"Inaonekana hali ya kisiasa itakuwa ngumu na huenda hali hiyo ikasababisha Wanawake kutokugombea kwa hiyo lazima kuwajengea uwezo."
Hayo yalizungumzwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Victoria Luhiri tarehe Febuary 14, 2019 katika mdahalo wa ushiriki wa Wanawake kwenye Uongozi uliandaliwa Mtandao wa jinsia Tanzania.
Maneno hayo ya Victoria yalimgusa bi Bahati Issa Suleiman na kutilia mkazo umuhimu wa kuwepo mafunzo kwa Wanawake wanaotaka kugombea uongozi ili kupata kushajihika kuingia kwa wingi katika siasa na kufikia 50/50 katika uongozi.
Bahati (umri wa Miaka 52), Mkaazi wa Kikungwi, Mkoa wa Kusini Unguja ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwa pamoja na Katibu wa UWT Tawi Kikundwi Mwaka 1995, Mjumbe Mkutano Mkuu Jimbo Mwaka 2005, Mwenyekiti wa UWT Jimbo 2017, pia aliwahi kugombea Udiwani Mwaka 2023, amesema ufanisi katika masuala ya uongozi hutokana na ari ya mtu lakini pia kwa kupata mafunzo.
Anasema "Kupatiwa mafunzo ya uongozi ni kitu cha maana sana na kinatupa hamasa Wanawake kuweza kugombea nafasi za uongozi."
Kwa Zanzibar TAMWA ni tasisi ya kwanza ambayo imechukua Wanawake wengi na kuwapa mafunzo yanayotowa muongozo wa namna ya kugombea nafasi za uongozi.
"Mimi baada ya mafunzo kutoka TAMWA nilipata ujasiri mkubwa wa kugombea nafasi ya udiwani licha ya kuwa sijafanikiwa lakini niliweza kupambania sijavunjika moyo," anasema.
Anaeleza lazima Wanawake wakitaka kugombea wawe na uthubutu na ujasiri kwani kuna wengi ambao wanavunjwa moyo na kupoteza msimamo wa kufanya wanachotaka.
Kupata taarifa na matukio kuelekea uchaguzi mkuu 2025 kwa kila mkoa ingia hapa: Special Thread: Mijadala na Matukio ya Uchaguzi Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Mafunzo ndio pekee yatakayotowa muelekezo na njia za Wanawake kupita ili kupata nafasi hizo za Uongozi ifikapo 2025.
Tukiwa kwenye mafunzo hukutana Wanawake tofauti na kila mmoja hupata mawazo kutoka kwa mwenzake na pia tunapeana uzoefu na changamoto tunazopitia inakuwa rahisi mwanamke anaetaka kugombea kujipanga.
Mmoja wa watu walionufaika na mafunzo Uongozi na kuhesabika kama mmoja wa viongozi bora waliopata haya mafunzo ni Zainab Salehe Salim, maarufu kwa jina la ‘Zasasa’.
Soma Pia kwa taarifa zaidi zinazowahusu wanawake kipindi hichi cha uchaguzi: Kipindi hiki cha Uchaguzi wanawake wanapata nafasi ya kutosha kushiriki kwenye masuala ya uchaguzi?
Zainab alikuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (Zanzibar University) alipatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo Wanawake kushika hatamu za uongozi.
Dada huyu aliyewahi kuwa Makamo wa Rais katika Serikali ya Wanafunzi ndani ya chuo hicho.
Katika safari yake ya uongozi alikumbana na changamoto nyingi, zikiwemo zile ambazo hakuzitarajia ndani na nje ya chuo.
Hata hivyo, alikata tamaa na alikataa kuwa kiongozi na kuona amerejeshwa nyuma na badala yake haukuwa na nia tena ya kuwa kiongozi kwani hakuona mambo yaliyompa nguvu zaidi za kusonga mbele katika safari yake.
"Ilifika wakati sikutaka kuendelea kuwa Makamo wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi chuoni," anasema na kuendelea:
“Lakini baada ya kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyokusanya taasisi nyinyi, zikiwemo TAMWA na Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) nilipata uelewa mzuri kuhusu uongozi na kuamua kusonga mbele.”
