Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wananchi wa Nyamongo na Mkoa wa Mara kwa ujumla kufanya kampeni za kistaarabu na kujitokeza kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Dkt. Biteko ameeleza kuwa maendeleo hayaletwi kwa matusi wala kuvunjiana heshima na kuwa wananchi hao washinde ubaya kwa wema. Aidha, Dkt. Biteko amefika eneo hilo kwa lengo la kuwaomba wananchi wa Nyamongo wachague watu ambao wataungana na Serikali katika kuwaletea maendeleo.
Dkt. Biteko ameyasema hayo wakati akifungua kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mkoa wa Mara zilizofanyika katika Mji wa Nyamongo Wilaya ya Tarime.
“Mwaka huu tuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni uchaguzi mkubwa wa kumchagua mtu atakayejua hali na maisha ya watu katika ngazi ya mtaa na ambaye atabeba shida za watu na kuzitatua,” amesema Dkt. Biteko.