Bajeti ya 2026/27: Mabadiliko ya Kodi, nani ananufaika, nani anaongeza mzigo?

Waufukweni

JF-Expert Member
Joined
May 16, 2024
Posts
5,383
Reaction score
18,776
Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 imeonyesha ongezeko la matumizi kutoka Tsh. Trilioni 56.49 katika mwaka 2025/26 hadi Tsh. Trilioni 62.33, sawa na ongezeko la zaidi ya Tsh. Trilioni 5.8. Ongezeko hili linaashiria dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha huduma za kijamii, utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kukuza uchumi wa taifa.

​

Ukuaji wa uchumi ulifikia asilimia 5.9 mwaka 2025, kiwango ambacho kiko chini kidogo ya lengo lililowekwa la asilimia 6, lakini ni ongezeko ikilinganishwa na asilimia 5.6 ya mwaka 2024. Ukuaji huu ulichochewa zaidi na sekta za kilimo, ujenzi, shughuli za kifedha na bima pamoja na sekta ya madini. Kwa upande wa mchango katika Pato la Taifa (GDP), sekta ya kilimo iliongoza kwa kuchangia asilimia 24.3, ikifuatiwa na sekta ya ujenzi iliyochangia asilimia 11.9, huku sekta ya madini na uchimbaji mawe ikichangia asilimia 10.3.

Katika eneo la kodi, bajeti ya 2026/27 imeleta mabadiliko yanayolenga kuongeza ushiriki wa sekta binafsi huku ikipanua wigo wa walipakodi, tofauti na bajeti ya 2025/26 ambayo msisitizo wake mkubwa ulikuwa kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuongeza idadi ya walipakodi wapya.

Mabadiliko ya Kodi na Sheria nyingine:

Kodi za Moja kwa Moja (Income Taxes)

  • Kupunguzwa kwa kodi ya faida inayochukuliwa kama imegawiwa kwa wenyehisa (deemed distribution) kutoka 30% hadi 15%.
  • Msamaha wa miezi 12 (Likizo ya Kodi) kwa walipakodi wapya waliosajiliwa chini ya mfumo wa kodi ya makadirio (presumptive tax).
  • Ongezeko la kodi ya huduma za kidijitali kutoka 2% hadi 3%.
  • Kodi ya zuio (withholding tax) ya 1% kwenye malipo ya mazao ya chakula, wanyama hai, maziwa yasiyosindikwa, samaki, na mabondo ya samaki.
Kodi Zisizo za Moja kwa Moja (Indirect Taxes)
  • Kuanzishwa kwa ukomo wa lazima wa siku 30 wa urejeshaji wa kodi ya VAT, kukiwa na riba endapo utatokea ucheleweshaji.
  • Kuondolewa kwa ukomo wa muda wa kuhairisha kodi ya VAT (VAT deferment) kwa bidhaa za mtaji zinazoingizwa nchini.
  • Mabadiliko kutoka marekebisho ya ushuru wa bidhaa kila baada ya miaka mitatu hadi marekebisho ya kila mwaka, kukiwa na ongezeko la 8% katika Mwaka wa Fedha wa 2026/27.
Mabadiliko Mengine
  • Kutambuliwa kwa misamaha ya kodi katika Makubaliano ya Mfumo (Framework Agreement) kwa wawekezaji wa sekta ya madini.
  • Kuongezwa kwa muda wa kisheria wa utatuzi wa migogoro ya kodi nje ya mahakama kwa njia ya amani hadi siku 90 (kutoka siku 60).
  • Pendekezo la kutekeleza hatua mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya malipo yasiyo ya fedha taslimu (cashless economy).
Je, nani ananufaika, nani anaongeza mzigo?

Kwa kifupi mabadiliko ya kodi ya 2026/27 yanaonyesha kuwa watakaoisoma namba na kubeba mzigo mkubwa ni walaji wa bidhaa za ushuru (kama vinywaji na mafuta) kutokana na ongezeko la kila mwaka la 8%, watumiaji wa huduma za kidijitali zilizopandishwa kodi hadi 3%, pamoja na wadau wa sekta ya kilimo na uvuvi wanaokabiliwa na kodi mpya ya zuio ya 1%.

Kwa upande mwingine, wanaokula mema ya nchi na kunufaika zaidi ni wenyehisa wa makampuni waliopunguziwa kodi ya usambazaji faida hadi 15%, wafanyabiashara wapya wanaopewa likizo ya kodi ya mwaka mzima, pamoja na makampuni makubwa yanayodai marejesho ya VAT ambayo sasa yatalipwa ndani ya siku 30 kukiwemo na riba kukiwa na ucheleweshaji.

Kwa ujumla, bajeti ya 2026/27 inaonyesha mabadiliko ya kimkakati kutoka katika kutegemea zaidi matumizi ya Serikali kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi kwenda katika kuhamasisha uwekezaji, ubunifu na ushiriki mkubwa wa sekta binafsi. Mafanikio ya bajeti hii hayataamuliwa na ukubwa wake pekee, bali na kiwango cha utekelezaji wake na uwezo wake wa kubadilisha maisha ya wananchi kupitia ajira, huduma bora na fursa za kiuchumi.

Soma zaidi kuhusu Bajeti:
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…