Asante Kariakoo!

Asante Kariakoo!

Mzee Rufiji

JF-Expert Member
Joined
Aug 24, 2024
Posts
261
Reaction score
395
ASANTE SANA KARIAKOO!

NINGEKUWA kwenye jengo lililoporomoka. Sina matumaini ya kuokolewa. Nini ningefanya? Simu yangu ingekuwa na charge, network ipo sawa, ningeandika ujumbe gani kwa familia? Ningepost nini mtandaoni jamii isome?

Moyo mzito kuwafikiria waliowapoteza ndugu zao waliowapenda. Waliagana asubuhi kwa bashasha na matumaini ya msako wa riziki na manunuzi. Kumbe ni ile siku isiyobashiriwa.

Namfikiria mwenye jengo. Namfikiria Shetani. Bila tetemeko la ardhi wala kimbunga. Jengo limemwagika. Ujenzi chini ya kiwango? Ghorofa kwa bei chee? Walisema wahenga, tamaa mbele, mauti nyuma.

Nasoma ujumbe na kusikiliza sauti za waathirika waliokwama handakini. Najaribu kumwelewa Mungu. Shetani ametoa adhabu. Mungu anatoa fundisho.

Nawatazama vijana shupavu waliojitoa kuokoa wenzao waliokwama. Nauona Utanzania. Saa 40 na mshale unaendelea, haijawezekana kuwafikia waliokwama handakini. Unadhihirika udhaifu wetu.

Utajiri wa mbwembwe. Ufahari na maonesha kusaka mitaji ya kisiasa. Mipango ya bajeti ya kila mwaka. Kariakoo imethibitisha kama nchi hatujawahi kuwa tayari kukabiliana na ajali.

Soma Pia: Live Updates Kuporomoka kwa Ghorofa Kariakoo Nov 16: Watu 7 wengine waokolewa

Nazungumza na nafsi yangu. Mimi kama baba, naweza kusafiri nikaacha wanangu wanaangamia ajalini? Niseme safari ilishapangwa, kwa hiyo siwezi kuahirisha. Nitoe maagizo kwa wadogo zangu: “Walioumia watibiwe, waliopoteza maisha wazikwe.”

Ni baba gani mimi? Nisafiri kutafuta fedha kwa ajili ya watoto ninaowaacha wanakufa? Ni swali kwangu, ningekuwa Rais wa Tanzania, ningeridhika kwenda Brazil kwenye mkutano wa G20, nikiwaacha Watanzania wakipoteza maisha Kariakoo?

Lengo namba moja la urais wangu ni nini? Bila shaka maisha ya Watanzania ndiyo kipaumbele. Kama ndivyo, nawezaje kukwea ndege nikiacha Watanzania wameangukiwa na ghorofa Kariakoo, makumi kwa makumi wakiwa hawajui hatima yao?

Rais kama mfariji mkuu wa nchi. Tangazo likitoka kuwa nimeahirisha ziara nje ya nchi kwa sababu ya ghorofa kuanguka Kariakoo, ili nibaki nikihakikisha nahimiza uokoaji na kupokea ripoti za mara kwa mara, tena hatua kwa hatua, ni kiasi gani nyoyo za wananchi zitafarijika?

Tuwatakie safari jema ndugu waliokatishwa uhai wao. Tuwaombee afua waliojeruhiwa. Tuwaweke kwenye maombi waliopoteza mali. Kariakoo kitovu cha uchumi, ndiyo kitovu cha ujenzi holela. Mamlaka husubiri maafa kuchukua hatua. Asante sana Kariakoo.

©Luqman MALOTO
 
Nchi haina vifaa vya uokozi, angekuwepo mama yenu bado isingesaidia kitu, haokoi yeye ni vifaa na nguvu kazi.

Bajeti itengwe, we unadhani wangekuwa na roboti pale, linaingia lina camera, mtu anaeliendesha anaona kinachojiri ndani, kisha. Liwe na features tofauti tofauti, mfano linaweza kudrill, linaweza kucalculate kwa hapa waliponasa ikifanyika hivi wanatoka, kwa hapa njia rahisi ni hii.

Tuwekeze kwenye teknolojia.
 
Nakunukuu,
"Utajiri wa mbwembwe. Ufahari na maonesha kusaka mitaji ya kisiasa. Mipango ya bajeti ya kila mwaka. Kariakoo imethibitisha kama nchi hatujawahi kuwa tayari kukabiliana na ajali"

Aisee
 
Nchi haina vifaa vya uokozi, angekuwepo mama yenu bado isingesaidia kitu, haokoi yeye ni vifaa na nguvu kazi.

Bajeti itengwe, we unadhani wangekuwa na roboti pale, linaingia lina camera, mtu anaeliendesha anaona kinachojiri ndani, kisha. Liwe na features tofauti tofauti, mfano linaweza kudrill, linaweza kucalculate kwa hapa waliponasa ikifanyika hivi wanatoka, kwa hapa njia rahisi ni hii.

Tuwekeze kwenye teknolojia.
Umeeleza vyema kabisaa,Kama hayo ma robot yapo yanunuliwe,

NB.
Lisiwe Kama lile robot la nape bungeni

So painful 😣
 
Back
Top Bottom