Huyu Kamanda ni mwongo manake katika maelezo yake anasema kwamba watu 7 wameogelea kutoka sehemu boti ilipoungua hadi wakafika juu na walikuwa hai,, sasa hivi jamani boti inaweza kushindwa na watu ambao waliogelea na kufika wakiwa hai kuliko hilo Boti lao? hawajaenda popote waongo kabisa!! Eti asubuhi wakenda tena ,wanenda kutafuta chaza?
_________________________________________
Date::4/15/2009
Watu 20 wahofiwa kufa baharini baada ya boti kushika moto
Burhani Yakub,Tanga na Salim Said, Dar
ZAIDI ya watu 20 wanasadikiwa kufa maji katikati ya bahari ya Hindi na wengine 13 kuokolewa baada ya boti walilokuwa wakisafiria kutoka Tanga kuelekea Kisiwani Pemba kushika moto.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Nyakoro Sirro, ajali hiyo ilitokea saa 7.00 usiku wa kuamkia jana katikati Bahari ya Hindi wakati.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinasema boti hiyo ambayo ni mfano wa jahazi ililopata ajali hiyo ni la kubeba mizigo linalojulikana kwa jina la Amana Pemba, ambayo hufanya safari zake kati ya Pemba ,Unguja, Dar es saalam na Tanga.
Kamanda Siro alisema boti hilo lilikuwa na kibali cha kuondoka katika Bandari ya Tanga saa 11.00 jioni kwenda Pemba, lakini haikuondoka hadi saa 3.30 usiku ndipo ikaanza safari yake ya kuelekea Pemba likiwa na mizigo na abiria 40.
Kamanda Sirro alisema kwa mujibuwa taarifa alizopata, ajali hiyo ilisababishwa na godoro ambalo lilishika moto baada ya kugusa injini na kisha kulipukuka.
Alisema mmoja wa abiria waliokuwa ndani ya boti hiyo aliuona moto huo akapiga kelele na wengine wakaanza kutapatapa huku baadhi yao wakichupa majini ili kujiokoa.
Abiria mmoja alitupigia simu kututaarifu juu ya tukio hilo na kuomba msaada, ndipo Boti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ikaondoka usiku huo kwenda kuwaokoa, lakini ilipofika katikati ilishindwa kuendelea na safari kutokana mawimbi kuwa makubwa hivyo ikarejea Tanga, alisema Sirro.
Alisema abiria sita kati yao waliokolewa na jahazi lijulikanalo kwa jina la Amana Tanga likitokea Pemba kuelekea Tanga ambao waliwasilishwa jijini hapa jana alfajiri na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo.
Kwa mujibu wa melezo ya Sirro watu wengine saba wakiwamo wafanyakazi wa boti hiyo waliogelea na kufanikiwa kufika pwani katika eneo la Kigombe wakiwa hai.
Alisema jana alfajiri timu ya waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Jeshi la Polisi kutoka Bandari ya Tanga na kikosi cha Zimamoto viliondoka kwa boti kuelekea eneo la tukio kwa ajili ya uokoaji.
Abiria waliookoka katika ajali hiyo wamesema kuwa kuna uwezekano kuwa wenzao wengi wamekufa maji kwa kuwa waliwaacha wakitaptapa na wengine walishindwa kuogelea kutokana na kukosa nguvu.
Wenzetu wengi tu watakuwa wamekufa. Kama Boti ya uokoaji ya Bandari ya Tanga ingefika usiku ingewakoa lakini kama wameenda asubuhi watakuwa wamechelewa kwani kulikuwa na wanawake na watoto ambao hawakuwa na uwezo wa kuogelea kwa muda mrefu, alisema mmoja wa abiria hao ambaye alinusurika, Jumaa Idd Jumaa mkazi wa Chake chake, Pemba.
Hata hivyo, Kamanda Sirro aliwaambia waandishi wa habati kuwa atatoa taairfa kamili ya idadi ya abiria walikufa kikosi cha waokoaji kitakaporejea.
Jijini Dar es Salaam Salim Said anaripoti kuwa Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Hamad Rashid ametoa salamu za pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na famili za marehemu na walioathirika katika ajali hiyo iliyowaka moto baharini.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, Rashid alisema amepata mshtuko baada ya kupata taarifa za ajali hiyo na kwani katika boti hiyo kulikuwa na baba yake mdogo.