Polisi nchini Kenya wamerusha mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa muungano wa upinzani National Super Alliance ambao wamekuwa wakiandamana mjini Kisumu, magharibi mwa nchi hiyo.
Maandamano pia yamefanyika katika miji mingine mikuu ingawa hali imekuwa tulivu.
Muungano wa Nasa umekuwa ukifanya maandamano kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kushinikiza mageuzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mpya.
Uchaguzi ambao umepangiwa kufanyika tarehe 26 Oktoba umeingiwa na utata baada ya mgombea wa Nasa Raila Odinga kutangaza kujiondoa rasmi Jumanne.