Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Andrew Msechu
SERIKALI jana ilitangaza bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2010/11 ambayo inaonekana kupunguza makali kwenye baadhi ya sekta huku ikiongeza makali kwenye maeneo mengine.Bajeti hiyo ya Sh1.1 trilioni inaendelea kuweka kipaumbele katika uboreshaji miundombinu, elimu, afya, kilimo, na maji huku ikielekeza nguvu katika kubana matumizi ya serikali, ukusanyaji zaidi wa kodi, kitu kilichopigiwa kelele na washirika wa maendeleo ambao wamezuia Sh297 bilioni wanazotarajiwa kuchangia kwenye bajeti hiyo.
Bajeti hiyo iliyowasilishwa bungeni jana na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo imeanisha maeneo mengi ambayo yatasaidia kufanikisha mpango wa Kilimo Kwanza, ikiwa ni pamoja na kuondoa kodi na ushuru katika pembejeo za kilimo na zana za ufugaji na kupunguza kwa asilimia moja kodi ya mapato ya wafanyakazi kutoka asilimia 15 na kuwa 14 kwa kima cha chini cha mishahara.
Hata hivyo, bajeti hiyo haijaonyesha kama imepanua wigo wake wa kodi ili kuhakikisha inatimiza malengo yake ya kukusanya angalau asilimia 70 ya fedha za bajeti hiyo, ambayo inaonekana itaendelea kutegemea wahisani ili kufanikisha miradi ya maendeleo.
Mbali na kupunguza kodi ya mapato kwa asilimia moja kwenye mshahara wa kima cha chinim serikali pia imeitikia shinikizo la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) kwa kutangaza kuwepo kwa ongezeko la mshahara kwa kima cha chini, lakini kiwango kamili kitatangazwa na waziri husika.
Tucta imetishia kuitisha mgomo wa wafanyakazi wote kutokana na serikali kuchelewa kutangaza ongezeko la kima cha chini cha mishahara baada ya pande hizo kufikia makubaliano katika mkutano uliofanyika Mei 8. Waziri husika alitakiwa atoe tangazo hilo ndani ya siku 21 tangu tarehe ya maafikiano, lakini hadi leo bado halijatolewa.
Mkullo alilieleza Bunge kuwa bajeti ya mwaka huu wa fedha ni muendelezo wa mkakati wa miaka mitano, ambapo baada ya mwaka wa fedha 2009/2010 unaomalizika mwezi huu, inakamilisha kipindi cha miaka mitano cha Serikali ya Awamu ya Nne iliyoingia madarakani Desemba 2005.
Mkulo alisema serikali imezingatia umuhimu wa kupunguza kiwango cha chini cha Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi kutoka asilimia 15 hadi asilimia 14 na nyongeza ya kima cha chini cha mshahara, ikiwa na lengo la kuwaongezea kipato na kuwapunguzia mzigo wa kodi watumishi wa umma wenye kipato cha chini.
Hadi sasa, serikali ilikuwa ikikata kodi ya asilimia 15 kwenye mshahara unaoanzia Sh100,001 hadi Sh360,000, kiwango ambacho wafanyakazi wamekuwa wakikilalamikia kuwa kinatafuna mshahara wao. Hata hivyo, kwa tangazo hilo, viwango vinavyokatwa kwenye mishahara ya kuanzia Sh360,001 vitabakia kama vilivyo.
Bajeti hiyo pia imeweka unafuu mkubwa kwenye kilimo ambacho kimetengewa Sh903.8 bilioni kutokana na kuweka misamaha mingi katika vifaa vya kilimo, pembejeo na usafirishaji wa mazao. Hata hivyo, bajeti hiyo haijagusia kabisa sekta ya uvuvi, ambayo katika siku za karibuni imeonekana kuwa inaweza kuliingizia taifa mapato makubwa.
Katika kuhamasiaha maendeleo ya kilimo, serikali imefanya mabadiliko kadhaa katika Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka shambani hadi kwenye viwanda vya usindikaji kwa wakulima wenye kilimo cha mkataba wa miwa, mkonge na chai.
