Aspirin inaweza kusababisha damu kuvuja tumboni

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363


Wiki iliyopita nilizungumzia kuhusu Paracetamol, ambayo ni maarufu kwa jina la Panadol, tuliona kwamba dawa hiyo inapotumiwa kiholela, inaweza kusababisha madhara kwa viungo vya mwili kama vile ini, figo na ubongo.

Leo katika mfululizo huu wa kuzungumzia madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya dawa za maumivu, nitazungumzia Asprin.
Siyo watu wengi wanapendelea kutumia Aspirin kwa ajili ya kutuliza maumivu kama ilivyo kwa Panadol na Diclopar au diclofenac.

Pamoja na mazingira hayo, kuna wanaoitumia bila kujua, kupitia dawa nyingine zilizochanganywa na paracetamol pamoja na caffeine.
Dawa hizo ni kama vile Headex, Mifupen, Action ama dakika tatu. Zote hizo ni mchanganyiko wa dawa kadhaa, asprini ikiwa ni miongoni.

Dawa hizi kwa sasa zinapatikana hadi kwenye maduka ya vyakula na hazina udhibiti wowote kwani hata machinga anaweza kuzijumuisha kwenye bidhaa anazouza.
Kama nilivyoeleza awali, matumizi holela ya dawa hizi za kutuliza maumivu yamekithiri, hivyo baadhi hutembea nazo mifukoni au kwenye pochi.

Watu wa namna hii huwa hawatibu chanzo cha matatizo yao, bali wanatumia dawa hizo ili kujipa ahueni ya maumivu ambayo ni dalili tu ya yale yanayowasumbua.
Leo katika kuzungumzia Aspirin nimezungumza na Mtaalamu wa Dawa nchini, Mfamasia Mildred Kinyawa.

Kinyawa ambaye ni Msajili wa Baraza la Wafamasia Tanzania anaanza kwa kueleza:
Kwa jumla, kitu chochote kikishaitwa dawa ni muhimu kutumiwa kwa uangalifu. Hakuna dawa isiyo na kiwango fulani cha madhara kwa mtumiaji. Pia hiyo ni mbaya zaidi kwa wale wanaotumia kiholela.

Anasema kuwa kitaalamu Aspirin ni dawa nzuri kuliko dawa nyingine za kutuliza maumivu kwa sababu huweza kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.
Anabainisha kuwa kama ilivyo paracetamol, Aspirin inaweza kutuliza maumivu madogomadogo kama vile kuumwa kichwa, mafua na kushusha homa.

Kinyawa anafafanua kwamba, tofauti na Paracetamol, Aspirin inaweza kutuliza maumivu makali kama vile ya mifupa, meno na hata kutibu uvimbe.
Faida nyingine za Aspirin ni kwamba huweza kumsaidia mtu asipate matatizo ya moyo au kiharusi kutokana na damu kuganda na kuziba mishipa ya damu.

Anaeleza kuwa Aspirin huweza kuyeyusha vipande vidogovidogo vya damu iliyoganda na kujikuta ikiendelea kusafirishwa kwenye mfumo wa damu.
Kinyawa anaielezea damu iliyoiganda kuwa inaweza kuziba mirija kwenye moyo au ubongo na kusababisha madhara makubwa ikiwamo kifo cha ghafla.

Athari za Aspirin

Mfamasia huyo anasema kwamba kwa namna ilivyotengenezwa, Asprin ina asili ya aside, hivyo inapotumiwa wakati tumbo likiwa wazi hukwangua tumbo na kumsababishia vidonda tumboni.

Kwa watu wenye matatizo ya vidonda vya tumbo, hushauriwa kutokutumia kabisa asprini kwa sababu huchangia kuongeza tatizo.
Tafiti nyingine ambazo zimewahi kufanywa na kuandikwa kwenye majarida mbalimbali ya afya duniani zinaonyesha kuwa mtu akitumia aspirin na pombe anaweza kusababisha damu kuvuja tumboni kiasi cha kuhatarisha maisha yake.

Utafiti uliofanywa mwaka 2009, ulibaini kwamba matumizi mabaya ya Aspirin kutibu mafua makali kwenye kipindi cha mwaka 1918-19 ilisababisha athari mbalimbali zikiwamo za mapafu kujaa maji, vifo na udhaifu wa mwili kushambuliwa na bakteria pamoja na virusi.
Utafiti huo ulisababisha matumizi ya Aspirin kupungua na hata kupendekezwa isitumike kwa watoto chini ya miaka 16.


Inafanyaje kazi?
Aspirin inafanya kazi kwa kupunguza uzalishaji wa kemikali inayojulikana kama prostaglandin ambayo kwa kawaida husababisha maumivu.

Mara nyingi Aspirin inapendekezwa kutumiwa na watu wazima na mtumiaji awe ameshakula au kutumia wakati anakula.
Wiki ijayo nitamalizia mada hii kwa kuelezea juu ya Diclopar na Diclofenac.


HAYA NDIO MATUMIZI SAHIHI YA DAWA YA ASPRIN


Aspirin ni dawa inayotumika kutuliza maumivu na uvimbe(inflammation) katika mwili.

Dawa hii pia hutumika kutuliza homa pamoja na kuzuia matatizo ya moyo(atherosclerotic plaque), saratani ya utumbo mpanana(colorectal cancer), kiharusi endapo daktari ataona ni vema.

Aspirin hutumika kutuliza maumivu ya kichwa, mgongo,meno, misuli na mengine yanayofanana na hayo. madhara(side effects) za aspirin zinatofautiana kulingana na umri, hali ya kiafya pamoja na kiasi cha dawa kilichotumika.

1. WATOTO

Aspirini haishauriwi kutumika na watoto wadogo kwani zinaweza kusababisha ugonjwa uitwao Reyes syndrome.

Ugojwa huu mara nyingi huwapata watoto wenye umri chini ya miaka 12 ambao wanatumia aspirin mara kwa mara. Imegundulika kwamba watoto wenye magonjwa kama tetekuwanga wana hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa huu baada ya kutumia aspirin.


Ugonjwa huu hushambulia ini na ubongo
na unaweza kusababisha kifo kama mtoto hatapata matibabu haraka.

Dalili za Reyes syndrome ni pamoja na:


  • Kutapika mara kwa mara
  • Mabadiliko ya tabia
  • Kuzubaa
  • Kupumua haraka haraka(hyperventilation)
Dalili hizi hutokea baada tu ya kupona ugonjwa wa mafua au tetekuwanga.
Uwepo wa ugonjwa huu unaweza kugundulika kwa kupimwa damu au mkojo na matibabu ya haraka yanahitajika ili kuzuia madhara makubwa zaidi kwenye ubongo pamoja na ini ambayo yanaweza kusababisha kifo.

2. VIDONDA VYA TUMBO (ulcers)
Inashauriwa watu wenye vidonda vya tumbo wasitumie Aspirin kwani inaweza kuongeza tatizo hilo na hata kusababisha uvujaji wa damu tumboni.


Dawa mbadala kama vile paracetamol inaweza ikatumika kutuliza maumivu badala ya aspirin kwa mtu mwenye vidonda vya tumbokwa kuwa aspirin ina asili ya tindikali(acidic).

3. KIUNGULIA (heart burn)
Kwa kuwa aspirin huongeza kiasi cha tindikali tumboni, kiasi kidogo cha tindikali hiyo hurudi kwenye koo la chakula na kusababisha mtu apate kiungulia.

4. KUVUJA DAMU KWENYE UBONGO(Cerebral hemorrhage)
Moja wapo kati ya kazi za aspirin ni kuzuia damu kuganda(anti-clotting) na hivyo huweza kusababisha kuvuja kwa damu kwenye ubongo.


  • Watu wanaotarajia kufanyiwa upasuaji wanashauriwa wasitumie aspirin kwa kuwa inaweza ikasababisha wavuje damu nyingi wakati wa upasuaji.

5. ALEJI (allergy)
Baadhi ya watu hupata madhara baada ya kutumia aspirin.

Baadhi ya dalili za kuwa na aleji ya aspirin hutokea lisaa limoja baada ya kumeza kidonge cha aspirin nazo ni ni pamoja na:


  • Kuwashwa kwa ngozi pamoja na kutokwa na vipele(skin rashes)
  • Kushindwa kupumua vizuri(pumu/asthma)

6. KUTUMIA KIASI KIKUBWA CHA ASPIRIN (
aspirin poisoning/salycilism)
Kama zilivyo dawa zingine, matumizi makubwa ya dawa hii huifanya iwe sumu mwilini(intoxication).

Sumu zilizoko mwilini huchujwa kwenye ini ila, ini huzidiwa kama kiasi cha sumu kikizidi. Matumizi ya aspirin kwa muda mrefu pia huweza kusababisha magonjwa ya ini pamoja na figo.

Dalili zake hutegemea na kiasi pamoja na muda wa matumizi,

Madhara yatokanayo na matumizi ya kiasi kikubwa cha aspirin kwa muda mfupi(Acute aspirin poisoning)


  • Maumivu makali ya tumbo
  • Kichefuchefu na kutapika
Madhara yatokanayo na matumizi ya kiasi kidogo cha aspirin kwa muda mrefu(Chronic aspirin poisoning)


  • Uchovu
  • Kutetemeka(seisures)
  • Moyo kwenda mbio
  • Kupumua kwa kasi(hyperventilation)

MUINGILIANO NA DAWA NYINGINE


  • Kwa wanaotumia dawa za kisukari, aspirin inaweza ikasababisha sukari kushuka kupita kiasi (hypoglycemia)
  • Kwa wanaotumia aspirin ili kuzuia matatizo ya moyo au kiharusi, hawatakiwi wachanganye pamoja na dawa zingine za maumivu kama ibuprofen
  • Madhara ya aspirin huongezeka pale inaponywewa pamoja na pombe, kwani husababisha damu kuvuja kwa wingi tumboni kwa watu wenye vidonda vya tumbo

MATUMIZI SALAMA YA ASPIRIN


  • Ili kupunguza hatari ya kupata vidonda vya tumbo, usitafune aspirin, meza kama ilivyo.
  • Meza aspirin kwa angalau glass moja ya maji
  • Usivunje wala kusaga kidonge cha aspirin kabla ya kumeza
  • Hakikisha unamtaarifu daktari wako kama unatumia aspirin kabla ya upasuaji/operesheni(surgery)
  • Watoto wa chini ya miaka 12 wasitumia aspirin pasipo ushauri wa daktari
  • Usitumie vidonge vya aspirin vyenye harufu ya siki(vinegar) kwani vinaashiria kuwa vimeisha muda wake

SOURCES






 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…