Bajeti imepita, utekelezaji uwe makini

Bajeti imepita, utekelezaji uwe makini

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
Tangu Juni 13, mwaka huu, Waziri wa Fedha, Dk. Willim Mgimwa, alipowasilisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2013/14 ambayo aliomba bunge kupitisha Sh. trilioni 18.249 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje, kumekuwa na mjadala wa kina ndani ya Bunge lakini hata nje ya Bunge kwa nia ya kuboresha mapendekezo hayo.

Baada ya kuwasilishwa kwa bajeti hiyo ambayo inajumuisha mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yanayotarajiwa kufikia Sh. tilioni 11.154.1 sawa na asilimia 20.2 ya Pato la Taifa, wabunge walianza kuijadili Jumatatu ya Juni 17, mwaka huu wakitoa hoja mbalimbali juu ya udhaifu wa uzuri wa bajeti hiyo ambayo inakadiriwa kwamba mapato kutokana na vyanzo vya halmashauri yanatafikia Sh. bilioni 383.5 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.

Hoja za wabunge ambazo zimekuwa na joto kubwa ni suala la ongezeko la ushuru wa mafuta ya petrol, kodi kubwa kwenye magari madogo, punguzo dogo kwenye kodi ya mapato ya wafanyakazi ya lipa kadri unavyapata (PAYE), kodi mpya kwenye simu, ambazo kwa ujumla wake wabunge wengi walionyesha wasiwasi kuwa zitaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi, hivyo wakashauri serikali kuzipunguza.

Serikali pia ilishambuliwa kwamba imeshindwa kuwa na ubunifu katika kuibuka na vyanzo vipya vya mapato na kuendelea na vya zamani vya mafuta, sigara, vinywaji baridi na vikali, huku maeneo mengine ambako maliasili za taifa zinavuna yakifumbiwa macho hivyo kutokuchangia kiasi cha kutosha katika maendeleo ya taifa.

Wakati wabunge wakihoji sababu za kuibuka na kodi kwenye huduma za simu ambayo itawaongezea gharama za maisha, waliituhumu pia serikali kwa kuendelea na kasumba ya matumizi makubwa. Matumizi haya yalibainishwa kuwa ni watumishi wa umma katika safari, posho, semina, ununuzi wa mafuta na vilainisho.

Pamoja na hoja na michango mbalimbali iliyotolewa na wabunge kwa ujumla wao tangu kuanza kwa mkutano wa bajeti Aprili mwaka huu, yapo mengi ambayo serikali imechukua, lakini pia kuna mengi ya maana ambayo kwa hakika hakupata ufumbuzi na wala serikali haijaona kuwa kuna sababu ya kuchukua na kutoa majibu ya kina.

Kwa mfano, wakati serikali ikizungumzia habari ya kujenga viwanja vya ndege, imeshindwa kutambua kuwa kinachotakiwa kwa haraka kwa sasa ni kuelekeza nguvu nyingi zaidi na kwa kasi kubwa kufufua reli. Reli ndiyo suluhisho la kipekee kwa huduma za usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo.

Hakuna taifa lolote duniani ambalo lilipiga hatua kubwa za maendeleo kwa kutegemea barabara kama njia kuu ya kusafirisha mizigo, huduma na abiria.

Kwa maana hiyo hoja ya kuelekeza nguvu zaidi kwenye kujenga reli na kufufua hizi zilizopo ni ya masingi na ambayo kama kweli tumedhamiria kupata matokeo makubwa ya kujenga uchumi kwa matokeo makubwa sasa (big results now) hakuna jinsi ni lazima kipaumbele cha kwanza, cha pili na tatu viwe ni ujenzi wa reli.

Hata hivyo, pamoja na ukweli kwamba siyo kila pendekezo la wabunge limezingatiwa, jana waliipitisha bajeti husika baada ya kupiga kura.

Kinachofuata sasa kuanzia Julai mosi mwaka ni utekelezaji wa bajeti hiyo.
Kwa miaka mingi kumekuwa na tofauti ya utekelezaji wa bajeti na kile kilichopitishwa na bunge. Fedha nyingi ama hazitolewi kwa wakati au hazitolewi kabisa.

Pia kwa miaka mingi mfumo mzima wa upitishaji wa bajeti ulikuwa unakwamishwa na changamoto ya muda. Utaratibu wa kupitisha kwanza bajeti kuu ndipo zifuate za wizara moja moja zilikuwa zinafikisha mkutano wa bajeti kwenye katikati na hata wakati mwingine mwishoni mwa Agosti wakati kisheria utekelezaji wake ulipashwa kuanza mwaka wa fedha unapoanza Julai mosi.

Hali hii ilifanya utoaji wa fedha kuchelewa, mara nyingi fedha za maendeleo zilikuwa zinafika kwenye maeneo husika, hususan kwenye halmashauri zikiwa zimechelewa mno na nyingi zilikuwa hazitumiki kabisa na matokeo yake ni kurejeshwa Hazina.

Mwaka huu utaratibu mpya wa kupitisha bajeti umeanza kwa serikali kuwasilisha kwanza bajeti za wizara moja moja na kisha kumalizia na bajeti kuu ya serikali, lakini pia utaratibu wa kuanza kuwa mkutano wa bajeti umebadilika kutoka Juni hadi Aprili, kwa maana hiyo mchakato mzima wa kupitisha bajeti ya serikali pamoja na wizara zake unamalizika kabla ya kuanza kwa mwana mpya wa fedha Julai mosi.

Tumeona ufanisi katika kupitisha bajeti hiyo licha ya kuwa na mapungufu yake kwa maana nyingi, vipaumbele kutokupangwa sawa sawa, kiasi kidogo cha fedha kwenye baadhi ya maeneo nyeti yanaohitaji fedha zaidi; hata hivyo mabadiliko ya muda wa mchakato wa bajeti umekuwa na manufaa ya kiutendaji katika kuipitisha.

Ni matarajio yetu kwamba baada ya kazi hii iliyofanyika Dodoma kuanzia Aprili hadi jana, utaanza kutekezwa kwa vitendo halisi kuanzia Jumatatu ijayo, yaani Julai mosi mwaka huu.

Kwa kufanya hivyo pamoja na changamoto ambazo zimeibuliwa na wabunge na wadau wengine, mwaka wa fedha ujao Watanzania kwa ujumla wao wataona usimamizi na utekelezaji wa bajeti ulio bora zaidi kuliko miaka mingi iliyopita.




CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom