Katika kipindi cha miaka minne iliyopita akiwa madarakani rais Biden, msimamo wake kuhusu Afrika ulikuwa una uafadhali kuliko ule wa mtangulizi wake Donald Trump, lakini ahadi nyingi bado zimebaki kuwa "maneno matupu." Katika mkutano wa kilele kati ya Marekani na Afrika uliofanyika mwaka 2022, Marekani ilitangaza kuwekeza dola za kimarekani bilioni 55 katika miaka mitatu inayofuata ili kuunga mkono "Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063," huku Biden mwenyewe akiahidi kutembelea Afrika mwaka uliofuata.
Lakini hali halisi ni kuwa kati ya dola hizi bilioni 55, ni dola bilioni 15 tu zilizotengwa kwa ajili ya miradi mipya, huku dola bilioni 40 zikiwa ni kwa ajili ya "kuzindua upya" mipango ya zamani ya Marekani barani Afrika. Aidha, kiasi hicho kikubwa cha pesa, ambacho kinaonekana kuwa cha kuvutia, hakijawanufaisha watu wa Afrika moja kwa moja. Badala yake, sehemu kubwa ya fedha hizo zimetumika kuimarisha ushawishi wa Marekani kupitia mafunzo na semina mbalimbali, na hata kuunga mkono makundi ya kupinga serikali za nchi za Afrika.
Ni wazi kwamba nia ya Marekani kuwekeza Afrika inalenga zaidi mambo ya siasa kuliko uchumi. Kwa Biden yeye binafsi, pia hajatimiza ahadi ya kufanya ziara barani Afrika, mpaka mwaka huu, ambapo ziara yake ya Angola, awali iliyopangwa kufanyika mwezi Oktoba, iliahirishwa hadi wiki hii kutokana na janga la kimbunga lililotokea Marekani.
Kuhusu safari hii ya Biden nchini Angola, lengo kuu ni kuhimiza maendeleo ya urithi wake wa kisiasa yaani mradi wa "Ushoroba wa Lobito." Mradi huu, ambao ulitangazwa na Marekani kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa Kundi la Nchi Saba (G7) Mei mwaka 2023, unahusisha ujenzi wa reli inayounganisha Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Zambia, na unatajwa kuwa ni uwekezaji mkubwa zaidi wa Marekani kuhusu sekta ya reli barani Afrika. Kwa mtazamo wa jumla, ujenzi wa reli barani Afrika ni jambo linaloweza kunufaisha watu wa bara hilo, lakini hali halisi ni kuwa mradi huo ni hadaa tu.
Kwanza, "Ushoroba wa Lobito" si dhana mpya. Reli kuu ya mradi huo ilijengwa mwanzoni mwa karne ya 20 na wakoloni wa Kireno, lakini iliharibiwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Angola miaka ya 1970. Baadaye, kampuni ya China ilichukua miaka minane kuijenga upya reli hiyo, na kuiita Reli ya Benguela. Hivyo, huo Ushoroba wa Lobito ni karibu sawa na Reli ya Benguela. Biden sasa anajaribu kutumia jina jipya la mradi huo ili kuonyesha mchango wa Marekani katika miundombinu ya Afrika, jambo ambalo ni la kudanganya watu.
Pili, lengo kuu la Marekani katika mradi wa Lobito ni kurahisisha usafirishaji wa madini muhimu kutoka sehemu za ndani za Afrika kwenda bandari za magharibi mwa Angola kwa ajili ya kuuzwa nje. Biden hakuficha kusema kuwa huu ni mkakati wa kupunguza ushawishi wa China katika sekta ya madini barani Afrika. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na hitaji la nishati mbadala, umuhimu wa kimkakati wa Afrika kama bara lenye maliasili nyingi (asilimia 30 ya madini ya dunia) umeongezeka sana.
Badala ya kusaidia maendeleo ya bara hilo, Marekani inachochea mvutano wa siasa za kijiografia barani Afrika, na kujaribu kudhibiti madini muhimu ili kudumisha umwamba wake wa kiuchumi duniani. Hata hivyo, nia hii mbaya ya Marekani tayari imegunduliwa na nchi za Afrika. Kabla ya ziara ya Biden, Rais João Lourenço wa Angola alisema katika mahojiano kuwa Angola haitachagua upande kati ya Marekani na China, akiashiria kuwa ziara hii ya Biden haitayumbisha uhusiano wa Angola na China.
Tatu, jambo linalotiliwa shaka zaidi kuhusu ziara hii ni kwamba Biden anakaribia kuondoka madarakani baada ya mwezi mmoja hivi. Kutokana na mvutano wa kisiasa ndani ya Marekani unaosababisha ukosefu wa mwendelezo wa sera na sintofahamu kubwa, ni wazi kuwa athari ya Biden kwa serikali ya awamu ijayo itakayoongozwa na Donald Trump itakuwa ndogo sana.
Mbali na kwamba Trump alitoa kauli nyingi zinazodhalilisha Afrika katika kipindi chake cha urais na kushikilia sera ya kutetea maslahi ya Marekani kwanza, ni vigumu sana kutabiri hali ya utekelezaji na ufanisi wa mradi wa Ushoroba wa Lobito chini ya utawala wa Trump. Hili ni swali kubwa ambalo hata Biden mwenyewe huenda hana majibu.