Mbunge wa Jimbo la Namtumbo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Vita Kawawa, ameainisha mafanikio ya miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika jimbo lake kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake huku akitoa wito kwa wanaotamani kugombea nafasi yake kusubiri hadi Julai 2025 ili kumpa nafasi ya kumaliza kazi aliyoianza.
Kawawa ameyasema hayo wakati akihutubia wananchi wa Kata ya Ligera Tarafa ya Sasawala wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma amesema kuwa ni muhimu azungumzie miradi mbalimbali ya maendeleo aliyoifanya kwa sababu watu wameanza kumchafua kana kwamba CCM na serikali yake haijafanya kitu. Ameeleza kuwa serikali imewekeza mabilioni ya shilingi katika sekta za afya, elimu, na miundombinu kwa manufaa ya wakazi wa Namtumbo.
Mbunge Kawawa amebainisha kuwa serikali imejenga Kituo cha Afya katika Kata ya Ligera kwa gharama ya shilingi milioni 500, pamoja na kuleta vifaa tiba. Amesema juhudi hizi ni sehemu ya mpango wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wa kuboresha huduma za afya kwa akina mama, watoto, na wazee.
"Kama Mbunge, mimi nawajibika kuwasilisha changamoto za wananchi kwenye ngazi ya taifa, ambapo fedha za miradi kama vituo vya afya na zahanati hutolewa," amesema Kawawa.
Katika sekta ya elimu, Mbunge Kawawa ameeleza kuwa shule mpya ya msingi imejengwa katika Kijiji cha Mtelawamwahi kwa gharama ya shilingi milioni 360. Pia, shule ya msingi Lukimwa imepata madarasa mapya na maabara, huku bweni likikamilishwa kwa msaada wa mifuko ya saruji 100 na fedha za serikali kiasi cha milioni 30.
Kwa shule ya msingi Ligera, shilingi milioni 59 zilitumika kujenga madarasa mawili na vyoo, huku shule ya Njomlole ikipokea milioni 46 kwa ajili ya madarasa mawili na milioni 4 kwa ukarabati.
Kuhusu barabara, Kawawa amesema mvua zinazoendelea kunyesha zimeathiri miundombinu, lakini fedha za kuweka kifusi tayari zimetengwa na kazi itaanza mara fedha hizo zitakapoingia.
Mbunge huyo amezungumzia changamoto ya maji katika Kata ya Ligera, akieleza kuwa juhudi za kuchimba kisima kirefu katika eneo la Namahoka zilikumbwa na matatizo ya vifaa vya kuchimba kutumbukia shimoni. Hata hivyo, juhudi zinaendelea kutafuta eneo mbadala kwa ajili ya mradi huo.
Kawawa amewataka wananchi kupuuza maneno ya wapinzani na kuendelea kumuunga mkono, akisema kazi kubwa ya maendeleo inaendelea kufanyika.
"Wananchi wasikubali kurubuniwa na madalali wa siasa, bali wasubiri muda ufike kwa ajili ya uchaguzi," amesema.
Stawa Ndauka, mkazi wa Ligera, amesema wanaridhishwa na juhudi za maendeleo zinazotekelezwa na Mbunge Kawawa, hasa katika huduma za afya, elimu, na miundombinu.