Pia imesamehe kodi hiyo kwenye mashine na vifaa vya kukusanya, kusafirisha na kusindika maziwa, kutoa unafuu wa kodi ya ongezeko la thamani vifaa vinavyouzwa kwa wataalamu wa mifugo waliosajiliwa, zana za kilimo, usafirishaji wa maua kwa ndege kwenda nje ya nchi, huduma za kuzalisha mifugo kwa njia ya kupandisha mifugo na kutumia mashine maalum za kuzalishia/kutotolea vifaranga.
Pia imeweka nafuu maalum kwa kodi kwenye mabanda yanayotumika katika kilimo cha maua, uuzaji wa bidhaa na huduma zitolewazo kwa wakulima waliosajiliwa au mashamba ya vyama vya ushirika kwa ajili ya kujenga miundombinu ya mashamba kama vile mitaro ya umwagiliaji, barabara za mashambani, ujenzi wa maghala au huduma nyinginezo za namna hiyo.
Hatua nyingine za kutoa ahueni ni kurekebisha kifungu cha 11 cha Sheria ya Kodi ya Mapato ili kuweka wigo wa ukomo wa maeneo ya uchimbaji wa madini kwa nia ya kudhibiti gharama zinazotakiwa kutolewa katika kukokotoa faida itakayotozwa kodi ya mapato kuwa ni zile za eneo husika tu, ikihusisha kampuni zote za madini.
"Kwa kuwa bado kuna biashara nyingi zinazofanywa na watu wasiokuwa na namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN), napendekeza kodi ya zuio inayozuiwa na serikali kwa wauzaji wa bidhaa na watoa huduma waliokuwa na TIN, izuiwe pia na wafanyabiashara wote waliosajiliwa ili kuwahamasisha wasiokuwa na namba za utambulisho kwenda kusajiliwa.
Hatua hizi za Kodi ya Mapato kwa pamoja zitapunguza mapato ya serikali kwa kiasi cha Sh 4.468 bilioni," alisema.
Alisema marekebisho ya ada ya usajili na uhamisho wa umiliki wa magari na pikipiki yatafanyika kwa kuongeza viwango vya ada, hatua inayotarajiwa kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha Sh3.19 bilioni.
Katika mapendekezo hayo, Mkullo alitaka kufanyika kwa marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa ili kupunguza ushuru kutoka Sh97 hadi Sh80 mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ili kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa hapa nchini, ikiwa na lengo la kukuza viwanda, ajira na mapato ya ndani.
Wakati serikali ikiondoa makali kwenye maeneo hayo, wananchi watalazimika kujikuna zaidi watakapotaka bidhaa za matumizi ya ziada baada ya serikali kuongeza ada kwenye magari, kuongeza kodi kwenye vinywaji vya kileo.
Katika bajeti hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na Watanzania, Mkullo alisema viwango maalum vinavyopendekezwa ni katika vinywaji baridi, akieleza kuwa viwango hivyo vitaongezeka katika bia inayotengenezwa na nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa.
Alisema marekebisho hayo yanazingatia kiasi cha wastani wa mfumuko wa bei na kwamba sasa vinywaji baridi kodi itaongezeka kutoka Sh58 kwa lita hadi Sh63 kwa lita na bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini, na ambayo haijaoteshwa itapanda kutoka Sh209 kwa lita hadi Sh226 kwa lita.
Marekebisho mengine ni kuongeza kodi katika bia nyingine zote, kutoka Sh354 kwa lita hadi Sh382 kwa lita, wakati mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 itapanda kutoka Sh1,132 kwa lita hadi Sh1,223 kwa lita, vinywaji vikali kutoka Sh1,678 kwa lita hadi Sh1,812 kwa lita, kurekebisha viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara.
Alieleza kwamba bia nyingine zote zizizotengenezwa nchini pia zitapanda na mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 utapanda pia, hali kadhalika vinywaji vikali.
Serikali pia imependekeza marekebisho ya viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara, ikitaka sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75 kwa kila sigara 1,000.
Pia kwa sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, wakati sigara nyingine zenye sifa tofauti na hizo za awali kutoka sh34, 633 hadi sh26,604 kwa sigara 1000.
"Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara pia kutoka shilingi 12,441 hadi Sh13,436 kwa kilo, na ushuru wa (cigar) unabaki kuwa asilimia 30. Hatua hizi katika ushuru wa bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 20.042 bilioni," alisema.
Mkulo aliweka bayana kwamba bajeti hiyo aliyoiwasilisha katika mkutano huo wa mwisho wa Bajeti kwa Bunge baada ya miaka mitano ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Nne, ina nia njema ya kuwapa fursa ya kurudi kwa wananchi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, kwa ajili ya kuomba ridhaa yao ya kurudi tena bungeni.
"Bajeti ya mwaka huu, sera za matumizi zililenga kutoa upendeleo wa mgao wa matumizi kwenye sekta za kipaumbele ikiwa ni pamoja na Elimu, Miundombinu na Kilimo.
Aidha sera za matumizi pia zilihusisha kuimarisha mfumo wa usimamizi wa fedha na ufuatiliaji wa matumizi pamoja na tathimini ya mpango wa bajeti ili kuhakikisha rasilimali fedha inatumika kwa ufanisi," alisema.
Mkulo alisema kwa kuzingatia maeneo ya kipaumbele aliyoyaainisha, maeneo yaliyopata upendeleo wa ongezeko kubwa katika bajeti ni Miundombinu iliyopata ongezeko kwa asilimia 37.3, Kilimo iliyopata ongezeko la asilimia 35 na Elimu iliyopata ongezeko la asilimia 17.2.
Afya imepata ongezeko la asilimia 25.2, Maji ongezeko la asilimia 14.5, Nishati na madini ongezeko la asilimia 14.6.
Waziri Mkulo alisema Sh30 bilioni zimetengwa kwa ajili ya utafiti na ufuatiliaji, kwa ajili ya maeneo yatakayopata upendeleo katika awamu ya kwanza ambayo ni ukarabati wa Miundombinu katika taasisi zinazohusika na tafiti mbalimbali.
"Kwa hiyo, bajeti ya mwaka wa fedha 2010/2011 inalenga kuendelea na utekelezaji wa sera na malengo ya kiuchumi na kijamii. Katika kipindi hiki, yamekuwepo mafanikio ya kuridhisha katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kuimarisha miundombinu ili kuwezesha uchumi kukua na kupunguza umaskini," alisema.
Bajeti hiyo pia imerekebisha kwa asilimia nane viwango maalum vya ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa zinazotozwa ushuru huu isipokuwa zile za mafuta ya petroli, kwa kuzingatia kiasi cha wastani wa mfumuko wa bei.
Katika kukabiliana na makali ya bajeti hiyo, Mkulo alisema serikali imeamua kudhibiti na kusimamia vyema matumizi yake, hasa katika mawasiliano, nishati na matumizi ya ununuzi na matengenezo ya magari.
Katika bajeti hiyo, Mkullo alisema katika mikakati ya mwaka huu wa fedha, serikali itaendelea kutekeleza sera za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuweza kugharamia sehemu kubwa ya matumizi ya kawaida, ikiwemo kuendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa kuhakikisha kuwa pale inapowezekana malipo yanafanyika kwenye mabenki.
Mikakati mingine aliyoieleza ni pamoja na kuweka mkakati wa kuboresha huduma za utalii kwa kutathimini hoteli ili ziwe katika viwango vinavyokubalika kimataifa kwa lengo la kuongeza mapato yatokanayo na ada, kuhimiza utekelezaji wa Sheria ya Fedha inayoelekeza mashirika na taasisi kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali na kuendelea kupanua wigo wa kodi kwa kusajili walipakodi wapya na kuimarisha uchumi tulivu pamoja na kuweka mazingira bora ya biashara ili kuwezesha sekta binafsi kukua.
Alisema serikali pia itaendelea kusimamia kwa karibu mageuzi makubwa yanayoendelea ndani ya Mamlaka ya Mapato (TRA) chini ya mpango wake wa tatu wa maboresho ya miaka mitano ambayo yamekuwa msingi wa kukua kwa mapato ya ndani mwaka hadi mwaka na kuchukua hatua za kuboresha ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kutoka Wizara na Idara za Serikali.
Pia kupitia upya utaratibu wa kutoa misamaha ya kodi kwa lengo la kuongeza udhibiti na kuendelea kuhakikisha kwamba watendaji wa mamlaka za serikali za mitaa wanajengewa uwezo kwa kuwapatia utaalamu wa kutosha ili kuongeza ufanisi katika ukadiriaji na ukusanyaji wa mapato katika serikali za mitaa.
Bajeti 2010/11 ni ya kujumlisha na kutoa