Ndugu mtoa hoja,
nitangulie kusema kua (kwa mawazo yangu) muungano uwepo ama usiwepo bado maisha ya Watanganyika na Wazanzibari yataendelea kuwepo. Kwa hiyo nje ya muungano matatizo tuliyonayo yataendelea kuwepo hali kadhalika pia ndani ya muungano bado matatizo tuliyonayo yataendelea kuwepo. nasema hivi kwa maana kua matatizo yanayotukabili kwa sasa (binafsi kwa mtazamo wangu) hayasababishwi na muungano bali kiini hasa cha matatizo ni viongozi kukosa sifa za uongozi.
Katika hali isiyokua ya kawaida utamkuta mtu anataka kuwa kiongozi, labda katika ngazi ya kijiji/mtaa (mwenyekiti), kata (diwani), jimbo (mbunge) au hata nchi (rais), cha ajabu utakuta mtu huyo ukimwuliza swali kua kwa nini anataka kua kiongozi jibu lake litakua jepesi sana eti anataka kuleta maendeleo ktk eneo husika. Kiuhalisia kazi ya kiongozi ni kuwaongoza watu wake waweze kufikia malengo yao waliyojiwekea. Sasa mbunge anaposema ataniletea maendeleo (sawa sikatai ila) nashangaa sana kwa sababu leo namchagua kuwa mbunge wangu lakini baada tu ya uchaguzi haonekani jimboni mpaka baada ya miaka mi5 kupita, sasa atapata wapi mawazo yangu ili aweze kuniongoza kufikia malengo yangu? (KUMRADHI MTOA HOJA, NIMETOKA NJE YA MUKTADHA ILI NIWEZE KUELEWEKA).
Nikirudi kwenye hoja ya msingi (kama nilivyoielewa mimi) ni kwamba watu wanataka kuwa viongozi ili waweze kutajirika kwa haraka kupitia rasilimali za taifa pamoja na jasho la wavuja jasho. hapa ndipo matatizo mengi ya sisi Watanzania (au hata Waafrika na sehemu zingine kwa ujumla) yanapoanzia, kisa nini? (eti siasa inalipa). Watu wanaacha taaluma zao ili wapewe vyeo vya kisiasa (wakuu wa wilaya kwa mfano kutoka uandishi wa habari, uhandisi, ualimu wa shule au chuo, nk.).
Niseme tu kwamba tusiumize vichwa kukomalia kuwa na muungano ama la, cha msingi tukomae na viongozi wetu japo wapunguze uroho wa madaraka. Hili tutalifanikisha kwa kuanza mchujo mkali ngazi ya mtaa na kuendelea, yaani tuanze kuwahoji hao wanaotaka kutuongoza kama wako tayari kutuongoza kweli. Na kama wako tayari kutuongoza basi tuwekeane utaratibu (sijui kama upo kwenye katiba) wa kuwatathmini hao viongozi kila baada ya muda fulani (mfano kwa mwenyekiti wa mtaa/kijiji kila baada ya miezi miwili au mitatu). Tathmini hii inaweza kufanyika kupitia (kwa mfano) kusomewa mapato na matumizi au kupewa taarifa za muhimu kuhusu utekelezaji wa mipango yetu pamoja na kutoa mapendekezo palipo na mapungufu. Tukiweza ngazi za chini hata huko kwenye ubunge na urais tutafanikiwa pia.
Nasisitiza tena kua haya masuala ya muungano (kuudumisha au kuuvunja) tuachane nayo wala hayatusaidii asilani. 'Nasikia' siku hizi tumeongeza na mambo mengine kama (mfano tu lakini) umakonde na unyakyusa, ufreemason na umizimu, ubara na uvisiwani, na mengineyo mengi ya kufanana na hayo. Vyote hivi ni kama mbwa kutupiwa mfupa halafu mwizi anaingia ndani na kufanya mambo yake bila bughudha yoyote.
Mwisho, kumradhi kama nimetoka nje ya mada husika.