Bado unasubiri kibali kutimiza ndoto zako? Soma dondoo hizi 7

Peter Agostino

Senior Member
Joined
Sep 23, 2016
Posts
105
Reaction score
229
1.Usisubiri ruksa wala kibali
Acha kuwa kama wanariadha au wacheza soka kusubiri kipenga(filimbi) ilie ndipo uanze kucheza mechi. Watu wengi linapokuja suala la kutimiza ndoto zao hawana tofauti na mwanamichezo anayesubiri filimbi au kengele ilie ndipo aanze jambo.


Ulimwengu wa namna hiyo wanaishi watoto. Hebu kumbuka ulipokuwa mtoto unasoma tangu chekechea mpaka chuo kikuu au ngazi nyingine yeyote ile. Katika kipindi hicho ulizoea kuishi kwa kufuata ratiba matukio karibu yote, mfano ulizoea shule kufunguliwa January na kufungwa June, somo la hesabu kuanza saa 4 na kumalizika saa 5 kisha unaenda mapumziko au kupata kikombe cha uji nk.


Mtindo huo jinsi akili ya binadamu ilivyoumbwa, hushika vitu kulingana na ratiba na hujizoesha yenyewe kutegemea ratiba. Kwahiyo mtu anapokuja kuwa mtu mzima na kuingia mtaani katika maisha ya kawaida hushtuka baada ya kukuta dunia tofauti kabisa na ile aliyoizoea shuleni, hukuta hamna ratiba tena, kipenga wala kengele kila anapotaka kuanza jambo.


Katika maisha hupaswi kusubiri wingu lipungue, mvua wala wimbi litulie ndipo eti uanze safari, wewe anza hivyohivyo, ikiwa utasema usubiri basi utasubiri hapo milele.


2.Usisubiri zamu yako.
Kuna dhana moja watu husema hivi; “Ili ufanikiwe inakubidi uwe na roho mbaya” Unajua ni kwanini wenye roho mbaya hufanikiwa haraka? Ukweli ni kwamba hawafanikiwi kwa sababu wana roho mbaya hapana, bali kinachowafanya watu wabaya wafanikiwe ni kule kutokufuata utaratibu wa kawaida kama wa kukaa foleni na kusubiri jambo, wapo radhi hata kuhonga au kutumia nguvu na kumpita mtu aliye hoi mstarini akisubiri ilimradi tu yeye awahi kupata huduma, hamwogopi mtu na hivyo kufanikiwa haraka. Tabia hii pia wanayo watu wazuri wanaofanikiwa lakini wao hawatumii njia haramu kutimiza ndoto zao.



3. Jitoe ndani ya ukanda wako wa faraja
Sawa sawa na kama tulivyoona kwenye mbinu ile ya kwanza, baadhi ya wasomi, sio wote lakini, hata wanaotoka vyuo vikuu hujikuta wanashindwa kuendana na mazingira ya nje ya mfumo wa vyuo na kutafsiri maarifa waliyoyapata kwa vitendo kwasababu wamezoea maisha ya kufanya kila kitu kwa maelekezo kutoka kwa maprofesa, wakufunzi, serikali na mfumo mzima wa chuo kwani kila upande unataka mwanafuzi huyo afanikiwe.



Lakini katika maisha halisi kwenye uwanja wa mapambano goli halitulii sehemu moja tena ili iwe rahisi kwako kufunga bao, linazunguka kusini, kaskazini, mashariki na magharibi. Uwanja muda wote umejaa ukungu na tope, siyo shwari tena kama ilivyokuwa chuoni, tena hamna refarii wala mshika kibendera, na hata ukivunjika mguu hamna yeyote anayejali na mpira utaendelea kama kawa.


4. Kuwa makini na wale wanaokuzunguka.
Pingu nyingine inayoweza kukuzuia usisonge mbele kabisa kutimiza ndoto zako ni aina ya watu wanaokuzunguka wewe mwenyewe.



