Pre GE2025 Asya Mohamed: Ukosefu wa fedha ni moja ya changamoto kubwa kwa Wanawake wanaowania Uongozi

Pre GE2025 Asya Mohamed: Ukosefu wa fedha ni moja ya changamoto kubwa kwa Wanawake wanaowania Uongozi

Mijadala ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 (Kabla, wakati na baada)
Joined
Sep 23, 2024
Posts
64
Reaction score
43
Safari ya uongozi kwa Wanawake kamwe haijawahi kuwa nyepesi, Mwanamke anapita katika njia mbovu, milima na mabonde pia kona hatarishi. Licha ya ugumu huo, wengi wanapambana na mengi hadi kufanikiwa katika malengo ya ndoto zao.

Simulizi ya kuvutia ya Asya Mohamed, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja, inatuonesha Wanawake wanaweza kufanikiwa na kufanya vizuri katika uongozi.
Screenshot 2025-01-15 122547.png

Asya Mohamed, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja
Amekuwa Mbunge wa Viti Maalum katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha Mwaka 2020 – 2025, anasema wagombea Wanawake wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya ukosefu wa fedha za kujiendesha wakati wa uchaguzi na kampeni.

Asya Mohamed Muhidin, alingia katika siasa Mwaka 2008 na kuanza kugombea Uenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema – BAVICHA Mwaka 2010 hadi 2015 na kushinda nafasi hiyo.

Anasema “Mimi binafsi changamoto ya uhaba wa rasilimali fedha, ilinikuta na kunifanya nikakosa Ubunge Mwaka 2020 wakati nagombea Jimbo la Chumbuni Unguja.”

Anaeleza kuwa ushiriki wa Wanawake katika uongozi ni hatua muhimu sana kuelekea usawa katika Uongozi na maendeleo ya kijamii, hata hivyo uwakilishi wa Wanawake katika nafasi za uongozi bado ni mdogo na unakwamishwa na changamoto mbalimbali kufikia usawa huo.

“Bado Wanawake hawajatosha katika nafasi za uongozi, kutokana na sababu nyingi lakini pia kukosa msaada wa mtaji wa kufanya kampeni wakati wa uchaguzi,” anasema Asya.

Hadi sasa ni nchi 26 pekee zinaongozwa na Wanawake kama Wakuu wa Nchi au Serikali Duniani kote na nchi 119 hazijawahi kupata fursa hiyo, jambo ambalo lina athari kubwa kwa matakwa ya Wasichana wanaokuwa katika mwenendo wa sasa.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na maswala ya Wanawake (UN Women), imesema licha ya baadhi ya Maendeleo yaliyopo Wanawake bado kwa kiasi kikubwa wametengwa katika utawala na Diplomasia.

Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, Bi Sima Bacchus amesema uwakilishi wa Wanawake katika uongozi bado hautoshi, ulimwenguni kote na sasa ni wakati wa kukamilisha malengo ya mkutano wa Beijing kuhusu haki za wanawake katika kila Nyanja.

Amesema wakati Dunia inajiandaa kuadhimisha Miaka 30 tangu kupitishwa kwa Azimio la Beijing na jukwaa la Utekelezaji hati yenye maendeleo zaidi Duniani ya kuendeleza Haki za Wanawake UN Women, inaendelea kufanya kazi ili kuhakikisha Wanawake wanachukua nafasi kubwa katika kuchagiza na kuleta mabadiliko chanya ikiwa ni pamoja na kushika nafasi za juu za Madaraka.

Katibu wa Ngome ya Chama cha ACT Wazalendo, Fatma Abdul-Habib Ferej ambae aliwahi kugombea nafasi za uongozi wa kisiasa Visiwani Zanzibar, naye amekiri kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa mitaji ya kuendesha Siasa kwa wagombea Wanawake ukilinganisha na Wanaume.

“Kama tunavyojua Uchumi wa Wanawake ulivyokuwa ni mdogo ukilinganisha na wenzao upande wa pili Wanaume, hivyo ni shida kukabiliana na vitu hivyo kama huna mtaji,” anasema Fereji huku akizitaka taasisi mbalimbali na mashirika kujitokeza ili kuwashika mkono wanawake ambayo hawana mtaji kipindi cha kampeni kwa lengo la kuongeza usawa wa kijinsia.

Anaongeza ili kuongeza ushiriki wa Wanawake katika nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi ni lazima kuwasaidia kwa kila hatua.

“Tunachokihitaji kwa sasa ni uongozi wa Wanawake na kuongeza uwakilishi wetu,katika Nyanja zote ambako maamuzi yanafanywa wakati huu na wanaume, katika masuala yanayoathiri wanawake na Maisha yetu,” anasema kuwa janga la kukosa uwakilishi wa Wanawake linaendelea Duniani kote kwa muda mrefu sana.

Anaongeza kuwa licha ya Tanzania na Zanzibar kuridhia mikataba na matamko mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa, yenye wito wa usawa katika uwakilishi na ushiriki wa Wanawake na Wanaume katika siasa, bado Wanawake wana uwakilishi mdogo katika vyombo vya maamuzi na nafasi za uongozi, baadhi ya sababu zinazochangia hali hii ni ukosefu wa rasilimali fedha kwa wale wanaotia nia ya kugombea nafasi za uongozi.

Kwa mujibu wa ripoti Maalumu ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 iliyotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar -TAMWA ZNZ inaeleza nafasi ya uwakilishi kwenye majimbo 50 ya Zanzibar, Wanawake ni 16% ambao ni nane.

Wabunge Wanawake wanaoiwakilisha Zanzibar ni wanne sawa na 8%, Mawaziri wakiwa ni sita sawa na 33% na Makatibu wakuu ni saba sawa na 39%.

Tunu Juma Kondo, ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania - UWT wa Chama cha Mapinduzi – CCM amekiri ni kweli Wanawake wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha, wakati wa kampeni jambo ambalo linawarudisha nyuma wengi kuingia katika kinjany’anyiro cha kugombea nafasi za uongozi.

Mchambuzi wa Masuala ya uongozi na Siasa Visiwani Zanzibar, Almasi Mohamed amesema ni kweli wagombea Wanawake wanakabiliwa na ukosefu wa rasilimali fedha, jambo ambalo linawarudisha nyuma wakati wa kugombea nafasi za uongozi.

Amesema kuwa,ni vyema kwa vyama vya siasa kuwasaidia wanawake wanaotia nia ya kugombea, ili kuongeza wingi wao jambo ambalo linapelekea maendeleo ya kijamii na taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Siti Ali Abass amesema hakuna fungu maalumu linalotolewa kwa ajili ya kuwawezesha Wanawake wanaotia nia ya kugombea, isipokuwa wizara hiyo inatoa mikopo kwa ajili ya wajasiriamali ili kujiajiri na kujiwekea akiba kwa maswala mengine baadae.

“Tunashauri Wanawake wachukuwe mikopo kwa ajili ya shughuli zao za kijasiriamali ili kujiajiri lakini pia kujiwekea akiba ili wakitaka kushiriki katika nafasi za uongozi iwe rahisi kwao,” ameshauri Mkurugenzi Siti.

ANDIKO LA: Maryam Nassor
 
Back
Top Bottom