Mbunge wa zamani wa Kiteto mkoani Manyara, Benedict Ole Nangoro na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kwenye Serikali ya awamu ya nne, amefariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru mkoani Arusha leo Desemba 7, 2025.
Msemaji wa familia, Christopher Ole Sendeka amesema Benedict Ole Nangoro alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo, ambapo aliwahi kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo mkoani Dodoma pamoja na nchi jirani ya Kenya.
Ole Sendeka ameeleza kuwa hivi sasa familia bado ipo kwenye majonzi ya msiba ila itapanga tarehe ya maziko na eneo ambalo marehemu atazikwa.
"Msiba umetokea leo Jumapili Desemba 7,2025 bado familia haijatamka lolote juu ya eneo ambalo maziko yatafanyika," amesema Ole Sendeka.
Mmoja kati ya wakazi wa kata ya Kibaya, Chief Mkomwa ametoa pole kwa wakazi wa eneo hilo kwa kuondokewa na kiongozi huyo.
"Nashauri azikwe Kiteto kwani alishawahi kupewa dhamana ya uongozi na watu wa Kiteto kuliko eneo lolote," amesema Mkomwa.