Balozi Mulamula: Nitamkumbuka Lukuvi kwa malezi yake Bungeni, kifo chake ni pigo kubwa kwa Taifa

News Tz1

Member
Joined
Nov 28, 2025
Posts
82
Reaction score
110
Aliyewai kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, ambaye pia ni Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Afrika kuhusu masuala ya Wanawake, Amani na Usalama, ameeleza kupokea kwa mshtuko kifo cha Mbunge wa Isimani, William Lukuvi.

Akizungumzia msiba huo leo, Balozi Mulamula alisema kiongozi huyo, ambaye alikuwa Chief Whip Bungeni, alikuwa anawaongoza na kuwaelekeza wabunge. Ameongeza kuwa atamkumbuka zaidi kwa malezi bora aliyowapa yeye pamoja na wenzake walipokuwa Bungeni.

Soma Pia: Waziri William Lukuvi (na Mbunge wa Isimani) afariki Dunia

“Mimi siwezi kusema nilifanya naye kazi, maana alikuwa kiongozi wetu mwandamizi. Binafsi nilijifunza mengi kisiasa kutoka kwake, hususan nikiwa Bungeni; alikuwa kama mwalimu kwangu. Kwa kweli kifo chake ni pigo kubwa sana kitaifa. Ameacha pengo kubwa Serikalini na Bungeni,” amesema Balozi Mulamula.

Aidha, ametoa salamu za pole kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Musa Hassan Zungu, kufuatia msiba huo wa kiongozi aliyedumu katika utumishi kwa miongo kadhaa.

“Tutaendelea kumkumbuka daima Mheshimiwa Lukuvi kwa unadhifu wake, uzoefu wake mkubwa, busara zake na ucheshi wake. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Mungu awe faraja kwa Mama Lukuvi na watoto katika kipindi hiki kigumu cha kumpoteza mpendwa wao. Bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe,” amesema Balozi Mulamula.

Taarifa za kifo cha Mbunge Lukuvi, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), zilitolewa jana na Katibu Mkuu Moses Kusiluka. Taarifa hiyo ilieleza kuwa umauti ulimkuta kiongozi huyo Machi 25, 2026, alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma, kwa tatizo la mshtuko wa moyo.

Ikumbukwe kuwa Lukuvi alikuwa Mbunge tangu mwaka 1995, na ameshika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo uwaziri katika wizara tofauti, hususan Wizara ya Ardhi.
 
Kifo chake ni pigo kwa taifa labda taifa la nyumbani kwake mkewe vimada na anaowajua mwenyewe lukuvi
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…