Baada ya kushiriki katika mjadala TAMWA walimchukua na kumpatia mafunzo ya kuwawezesha Wanawake katika uongozi na hivyo kumshajiisha zaidi kubadili maamuzi na kuendelea na uongozi.
Amesema mafunzo yalimuongezea ujasiri na kujua vizuri changamoto ambazo Mwanamke anatakiwa kuishi nazo anapokuwa kiongozi na kufahammu vizuri njia sahihi ya kupita ili kufanikiwa.
Sensa ya Watu na Makaazi ya Mwaka 2022 inaonesha Zanzibar ina watu 1,889,773 kati ya hao wanaume ni 915,492 huku Wanawake ni 974,281 hii ikimanisha Wanawake ni wengi.
Kwa wingi huu ipo haja ya Wanawake kupewa fursa sawa na Wanaume ili kupata watetezi wa keki katika ngazi za maamuzi na kuwasilisha changamoto zao.
Mwananchi wa Kijiji cha Koani ambaye ni Muanzilishi wa Vikundi vya Ushirika bi Lela Hamadi amesema mafunzo yapewe kipaumbele hasa kwa Wanawake wanaotaka kugombea kwani huamsha mawazo na fikra za wengi wanauwezo wa kuongoza ambao wanaogopa kutokana na maneno ya wanajamii.
Ndani ya jamii zetu kuna watu wenye uelewa wa karibu na wale ambao uelewa ni mdogo wao hadi waone mafanikio katika jambo hivyo kukiwepo na mafunzo itakuwa na msukumo mkubwa ya kupata wengi wanaotaka kugombea.
"Mafunzo yananguvu ya ushawishi na msukumo kubwa wa kuongeza idadi kubwa ya Wanawake kushiriki katika uongozi.
“Na mimi nilipata mafunzo kutoka TAMWA ndio nikaweza kumudu kuanzisha vikundi 570 katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo Kisakasaka, Fumba, Bweleo, Darajabovu, Kibaha, Kisarawe, Mwanza kwasababu mbinu za kufanya hivyo nishapatiwa kwenye mafunzo.
"Kila kitu kinahitaji ujuzi na mtu akipatiwa mafunzo huteleza jambo kwa ufanisi na hata Wanawake wakipatiwa elimu ya kugombea nafasi za uongozi wataongoza vizuri."
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo mkataba wake ulitiwa saini mwaka 2008 inaeleza kutaka kuondoa utofauti na kuwatenga Wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo na kusaidia kuwepo usawa wa kijinsia katika nchi wanachama na kufikia asilimia 50/50 kwenye maamuzi, Serikali na taasisi binafsi.
Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ, Dkt Mzuri Issa Ali amesema wanachukua hatua za kuwasaidia Wanawake kushiriki katika uongozi
Hii ni pamoja na kutoa elimu ya kujitambua, kujielewa na kuthubutu kuwa wagombea huku wakizijuwa haki zao za kidemokrasia.
Wanawake wa Unguja na Pemba wamepatiwa mafunzo ya uongozi ambayo yamewasaidia kutambua vikwazo wanavyoweza kukutana navyo na namna ya kukabiliana navyo.
Aliwanasihi Wanawake wanaotaka kuingia kwenye uongozi kutokuwa na hofu kwani hiyo ni haki yao iliyoainishwa katika Katiba na mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa ambayo nchi yetu imeiridhia na kuamua kuitekeleza.
Dira ya Zanzibar ya 2050 imeelezea jinsi gani masuala ya usawa wa jinsia juu ya kuondoa unyanyasaji na kuimarisha mifumo ya uwezeshaji wanawake, ikiwa pamoja na kuinua na kutoa nafasi za uongozi kwa wanawake.
Vilevile imelenga kuongeza fursa na kuwawezesha katika vyombo vya kutoa maamuzi na kwenye shughuli za uchumi, kijamii, siasa, ngazi za utawala na Huduma za Sheria.
ANDIKO LA: Thuwaiba Habibu