Barua ya wazi kwa Mufti wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Barua ya wazi kwa Mufti wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Yusufu R H Sabura

JF-Expert Member
Joined
Jun 26, 2020
Posts
355
Reaction score
486
Assalam alaykum warahmatullahi wabarakaatuh.

Habari ya majukumu hapo ofisini kwako, bila shaka umzima wa afya na waendelea vyema na majukumu waliyokupatia waislamu katika kukitumikia kiti hicho. Pamoja na raddi na mivuguvugu mingi unayoipata toka kwa mahasimu wako wa kiitikadi lakini bado unaonesha ukomavu na ustahimilivu mkubwa wa kiumri na kielimu katika uongozi wako kama kiongozi wa waislamu hapa Tanzania.

Bila kuchukua nafasi, Nataka nikuthibitishie kuwa waislamu wengi wanaridhika na utendaji wako wa kazi kama mufti. Lakini pia nikupe moyo wa kuendelea na majukumu bila kujali kelele za watu kwa vile hata mtume Muhammad(S.A.W) alikosolewa na waislamu waliodhani wangekuwa sahihi kuliko yeye. Hivyohivyo kwa makhulafaau arrashidun, ije kuwa mufti wa Tanzania ? kaza buti mzee.

Mufti Abubakar Zubeir, lengo kubwa la kukuandikia ujumbe huu ingawa si katika njia zilizo rasmi, ni kukudokezea uboreshaji wa utoaji wa elimu ya kiislamu pamoja na kuboresha watoaji wa elimu hiyo hapa nchini kwetu Tanzania. Sina maana ya kuonesha kuwa ofisi yako haiwezi kufikiria, na wala sina maana ya kwamba wazo hili mimi ndiyo wa kwanza kuwa nalo hapana, bali ni kuonesha kuguswa na mazingira ya kielimu yaliyopo tangu uislamu ufike nchini kwetu hadi sasa nchi yetu inaitwa Tanzania.

Niliwahi kuhudhuria mashindano ya kimataifa ya Qur an tukufu yaliyoandliwa na mama Aisha Sururu Allah amlipe kila la kheri, katika ukumbi wa diamond jubilee uliopo upanga Dar es salaam, pamoja na uzoefu wangu lakini pia malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya wasomeshaji wa Qur an juu ya hali zao za kimaisha !, hapo ndipo nilipopata wazo la kukuandikia barua ya wazi na Al hamdulillahi siku imefika.

Ninaamini kama mawazo haya yatazingatiwa basi maisha ya wasomeshaji wa Qur an yatabadilika na hakutakuwa na malalamiko tena wala minung'uniko juu ya maisha magumu wanayopitia walimu wetu.

Kwanza kabisa ninaiomba ofisi yako ya mufti ipitishe azimio la kuua na kufuta kabisa mfumo wa kizamani (usio rasmi) wa utoaji wa elimu ya kiislamu yaani hizi madrasa zilizozagaa mitaani kila kona. Sio kila mtu anaweza kuwa mwalimu, ifahamike kuwa ualimu ni fani na katika zama zetu ni fani ya kusomewa kabisa.

Pili, Taasisi za kiislamu zichukue jukumu la msingi la utoaji wa elimu ya kiislamu. Ziwepo taasisi zilizothibitishwa kiuwezo kama vile BAKWATA, AL HIKMA FOUNDATION, ISLAMIC FOUNDATION, nk. Na nikisema kiuwezo namaanisha kifedha, halafu taasisi hizi zichukue jukumu la utoaji wa elimu kupitia ujenzi wa markazi kubwakubwa.

hivyo basi elimu ya kiislamu itolewe huko, na ndani ya markazi hizo kuwepo na shule za kidunia ili mtoto apate huku na huku kwa vile elimu zote ni muhimu. Ifanyike kazi kubwa ili Markazi ziwepo kila mkoa na kila wilaya nchi nzima . Mzazi mwenye nia ya kuwa mwanae apate elimu ya dini atampeleka mwanae katika Markazi hizo na ikiwa hataki basi iwe juu yake na mola wake.

Markazi hizi zitakapojengwa watoto watakaoenda kusoma huko watalipa ada zenye kiwango stahiki tena stahiki kwelikweli ili ipatikane fedha ya kuendeleza elimu ikiwa ni pamoja na malipo ya mishahara ya walimu hao. walimu wa sasa wana maisha magumu kwa vile hakuna mfumo wa kuwatengenezea maisha safi, ndugu Mufti Uislamu sio kudhalilika, mashekhe wetu ni lazima tuwajengee mifumo mizuri na imara ili kuujenga uislamu.

Tatu, uandaliwe utaratibu wa recruitment wa waislamu wenye elimu na nia ya ualimu wapelekwe kwa udhamini pale Chuo kikuu cha Waislamu Morogoro, wafundishwe falsafa ya ualimu na mambo mengine ya kuwaongezea ujuzi wa kile wanachokifundisha, halafu hao ndio wapatiwe nafasi ya kuajiriwa katika markazi hizo kama walimu wa aidha Qur an ama fiq h ama somo lingine lolote la kiislamu. huku mtaani mtu akimaliza tu raabiu ibtidai(darasa la nne la dini) basi tayari anataka kuanzisha madrasa na huko atatembeza bakora ajabu haina kifani, hii sio sawa.

Ikiwa mtu atashindwa kusoma kwa kiwango cha kuwa mwalimu wa ngazi husika basi apewe jembe akalime, na elimu yake akaitumie kuitafuta akhera na sio kujivisha tu vazi la ualimu.

Mfano wa markazi hizi ni pamoja na;
Ilemela Islamic Seminary (Nimesoma hapa)
Al hikma schools na nyingine chache sana.

Maisha duni yanayoonekana kwa wasomeshaji wengi wa elimu ya kiislamu ni kwa sababu ya mfumo wa kizamani wa kielimu ambao bado tumeung'ang'ania. tunapaswa kuondokana nao kwa kuuboresha, na uboreshaji wake ni kuua mfumo huo wa kizamani na kuzivisha taasisi zenye uwezo wa kazi hiyo ya utoaji elimu, lakini pili, pafanyike juhudi za kimaksudi za kusomesha falsafa ya ualimu kwa waalimu wenye nia na kwa dhamana ya kifedha, watakaosoma wakaajiriwe kwenye taasisi hizo na mwisho kabisa wasioweza kusoma wakafanye shughuli zingine za kimaisha na sio ualimu holela.

Wako katika uandishi
Yusufu R H Sabura
0750883466/0717934194
 
Back
Top Bottom