Kwa wale wenye kumbukumbu, niliandika hapa JF kuwa kadri maamuzi ya kuinusuru ATCL yanavyochelewa, siku inayofuatia itaendelea kuwa ngumu kwa ATCL kuliko ile ya leo na hasara kwa ATCL itaongezeka kila siku zinavyozidi kuongezeka.
Matatizo yanayoikabili ATCL mimi na wachangiaji wengine tumejaribu kuyaeleza na hata kufikia kutoa mapendekezo ya nini kifanyike.
Vilevile nilijaribu kueleza kiini cha matatizo yanayoikabili ATCL kwa kuaninisha chanzo chake ambacho ni management team ambayo haikidhi matakwa hali ya uendeshaji wa shughuli za anga kwa kipindi hiki ambacho ATCL inatakiwa ikarabatiwe.
Hali ilivyo ya biashara ya usafiri wa anga sasa hivi ulimwenguni imegubikwa na matatizo mengi ikiwemo ongezo kubwa la bei ya mafuta, bima, vipuri nk. Unahitajika utaalam usio na shaka wa kuweza kuliendesha shirika liweze kubuni njia za kweli na zenye uhakika wa kulipatia shirika mapato ya kuweza kukabiliana na changamoto zilizogubika biashara hiyo.
Bado nitaendelea kusisitiza hatua za haraka zichukuliwe kuinusuru ATCL kwa kukodisha timu ya wataalam wa menejimenti ya uendeshaji wa mashirika ya ndege Aviation Management Experts. Hatua hii itasaidia kukarabati ATCL na vilevile kupasha utaalam wa kimenejimenti ulioko katika Aviation Industry ya leo.
Ninasikitika sana kuona ATCL inavyoendelea kukumbwa na matatizo kila kukicha na kupoteza mamilioni ya pesa bila kuonyesha kupatikana suluhu ya kudumu. Kwa mimi ambaye ninaishi nje ya Tanzania na ambaye tayari nilishafanya kazi kwenye Aviation Industry ya Tanzania kwa takriban miaka 20, ninafedheheka sana kuona hali ya ATCL ikiendelea kuporomoka.