Baada ya kusikitika na kunung'unika, Seif akawageukia wananchi wake na kuwauliza nini kifanyike. Mawazo mengi yalitolewa. Wengine wakipendekeza kuhama, wengine wakisema waanzishe vita na mawazo mengine mengi. Sokwe mmoja mzee kwa jina Uswege akasimama na kutoa maoni yake, alisema. "Mi naona kabla ya kufikiria ni jambo gani tutafanya kwanza tumuadhibu huyu msaliti, tukomeshe kwanza jambo hili. Tumpelekee mkia wake!" "Kweli kabisa, kweli kabisa." zilisikika kelele kubwa sana. "Tumpelekee kia lake, tumpelekee kia lake," alianza kuimba Uswege. Sokwe wote wakaitikia.
Tumpelekee kia lake, tumpelekee.
Hata kama anaoga,
Rumpelekee kia lake tumplekee.
Hata kama amelala,
Tumpelekee kia lake, tumpelekee.
Hata kama anakula,
Tumpelekee kia lake, tumpelekee.
Basi hapo mambo yakafanyika haraka haraka, mkia wa Binti Sokwe ukaletwa. Maandamano makubwa yakaanza kuelekea kwa Binti Sokwe huku wimbo huo ukiimbwa kwa sauti kubwa sana. Muda huo Binti Sokwe alikuwa amekaa mezani na Maduhu wakila. Kadri sokwe wale walivyokuwa wanakaribia huku wakiimba, Binti Sokwe akaanza kuona mabadiliko. Kwanza mwili ulianza kumuwasha, mara nywele zikaanza kumuota miguuni. Walivyozidi kukaribia, ndivyo nywele nazo zilivyozidi kuota. Mara mkia nao ukaanza kuota, hata hakuweza kukaa vizuri. Maduhu akashangaa kuona mkewe akihangaika kitini.
Sasa sauti za sokwe wanaoimba zikaanza kusikika, nywele zikamfika Binti Sokwe usoni. Maduhu akaruka kitini akimwaga chakula, akasimama amepigwa na butwaa. Kelele za sokwe zikazidi kukaribia, ni kama walikuwa nje ya nyumba ya Maduhu. Binti Sokwe akainuka na kukimbia, huku nyuma mkia wake wote ukiwa umemsimama. Hakuonekana tena hadi leo.