Nakushauri kafanye jaribio lifuatalo;
Buni kitu chako na kitu hicho chaweza kuwa ni biashara, kazi ya sanaa kama vile wimbo, igizo, hadithi, shairi au chochote kile na kisha wafuate marafiki zako unaopenda kupiga nao stori waonyeshe hiyo kazi kisha waombe wakupe maoni yao kukukosoa.



Ikiwa marafiki hao mrejesho wao wa awali kabisa utaonyesha ukosoaji unaolenga kukusahihisha ili kazi yako iweze kuwa bora zaidi, basi ujue unao marafiki wazuri. Lakini ukiwaona wanabeza na kukukatisha tamaa kwa kusema wao wangeweza kubuni kitu kizuri kushinda hicho cha kwako, basi ujue kabisa marafiki zako hao hawakufai na tambua hilo siyo tatizo lako bali lakwao hivyo fikiria mara mbilimbili kupoteza muda wako mwingi ukiwa nao. Unahitaji marafiki watakaokuokoa na wala siyo kukuzamisha zaidi majini uangamie. Chagua kuwa nao au kukaa nao mbali lakini ndoto zako zitimie.


5. Muda mzuri wa kuanza ni sasa.
Pengine unatamani sana kufanya kazi fulani lakini kazi hiyo inahitaji kwanza mtu upate shahada(digirii). Ina maana kwamba utahitaji miaka 3-4 ili uweze kuwa na sifa za kupata kazi hiyo. Ikiwa una umri wa miaka 20 sasa ina maana utamaliza shahada yako ukiwa na miaka 25 au 26. Sasa unaweza kuona kama ni muda mrefu lakini hebu fikiria kama utaamua kuja kuanza ukiwa na miaka 30 au 40 utamaliza ukiwa na umri gani na kazi hiyo utaifanya lini? Itakuchukua muda mwingi sana ukijutia kutokuanza mapema. Kadiri utakavyoanza mapema ndivyo pia utakavyo timiza ndoto zako mapema.



6.Ondoa woga
Woga mkubwa watu wanaokuwa nao wanapotaka kutimiza ndoto zao ni woga wa kushindwa. Hebu jaribu kuwafikiria wanamichezo tena. Wachezaji hufanya makosa mengi sana wakati wa mazoezi wanapokuwa wakijiandaa na michuano. Lakini pia hata siku yenyewe ya mashindano(fainali) bado hufanya makosa na hata kushindwa au kufungwa magoli. Lakini hiyo haiwezi kuwafanya wasicheze tena michezo kwani kushindwa ni sehemu ya kujifunza ili wafanye vizuri zaidi hapo baadae.



7. Kuwa na Mshauri/mtu wako wa mfano
Umewahi kuwaona wapanda milima? Kwanini wanakuwa na waongozaji(Guids)? Mshauri si lazima awe ni yule uliyemtafuta mwenyewe hapana, wengine hujitokeza wenyewe tu kulingana na jinsi mwenyewe unavyoonyesha juhudi zako kwa watu na jamii. Mshauri anaweza kuibuka miongoni mwa watazamaji, wale wanaoshuhudia kile ufanyacho sawa na ilivyo kwa wachezaji chipukizi wazuri wa mpira wanaochaguliwa na kocha katika mechi za majaribio mchangani. Wachezaji wakati mwingine wala hawajui kama miongoni mwa watazamaji wapo makocha wanaofuatilia, hivyo usifichefiche tena kile unachokifanya.



Hitimisho
Sasa umepta mwangaza kuwa hakuna chohchote kile kinachoweza kukuzuia usitimize ndoto zako, amua ni nini unachohitaji kukamilisha ndoto zako kisha unaweza kuweka katika vitendo mbinu nilizokueleza hapo juu. Anza hata kama ni kidogo usiogope kama utashindwa wala usisubiri ruksa na kibali kutoka kwa mtu yeyote.


Makala hii imechukuliwa kutoka kaatika blogu ya JIFUNZEUJASIRIAMALI.
 
Maisha hayamsubiri mtu, ni kupambana.

T[emoji769]
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…