The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Wakongwe Tyson na Evander wakiwa sasa ni marafiki.
Mike Tyson na Evander Holyfield wana historia ndefu na zitakazodumu kwa karne nyingi sana kwenye historia ya mchezo wa ndondi, na kama Evander anavyotaka, labda siku moja Mungu akipenda, kuna uwezekano wa nyongeza ya ukurasa katika kitabu cha historia yao.
Tyson na Holyfield tayari wamewahi kupigana mara mbili. Wawili hao walikutana baada ya Mike Tyson kumaliza kifungo chake gerezani, katika pambano la ubingwa lililopewa jina la Finally. Wakati huo, Evander alikuwa amestaafu, lakini alirejea akiwa hana nafasi kubwa ya kushinda pambano hilo.
Walikutana Novemba 9, 1996, ambapo Evander alifanikiwa kuwa bondia wa pili kumuangusha Mike Tyson kwa knockout, baada ya mwamuzi kusimamisha pambano hilo katika raundi ya 11.
Tyson akichezea kichapo cha Evander, Novemba 9, 1996.
Mike Tyson na Evander Holyfield walikutana tena miezi michache baadaye, Juni 28, 1997.
Katika pambano lililopewa jina The Sound and the Fury, lililofanyika katika ukumbi uleule wa MGM Grand Garden Arena kama pambano la kwanza, wawili hao waliweka historia kwa kupata malipo makubwa zaidi katika ndondi kwa wakati huo.
Hata hivyo, pambano hilo liliisha katika hali ya utata, baada ya Mike Tyson kumng'ata Evander sikio wakati wa pambano. Mwamuzi Mills Lane alisimamisha pambano hilo, na Evander alishinda kwa kutangazwa mshindi kwa sababu ya kitendo cha Tyson. Hii ilikuwa mara ya kwanza katika zaidi ya miaka 50 kwa pambano la ndondi kuisha kwa namna hiyo.
Tyson alipogeuza sikio la Evander kuwa kitoweo, Juni 28, 1997.
Baada ya pambano, ghasia zililipuka miongoni mwa watazamaji, na kusababisha majeruhi kadhaa. Tyson baadaye aliomba msamaha, na leseni yake ya ndondi nchini Marekani ilifutwa kwa muda na NSAC (Nevada State Athletic Commission) – yaani, tume ya serikali ya jimbo la Nevada inayosimamia na kudhibiti michezo ya mapigano kama vile ndondi, MMA, na michezo mingine ya mapigano katika jimbo hilo.
Ombi la Evander baada ya mechi ya Tyson na Jake Paul
Sasa, huenda baada ya kuona jinsi pambano la Tyson dhidi ya Jake Paul lilivyovutia fedha nyingi na mwamko mkubwa wa mashabiki, Bwana Evander anataka tena kumpa Mike nafasi ya kulipiza kisasi. Holyfield amechapisha picha ya wawili hao wakiwa kwenye kilele cha mafanikio yao kwenye Instagram yenye maandishi “The Trilogy,” huku chini yake akiandika “Mashabiki wanalitaka”, akiambatanisha pamoja na video ya Tyson baada ya pambano na Paul akisema bado hakuwa tayari kustaafu.
Posti aliyoweka Evander kwenye ikurasa wake
Video ya Tyson akisema bado hajamalizana na masumbwi. Ni baada tu ya pambano lake na Jake Paul.
Video ya Tyson akisema bado hajamalizana na masumbwi. Ni baada tu ya pambano lake na Jake Paul.
Hata hivyo, jibu la Tyson kwenye posti hiyo ni kuwa hayupo tayari kushiriki kwenye pambano analolitaka, na amejibu kwa heshima tu kuwa: “I love you brother, but the triology is our friendship” - yaani akimaanisha kuwa, "Nakupenda kaka, lakini urafiki wetu ndiyo ‘pambano letu la tatu’ "
Mashabiki wanasemaje?
Baadhi ya mashabiki walipinga wazo hilo. “Tunakupenda, kwa hiyo hatutaki kuona hilo,” aliandika shabiki mmoja. “Atang’ata sikio lingine tena,” aliandika shabiki mwingine, akirejelea tukio maarufu ambapo Tyson aling’ata na kung’oa sehemu ya sikio la Holyfield. “Hapana, msiifanye hiyo. Fanyeni podcast pamoja,” shabiki mwingine alitoa maoni yake.
Hata hivyo, mashabiki wengine walipenda wazo hilo. “Kusema kweli, hili lingekuwa pambano la kusisimua sana na linaweza kufanya jambo maalum kwa mchezo huu! Kurudisha kila kitu kilichofanya ndondi kuwa bora na kuikumbusha dunia kwa nini ndondi ni mchezo bora zaidi duniani!” aliandika mtu mmoja kwenye maoni ya Holyfield. “Evander dhidi ya Tyson III, lifanyeni litokee!”
Lakini shabiki mwingine aliandika kwamba wangependa zaidi kumwona Holyfield akipigana na Jake Paul, “Evander dhidi ya Jake… tunalihitaji,” aliandika shabiki huyo. Hata hivyo, shabiki mwingine alitoa maoni, “Kwa kuwa wote ni wazee, nafikiri hilo lingekuwa pambano la kufurahisha zaidi kuliko kumuweka kijana wa miaka 27 kupambana na bondia aliyestaafu.”
Hata hivyo, Tyson na Evander wamekuwa marafiki tangu Tyson alipomng’ata sikio mwaka 1997 na baadaye kuomba msamaha. TMZ iliripoti mwaka 2021 kwamba Evander na Tyson walitarajiwa kupigana pambano la tatu, lakini halikutokea.
Suala la kung'atana masikio limebaki utani tu kati ya wawili hawa.
Unadhani nani angeshinda iwapo wawili hao wangekutana tena ulingoni?