BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,591
- 8,826
MKAZI wa Mtaa wa Nyakabungo, Nyamagana mkoani Mwanza, Peter Domini, ameuawa kwa kushambuliwa na kupigwa na kitu chenye ncha kali wakati alipokwenda kwa jirani yake kudai Sh. 6,500.
MKAZI wa Mtaa wa Nyakabungo, Nyamagana mkoani Mwanza, Peter Domini, ameuawa kwa kushambuliwa na kupigwa na kitu chenye ncha kali wakati alipokwenda kwa jirani yake kudai Sh. 6,500.
Imeelezwa kuwa Domini alikwenda nyumbani kwa jirani yake, Julius Gaini, kufuatilia deni lake juzi majira ya saa 2:00 usiku. Baada ya kufika, aliwakuta watu watatu na kuzuka ugomvi uliowafanya watu hao kuanza kumshambulia na kusababisha kifo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Wilbroad Mutafungwa, jana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Mutafungwa alisema baada ya taarifa hizo kufika katika Jeshi la Polisi, waliwakamata watu watatu ambao ni Julias Gaini (59),Judith John (48) na Rhoda Julius (49) wote wakazi wa Mtaa wa Nyakabungo kwa tuhuma za mauaji hayo.
“Upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea na utakapokamilika, watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka dhidi yao. Kadhalika, niwatake watu kuacha kujichukulia sheria mkononi maana jeshi letu limejipanga kudhibiti vitendo vyote vya uhalifu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mutafungwa alisema jeshi hilo linawashikilia waganga wa kienyeji 34 kwa tuhuma za kujihusisha na ramli chonganishi wakati wakitoa huduma za uganga kwa wateja wao hali ambayo imekuwa ikisababisha migogoro na mauaji katika jamii mkoani hapa.
Alisema waganga hao walikamatwa kwa nyakati tofauti katika wilaya za Misungwi, Ilemela, Nyamagana, Kwimba, Sengerema na Magu huku wakikutwa na vielelezo mbalimbali zikiwamo nyara za serikali.
"Tumewakamata kutokana na oparesheni iliyoanza Mei 17 hadi 24, mwaka huu, wakifanya shughuli ya uganga bila kusajiliwa huku wakitumia nyara za serikali bila kibali. Hawa watu hawafuati sheria na ndiyo chanzo cha matukio mbalimbali yasiyofaa pamoja na mauaji ya mara kwa mara," alisema Mutafungwa.
Aidha, Kamanda Mutafungwa alisema oparesheni hiyo ni endelevu huku akiwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuwafichua waganga ambao wanaleta visa vya uchonganishi ndani ya jamii kupitia ramli chonganishi na kwamba watu waliokamatwa watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
NIPASHE