Je Talaka inaweza kutumwa kwa arafa ya simu ikafanyakazi?
Ndiyo inakubalika ktk uislam
TALAKA KATIKA UISLAMU.
Leo ndugu zangu ningependa tujifunze mambo mambo kadhaa kuhusu talaka, kwasababu talaka ipo na haikwepeki katika mfumo wa maisha yetu ya kila siku. tujifunze mada hii kwa njia ya maswali yafuatayo;
1.kuna aina ngapi za talaka katika uislamu?
2.Talaka tatu hutolewa wakati gani? na kwa kosa gani?
3.mume alie muacha mkewe kwa talaka tatu anaweza kumrejea?
4.ni mambo gani haramu kwa mume alie muacha mkewe kwa talaka tatu kutendewa au mtalaka wake?
5.neno talaka rejea lina maana gani katika uislamu?
6.nini haki za mke alie achwa toka katika mali za mume aliye mwacha?
Hayo ni baadhi ya maswali yahusuyo talaka ambayo kila mmoja anawajibu wa kufahamu majibu yake ili tuweze isaidia jamii yetu pindi inapo tokea suala la talaka.
1. Kwanza tukianza na swali la kwanza ni kwamba kwanza yatupasa kufahamu maana ya talaka kwa kuwa ndio msingi wa mada hii.
Talaka ni kufungua fungo la ndoa kwa tamko bayana au kwa kinaya (isiyo moja kwa moja ). na vigawanyo vya talaka ni kama vifuatavyo:
*talaka ya sunnah hii ni ile ambayo mume humuacha mkewe katika utwahara ambao hajawahi kukutana naye kimwili.
*Talaka ya bid'ah hii ni ile ambayo mume humuacha mkewe akiwa katika siku zake za ada, au katika kipindi cha damu ya uzazi au katika twahara aliomuingilia au kumuacha talaka tatu kwa mpigo mmoja. mwenye kutoa talaka ya aina hii huwa anapata madhambi lakini talaka yenyewe hua imepita ( imesihi/kukubalika) ila ile ya tatu huhesabiwa kuwa ni moja tu.
*talaka baain ni ile ambayo mume anamuacha mkewe akakosa haki ya kumrejea kwa kuwa eda imekwisha. hivyo, mume huyo akawa ni mposaji kama waposaji wengine na mke akikubali inabidi mume apose, atoe mahari na ifungwe ndoa upya.
*Talaka rejea ni ile ambayo mume anamiliki haki ya kumrejea mtalaka wake, huku ni mume kumrejea mkewe katika kipindi cha eda ya kuachwa talaka ya kwanza au ya pili.
baada ya ufafanuzi huo, tuje katika msingi wa swali lenyewe, ni kwamba zipo aina tofauti za kutoa talaka , nazo ni kama zifuatazo;
a) talaka ya bayana: hii ni talaka ilio wazi kabisa isiyo na utata wa aina yoyote, nayo ni kama kusema "nimekuacha " na tamko hili si lazima ukusudie kwani tamko lako linatosha.
b)talaka kinaya (isiyo ya bayana ) hii ni lazima ukusudie talaka kwa tamko lako si bayana , kama kusema " nenda kwa ndugu zako " au " usiseme na mimi " na yanayo fanana na hayo. ikiwa talaka imenuiwa basi itakuwa imetumika.
c)talaka ya hapo kwa hapo ni ile ambayo pindi inapo tolewa mke huachika papo hapo bila ya kuchelewa, hiyo ni kusema " wewe umeachika " baada ya mume kutamka hayo mkewe atakuwa ameachika.
d)talaka ya kutungika: ni ambayo mume ameitungika juu ya kitu kingine kuwa kitu hicho akikifanya au akikiacha atakua ameachika. mfano ni mume kusema " ukitoka hapa nyumbani bila ya ruhusa yangu utakua umeachika " na yanayo fanana na hayo.
e)talaka ya khiyari : hii ni mume kumwambia mkewe nimekupatia khiyari kutengana na mimi au kuachana na mimi. Akichagua kutengana talaka itakuwa imesihi/ imekubalika. ushahidi wa talaka hii upo katika Quran sura ya 33 ( surat ahzaab ) aya ya 28.
f)talaka kwa uwakala au maandishi: mume kama atamuwakilisha mtu mwingine kumuacha mkewe au akamuandikia mkewe talaka akimuarifu katika maandishi hayo kuwa amemuacha, mke atakuwa ameachika.
g)talaka kwa kuharamisha: hii ni kusema kwa mume kumwambia mkewe wewe ni haramu kwangu au unakuwa haramu, kama atakusudia kwa tamko hilo talaka, itakua talaka. Na kama atakusudia mzaha itakuwa mzaha lakini atawajibika mume huyo kwa tamko hilo kafara ya mzaha wake.
2. Ama kuhusu swali la pili ni kuwa hakuna wakati wowote ambapo mume anakubaliwa kisheria kutoa talaka tatu kwa mara moja au kikao kimoja. kufanya hivyo ni kosa na inahesabiwa kuwa ni talaka moja peke yake katika sheria ya kiislamu.
3. Ama katika swali la tatu ni kuwa ikiwa mume amemuacha mkewe talaka tatu mara moja, huhesabiwa ni moja tu. Ikiwa kwa hilo kwa hilo unamaanisha kumuacha mkeo kwa kumpatia talaka ya kwanza, kisha ya pili, mpaka ikafika ya tatu, basi haiwezekani kwa hao wawili kurudiana kama mume na mke mpaka kwanza mke aolewe na mume mwingine wakutane kimwili kisha aachwe. hapo ndio itawezekana kumrudia tena kwa kufuata utaratibu wote wa ndoa. ushahidi upo ktk qurani ( sura ya 2 : 230 ).
4. Ama kuhusu swali la nne ni kuwa haifai kwa watalaka kudhulumiana kwa njia moja au nyingine. pia haifai kwao kuweka chuki na uadui baina yao na kutoa siri walizo weka baina yao kwa wengine. kuoana ni kwa wema na ikitokea sababu ya kuachana basi tuachane kwa wema. pia haifai kwa mume kuchukua kutoka kwa mtalaka wake alivyo mpa kama hadiya kwa njia yoyote ile na vile vile si halali kwa mke kuchukuwa visivyo vyake kwa njia yoyote ile.
5.Ama kuhusu neno talaka rejea ni kama tulivyo lielezea hapo juu kuwa kuwa hii ni ile talaka ambayo mume anamiliki haki ya kumrejea mtalaka wake nako ni kumrejea mkewe katika kipindi cha eda ya kuachwa talaka ya kwanza au ya pili. ushahidi Quran ( sura 2 : 228).
6.Ama katika swali la mwisho ni kuwa pindi mke anapo achwa na mume anawajibu wa kumtazama kwa makazi, chakula, mavazi, matibabu, na yote anayo fanyiwa mke akiwa katika ndoa. Ama katika mali mke hatakuwa na haki yoyote isipokuwa kama walikuwa na ushirika katika hilo.
ikiwa hali ni hiyo kila mmoja atapata haki yake kama walivyo patana wao katika unyumba wao na ile kazi inavyo kwenda, mke atakuwa na yale mali aliyo patiwa na mtalaka wake wakiwa katika ndoa. haifai kwa mume kuchukua alivyompa kwa njia yoyote ile. ushahidi Qurani ( sura 2 : 229 ) na pia katika Qurani ( sura 4 : 20 ).
Hakika MOLA ANAJUA ZAIDI
Naamini tumejifunza machache katika mengi yahusuyo talaka.
Andiko kutoka kwa:
author: yurys law