KwetuKwanza
Member
- Mar 13, 2023
- 82
- 150
Habari za wakati ndugu wana Jukwaa,
Kwa muda sasa nimekuwa nafuatilia hii changamoto kwa wajawazito ambayo wanakumbana nayo wakati wa kujifungua katika vituo vya Afya na Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi Wilaya ya Bariadi hapa
kwenye mkoa wetu wa Simiyu.
Nimekutana na changamoto hizi kwenye Kituo cha Afya Ngulyati, Kituo cha Afya Muungano na Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi (Somanda).
Tena kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Mji ndiyo imekithiri zaidi, kwani malalamiko ambayo nimekutana nayo na mengi zaidi na hakuna kiongozi ambaye ameyafanyia kazi.
Wajawazito kwenye hii Wilaya wanapata tabu sana hasa wakati wa kijifungua, tabu hii inawapata wale ambao wanajifungua kwa njia ya upasuaji (operation).
Wakati Serikali kila siku inajinasibu kuwa huduma za Afya kwa wajawazito ni bure, hali ni tofauti kwa wajawazito wa Simiyu hasa Bariadi ambao wanapata huduma kwenye hivyo vituo.
Wajawazito hawa wakati wa kujifungua kwa njia ya upasuaji, utakiwa kununua vifaa vyote ambavyo vinahitajika wakati wa kufanyiwa zoezi hilo.
Baadhi ya vifaa hivyo ni mipira ya kuvaa mikononi (glaves) sindano za kushonea nyuzi, vifaa vyote vinavyohitaji kwa ajili ya kushona, dawa zote zinazohitajika kwa ajili ya kutibu kidonda.
Kwa kifupi ni kuwa mjamzito anapokwenda kujifungua kwa njia ya upasuaji, kitu ambacho anapata bure ni ule utalaamu wa madaktari na wahudumu wengine, lakini vifaa vyote vinavyotumika anatakiwa kununua.
Mama mmoja ambaye nilikutana naye Hospitali ya Halmashauri ya Mji, yeye alikuwa na mtoto wake ambaye alijifungua kwa njia ya upasuaji, anasema baada ya kufika hospitali aliandikiwa kwenda duka la dawa kununua vifaa mbalimbali.
Mama huyo anasema alitumia takribani Sh 200,000 kuweza kununua vifaa vyote, anasema kuwa alishangaa kuambiwa anunue vifaa ambavyo vinatakiwa kuwepo hospitalini hapo.
Anasema alipouliza watu wengine ambao walikuwa tayari wamepata huduma, walimwambia hata wao walinunua vitu hivyo.
Nimejaribu kufuatilia maeneo mengi, wajawazito wakati wa kwenda kliniki kuna vifaa huwa wanaambiwa kwenda navyo siku ya kujifungua, vifaa hivyo ni pamoja na kanga, nguo za mtoto, sabuni, pedi/pamba.
Lakini mjamzito anashauriwa kwenda na pesa kidogo za kujikimu, kuandaa usafiri wa kukupeleka hospitali na wakati wa kuruhusiwa, lakini kumwandaa msaidizi.
Mbali na hivyo kuna baadhi ya vifaa ambavyo mjamzito anatakiwa kuandaa ikiwa itatokea dharula (niweka picha ya hivyo vifaa) vifaa hivyo ni wembe, glaves, kifaa cha kufungia kitovu pamoja na mpira.
Vifaa hivyo vinatajwa kama ni dharula, ikiwa hospitalini kutatokea tatizo lolote la kuishiwa kwa vifaa hivyo.
Sasa kinachokea kwenye hizo hospitali, wajawazito wanaongezewa vifaa vingine zaidi hasa wale ambao wanajifungua kwa upasuaji, vifaa vyote vinavyohitajika wakati zoezi hilo utakiwa kuvinunua.
Vifaa hivyo kwa pamoja ukienda kwenye duka la dawa, nimebaini kuwa kila mjamzito utumia siyo chini ya Sh. 80,000 hadi 100,000 ili kuweza kuvipata vifaa vyote hivyo.
Hata hivyo ambavyo mjamzito anatakiwa kuwa navyo kwa dharula, wengi wanajiuliza kwa nini vikinunuliwa vinatumika hivyo vya wajawazito na siyo kwamba vinaanza kutumika vya hospitali.
Mbaya zaidi ni huyu mjamzito anayejifungua kwa upasuaji, utakiwa kununua dawa zote ambazo zinahitajika kwa ajili ya kuponesha kidonda mara baada ya huduma kukamilika.
Dawa hizo nazo gharama zake siyo chini ya shilingi 20,000 hadi 50,000, hali hiyo inaonyesha vituo hivi vya kutolea huduma za Afya havina dawa za kumeza kwa ajili ya akina mama wajawazito ambao wanajifungua kwa njia ya upasuaji.
Gharama za chini kabisa kwa mjamzito ambaye anajifungua kwa upasuaji, katika Wilaya ya Bariadi anatakiwa kuwa na kiasi ambacho hakipungui sh, 200,000 (laki mbili) ili aweze kupata huduma kwenye hospitali za serikali.
Changamoto nyingine ambayo nimekutana nayo na wananchi wanailalamikia hasa wanawake kwenye hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwa wajawazito ni huduma mbaya kwao ambazo zinatolewa na wahudumu.
Familia moja ilimleta shemeji yao kujifungua, walivyofika hospitali wahudumu hawakuwajali hata kidogo, bila ya hata kumpima semeji yao, baada ya kufika waliambiwa moja kwa moja mpeleke huyo chumba cha upasuaji.
Walipohoji mbona haraka hivyo na mjampima kujua kama anahitaji huduma hiyo, basi walijibiwa vibaya, mmoja wa ndugu akamtafuta daktari anayefahamiana naye hapo hopitali ndipo akamuomba ampime kwanza shemeji yake.
Baada ya kumpima, mjamzito huyo aligundulika kuwa haitaji huduma ya upasuaji bali anaweza kujifungua kawaida.
Wahudumu katika hospitali hiyo wanalalamikiwa sana na wagonjwa, Eneo la wajawazito ndiko hatari tupu, hakuna anayejali hata kidogo, hakuna huduma rafiki hata kidogo, wahudumu wanalalamikiwa huduma mbaya, lugha chafu na kutojali wagonjwa.