SoC04 BASATA okoeni sanaa ya Tanzania

SoC04 BASATA okoeni sanaa ya Tanzania

Tanzania Tuitakayo competition threads

positiveatittude

New Member
Joined
Aug 20, 2022
Posts
2
Reaction score
1
Baraza la sanaa la Tanzania linahusika kwenye ukaguzi wa maudhui ya sanaa pamoja na utoaji wa hakimiliki ya kazi za sanaa za wasanii wa Tanzania. Baraza hili limekua likijitahidi kuhakikisha maudhui yanayowasilishwa kwenye jamii hayavunji maadili ya kitanzania kwa kufungia kazi za sanaa zinazoonekana kukiuka maadili.

Lakini miaka inavyozidi kwenda ndiyo hivyo sanaa inazidi kubadilika, Si vibaya kwa sanaa kubadilika lakini pia sio jambo zuri iwapo mabadiliko hayo yanaenda kinyume na maadili ya jamii husika. Sanaa ya Tanzania hasahasa upande wa kuimba (bongoflava) na ucheshi inakua kwa kasi lakini jambo la kusikitisha ni kwa namna sanaa hiyo zisivyoheshimu maadili ya kitanzania.

Wasanii wengi wamekua wakiimba nyimbo zenye lugha kali ikiwemo matusi ya waziwazi. Nyimbo nyingi zimekua zikihamasisha ngono, mapenzi kinyume na maumbile, matumizi ya vilevi na madawa ya kulewa kama bangi. Isitoshe kwenye upande video imekua ni jambo la kawaida kumdhalilisha mwanamke kwa kumvalisha nguo zinacha sehemu kubwa ya miili yao wazi. Hii husababisha watu kutoweza kutazama video hizo kwenye mjumuiko wa familia kwani zinaleta aibu sana.

Msanii ni kioo cha jamii, hii inamaanisha anayoyafanya masanii yanaakisi yale yanayofanyika kwenye jamii husika. Lakini msanii ana uwezo wa kuijenga au kuibomoa jamii kutokana na maudhui anayoyawasilisha kwao. Hii ni kutokana na watu wengi kwenye jamii huwafuatilia kwa ukaribu wasanii na wengine hufikia mpaka kuigiza maisha yao. Hii imepelekea wasanii kutumiwa na wanasiasa kipindi cha kampeni ili kuwavuta watu wengi kwenye mikutano.

Lakini hali inazidi kua mbaya kwenye jamii kutokana na wasanii wengi wa maigizo, vichekesho na muziki kujali zaidi soko la maudhui yao bila kufikiria wanachokiwasilisha kina mchango gani jamii husika. Hali hii inapelekea kuharibika kwa taswira ya sanaa nchini na kuonekana kama ni mojawapo sekta inayoharibu maadili kwenye jamii.

Hivi sasa nchini kutokana na ongezeko la ukosefu wa ajira kwa vijana, wengi wao wamegeukia kwenye sanaa ili kuweza kujiingizia kipato. Lakini changamoto iliyopo ni namna wanavyowasilisha sanaa yao kwenye jamii. Wamekua wakidiriki kufanya chochote ilimradi sanaa yao iwafikie watu wengi. Jambo hili limesababisha wasanii kutengeneza kazi zilizo chini ya kiwango na zisizo na maadili, jambo ambalo huweka hatarini kizazi cha sasa na kinachokuja iwapo wataendelea kufumbiwa macho.

Kwa kinachoendelea kutendeka kupitia sanaa, ni vyema BASATA ikajitafakari na kuja na njia zitakazoweza kuirudisha sanaa kwenye mstari mzuri.

Yafuatayo ni baadhi ya yanayoweza kufanywa na BASATA ili kuhakikisha sanaa inatumika kuelimisha jamii;
  • Kuandaa semina za mara kwa mara na wasanii
BASATA iwe na utaratibu wa kuandaa semina maalumu kwa wasanii na wanaoandaa maudhui ya sanaa zitakazokua zikifanyika kila baada ya kipindi cha muda fulani. Semina hizi zitakua ni kwaajili ya kujadili changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wasanii na waandaaji wa maudhui ya sanaa na kuwapa elimu waasanii namna ya kufanya sanaa ya kistaarabu yenye kujenga jamii na sio kuibomoa.
  • Kutoa tuzo za heshima kwa wasanii wanaowasilisha kwenye jamii maudhui ya kuelimisha.
Wapo wasanii wanaotunga kazi za sanaa zenye kuelimisha na kuijenga jamii, hivyo ni vizuri BASATA kua na utaratibu wa kuwatambua na kuwapa tuzo za heshima. Njia hii itawaongezea nguvu ya kuendelea kuelimisha jamii na kuwafanya wasanii wengine wafuate njia yao ya kufanya sanaa inayoelimisha jamii.

  • Kufanya ukaguzi wa kazi za sanaa kabla ya kuwasilishwa kwenye jamii pamoja na kuzipanga kwenye makundi maalumu ya umri unaoruhusiwa kupokea sanaa hiyo.
Kama ilivyo kwa upande wa filamu nchini zinakaguliwa na bodi ya filamu na kupewa viwango vya ubora na kupangiwa umri utakaoruhusiwa kutazama filamu hiyo basi iwe pia kwenye sanaa nyingine. Ikiwa kazi hiyo ya sanaa haitakua na viwango vya kuwasilishwa kwa watoto, isiruhusiwe kufanyika hadharani au kwenye vipindi vya mchana kwenye vituo vya redio na televisheni. Hii itawaepusha watoto kukumbana na maudhui yasiowafaa na hivyo kuepusha kuharibu maadili ya watoto.
  • Kuhakikisha kila aina ya sanaa inakua na bodi yake.
Kama ilivyo kwenye filamu wana bodi ya filamu pia sanaa nyingine kama muziki, uchoraji na nyinginezo zinaunda bodi zao. Hii ni kwaajili ya kurahisisha ufuatiliaji wa kazi wa wasanii wao na kuhakikisha hazivunji maadili ya Kitanzania. Itaepusha BASATA kubeba mzigo mkubwa na kufanya kazi endapo malalamiko yatafiki9shwa kwao kutoka kwenye bodi hizo.

Kwa kumalizia napenda kusisitiza kwamba sanaa ni mwalimu wa jamii, inaweza kuharibu jamii kama ikitumika vibaya lakini pia inaweza kujenga jamii kama ikitumika vizuri. Jambo lolote hufikia jamii kwa haraka zaidi endapo likiwasilishwa kupitia sanaa. Sanaa inahitaji kipaji, ukosefu wa kipaji huwafanya wasanii watumie mbinu zozote ili kuwavuta mashabiki bila kujali maadili ya jamii husika. Lakini bado nafasi ipo ya kuilinda na kuimarisha sanaa ya Tanzania na kuhakikisha haivurugi maadili yetu. Sanaa ikiboreshwa itatumia kama mwalimu wa mengi, itatumika kuhamasisha mengi mazuri, itatumika kuvuta watalii pia itatumika kuwaonya wanaotoka nje ya mstari wa maadili na wanaofanya uonevu kwa wengine.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom