Biashara Tano(5) Unazoweza Kuanza Kufanya Wakati Bado Umeajiriwa, Na Kwa Mtaji Kidogo

Biashara Tano(5) Unazoweza Kuanza Kufanya Wakati Bado Umeajiriwa, Na Kwa Mtaji Kidogo

Makirita Amani

JF-Expert Member
Joined
Jun 6, 2012
Posts
1,915
Reaction score
3,422
Ajira sio salama tena kama ilivyokuwa zamani. Kwa sasa maisha yamekuwa ghali huku kipato cha ajira kikiwa hakitoshelezi. Hii inawafanya waajiriwa wengi kufikiria kuingia kwenye biashara.

Lakini pia kuingia kwenye biashara sio rahisi kama ambavyo mtu anaweza kuona. Kuna changamoto zake nyingi na kama ndio unatokea kwenye ajira huku ukiwa na mahitaji makubwa ya fedha, sio rahisi kuacha ajira na kuingia kwenye biashara moja kwa moja.

Kushindwa kuingia kwenye biashara moja kwa moja sio mwisho wa wewe kufanya biashara. Inawezekana kabisa ukawa na biashara huku unaendelea na kazi yako unayofanya sasa.
Leo kwenye mtandao huu wa NAPENDA BIASHARA utajifunza biashara tano unazoweza kufanya wakati bado unaendelea na ajira yako.


  1. Biashara ya mtandao(network marketing).
Hii ni biashara ambayo unaweza kuifanya kwa muda mchache kwa siku au kwa wiki na ukaanza kujitengenezea kipato hata kama kwa sasa bado umeajiriwa. Kupitia biashara hii wewe unakuwa msambazaji wa huduma au bidhaa kwa njia ya kuwaambia wengine uzuri wa bidhaa au huduma zile na wanaponunua wewe unapata kamisheni. Kuna faida nyingine nyingi kupitia biashara hii kama kuweza kutengeneza timu kubwa na ikakuongezea kipato kikubwa.

Kama unataka kufanya biashara ya aina hii jifunze kwanza kwa undani kwa kujisomea wewe binafsi kisha chagua kampuni unayoweza kufanya nayo na jiunge ili uanze kujenga biashara yako. Uzuri wa biashara hii ni kwamba kwa sehemu kubwa utafundishwa mbinu za kuweza kuendesha biashara yoyote.


  1. Kuwa mkufunzi binafsi.
Kama kuna ujuzi wowote ambao unao, basi jua kuna watu ambao pia wanauhitaji. Wewe unaweza kuwa mkufunzi binafsi kwa ule ujuzi ambao unao. Kwa mfano kama wewe ni mwalimu, basi unaweza kufanya biashara ya kuwa mwalimu binafsi kwa watoto ambao wazazi wao wana uwezo wa kulipia gharama ya juu kidogo. Wewe unakwenda kuwafundisha watoto hao majumbani kwao. Unatoa huduma nzuri na unahakikisha watoto wanaweza kufaulu vizuri.
Kama unataka kufanya biashara hii, chagua watoto wa aina gani unataka kufundisha, kisha angalia katika watu unaowafahamu ni wangapi wenye watoto wanaoweza kufaidi huduma zako. Tafuta wachache wa kuanza nao hata kwa gharama za chini, fanya nao kazi vizuri na kama watafurahia waombe wazazi wao wakutambulishe kwa marafiki zao ambao wanaweza kufaidika na huduma unayotoa.


  1. Ushauri wa kitaalamu.
Kwa kazi yoyote ambayo unaifanya, wewe una utaalamu fulani. Utaalamu huo unaweza kuwasaidia watu wengi sana ambao hawajui pa kuupata. Kama wewe ni daktari, unaweza kuwa unawapa watu ushauri kuhusu afya zao, wapo wengi sana wanaohitaji ushauri ila hawajui kama unaweza kupatikana, tena kwa bei rafiki kwao. Kama wewe ni mwanasheria uliyeajiriwa, unaweza kuwa unatoa ushauri wa kisheria kama biashara yako ya pembeni.
Kama unataka kuingia kwenye biashara hii ya kutoa ushauri wa kitaalamu, jua ule utaalamu ambao unao, kisha angalia ni watu gani wanaweza kunufaika na ushauri wako kisha tafuta wachache wa kuanza nao. Endelea kutoa huduma hii ya ushauri ukilenga kujenga jina na baadae unaweza kutoza gharama au kuongeza gharama kama ulianza na kidogo.


  1. Huduma za kitaalamu.
Hii ni tofauti na ushauri wa kitaalamu, hapa unatoa huduma kabisa. Kwa mfano kama wewe ni mhasibu uliyeajiriwa, unaweza kuanzisha biashara yako ya pembeni ya kutoa huduma za kihasibu kwa biashara ndogo ndogo. Wafanyabiashara wengi wadogo hawawezi kumudu gharama kubwa za kupata huduma za uhasibu, kama wewe unaweza kuwaandalia mahesabu yao kwa gharama ambayo wanaweza kuimudu, unaweza kutengeneza biashara kwenye eneo hilo. Kama wewe ni mwanasheria unaweza kutoa huduma za kisheria kwenye jamii kwa gharama ambazo ni rafiki. Kwa mfano kuandalia wenye nyumba mikataba ya upangishaji, kuandalia wafanyabiashara wadogo mikataba ya uajiri, kuwaandalia watu mikataba ya kibiashara na kadhalika. Kuna taasisi nyingi zinafanya hivi lakini zinawafikia wateja wakubwa tu, wewe unaweza kuanza na wateja wadogo na ukajenga biashara yako hapo.
Kama unataka kuingia kwenye biashara hii ya huduma za kitaalamu, jua ile huduma ambayo unaweza kutoa na anza na wateja ambao hawajafikiwa na watoa huduma waliopo. Tengeneza jina lako kwa kutoa huduma nzuri na kuza biashara yako kuanzia hapo.


  1. Anzisha na endesha blog.
Blog unaweza kuitumia kwa biashara zote ambazo tumejadili hapo juu. Unaweza kuitumia kwa kutoa ushauri wa kitaalamu. Kama wewe ni daktari unaandika kuhusu mambo ya afya. Kama wewe ni mtaalamu wa rasilimali watu unaweza kuitumia kuandika kuhusu sifa za kuajiriwa, kudumu kazini, kupandishwa cheo na mengine mengi. Kupitia yale unayoandika unaweza kutengeneza hadhira ambayo inakufuatilia na baadae ukageuza blog yako kuwa biashara kwa kutoza huduma unazotoa, kuweka matangazo au kuuza vitu vyako vingine.

Biashara hizi tano tulizojadili hapa unaweza kuanza leo hata kama huna fedha mfukoni. Kazi kubwa kwako ni kuanza na kutafuta mteja. Na uzuri ni kwamba popote ulipo umezungukwa na wateja, sema wengi hawajui kama huduma fulani inapatikana.

Kwa ushauri zaidi kuhusu kuanzisha na kukuza biashara yako piga simu 0713 666 445.


Kupata kitabu SIRI 12 ZA KUPATA WAZO BORA LA BIASHARA, wasiliana nami na utatumiwa kitabu.


PENDA BIASHARA, JIFUNZE BIASHARA.
 
Asante sana Mpwa wangu huwa nakusoma vyema sana. Tatizo vijana na Wazee wote wamekimbilia na kushikilia Siasa! Hapa utaona wachangiaji wachache tu
 
Mkuu natamani biashara ya duka niaje? Naweza fanyaje kufaidika nayo?
 
Blog siku hizi zinapungua umaarufu baada ya WhatsApp kushika kasi. Jambo linarushwa WhatsApp likiwa na picha hadi video tena muda huohuo wewe wa blog mpaka labda nusu saa ndio uliweke kwenye blog. Hata blog visitors wamepungua sana
 
Asante sana Mpwa wangu huwa nakusoma vyema sana. Tatizo vijana na Wazee wote wamekimbilia na kushikilia Siasa! Hapa utaona wachangiaji wachache tu

Asante sana mkuu. Taratibu taratibu tutaelewa tu, maana game imekuwa tight kila kona, na matumaini ya watu kwenye siasa yatakapofika kikomo hakutakuw ana namna nyingine zaidi ya kuweka juhudi na maarifa kwneye kazi na biashara.
 
Blog siku hizi zinapungua umaarufu baada ya WhatsApp kushika kasi. Jambo linarushwa WhatsApp likiwa na picha hadi video tena muda huohuo wewe wa blog mpaka labda nusu saa ndio uliweke kwenye blog. Hata blog visitors wamepungua sana

Inaonekana hujui tofauti ya vitu hivi viwili ulivyolinganisha hapo juu. Nakusihi ufanye utafiti kidogo au ujishughulishe japo kujua zaidi ndipo useme kipi ni kipi.
Nakubaliana na wewe kwamba wasap ina umaarufu, lakini ni tofauti kabisa na blog.
Na pia naweza kusema kwamba kama unataka kusisimua watu tumia wasap kama unataka kutengeneza fedha, tumia blog.
 
Back
Top Bottom