanakacha mikataba yao mipya.
Mpaka sasa Ajib anaonekana hajarudi vizuri katika kikosi.
Majuzi katika mechi ya Azam nilimuona akijongea kuingia katika kipindi cha pili akionekana ni mchezaji ambaye hana morali. Hakuna alichoenda kubadili.
Hapo hapo kuliibuka na suala la mishahara ya wachezaji.
Hili hata Yanga liliibuka, lakini hakuna mchezaji aliyejitokeza kuliongelea zaidi ya Waandishi kutafuta umbea. Inasemekana Waandishi walipoenda kusaka Umbea kwa Simba Mkude akaongea. Akaichanganya klabu.
Karibuni tu hapa nilisikia tangazo ambalo sidhani kama ni rasmi kutoka katika klabu ya Simba kwamba watagomea mechi yao ya Majimaji kwa sababu TFF wameufungia Uwanja wa Jamhuri, Morogoro baada ya wao kucheza lakini hawajaufungia Uwanja mbovu wa Majimaji, Songea kwa sababu tayari Yanga imeshacheza mechi yao pale na kushinda.
Kila siku ukifungua redio au kusoma gazeti unasikia habari za mkwara, hujuma, tahadhari kutoka Simba.
Ukichunguza sana unakuta habari hizi zinawavuruga wenyewe. Zamani Simba hawakuwa na tabia hizi. Walijua kucheza na saikolojia.
Miaka michache iliyopita Kundi la Friends of Simba wakati likiwa limeshika sana hatamu pale Msimbazi walikuwa wananiacha hoi kwa kuwaachia wachezaji wao simu za mkononi siku moja kabla ya mechi dhidi ya Yanga. Wale Yanga walikuwa wanawapora wachezaji wao simu.
Mechi ikicheza Yanga anafungwa. Tabia hii na vitisho hivi vimehama.
Simba wanajivuruga wenyewe.
-Edo