Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,833
- 1,301
BILIONI 11 ZIMETENGWA UJENZI SHULE 10 ZA MICHEZO
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo chini ya Makamu Mwenyekiti Mhe. Musa Sima imepokea na kujadili taarifa kuhusu maendeleo ya Sekta ya Michezo ikiwemo ujenzi wa Shule 56 za michezo nchi nzima, ambapo umeanza na Shule 10.
Akiwasilisha taarifa hiyo kwenye Kamati Oktoba 22, 2024 Bungeni Jijini Dodoma, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameeleza kuwa, ujenzi na Ukarabati wa miundombinu katika Shule hizo 10 ambazo ni Shule ya Sekondari Dodoma, Tabora Wavulana, Ufundi Tanga, Ikwiriri, Kiomboi Mpya, Ufundi Mtwara, Dkt. Damas Ndumbaro pamoja na Babati tayari zabuni ya kumpata Mkandarasi imekamilika na atapatikana mwezi Novemba.
Amesema, ujenzi na ukarabati huo utahusisha Viwanja vya Soka, Mpira wa kikapu, Wavu, Mpira wa Pete, michezo ya ndani, uwanja wa tenis,bwawa la kuogelea la viwango vya Olimpiki na vyumba vya kubadilishia nguo.
Kwa upande wa matumizi ya Fedha za Asilimia 5, zinazotokana na michezo ya kubahatisha, Mhe. Ndumbaro ameeleza kuwa, Mfuko wa Maendeleo ya Michezo kupitia Baraza la Michezo la Taifa umepokea Shilingi Bilioni 7.2 tangu mwaka 2021/ 22 hadi 2024/25 ambacho kimesaidia kuwezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa AFCON 2027, kuanzisha Mfumo wa usajili kidigitali, Uratibu wa mashindano ya CHAN 2025 na AFCON 2027, kutoa mafunzo kwa Wataalam na makocha wa michezo kutoka Vyama na Mashirikisho ya Michezo.
Wakichangia taarifa hiyo, Wajumbe wa Kamati wameelekeza wizara kusaka vipaji vya michezo hasa soka katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuimarisha timu ya taifa, ambapo pia wameshauri Timu ya Ngorongoro Heroes kupata malezi mahususi kwa ajili ya AFCON 2027.
Aidha, wameagiza kuharakishwa kwa mchakato wa kuanza kwa ujenzi wa uwanja wa mpira wa Dodoma ambao utatumika AFCON 2027, pamoja na matumizi ya VAR kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.